23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Taifa Stars kuivaa Zimbabwe Novemba 13

taif-stars

Na MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM

TIMU ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars’, imepata mwaliko kutoka Chama cha Soka cha Zimbabwe (Zifa) wa kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Zimbabwe Warriors utakaopigwa Novemba 13, mwaka huu jijini Harare.

Kikosi cha Taifa Stars kinachonolewa na  kocha, Charles Mkwasa, hakijafanikiwa kucheza mechi ya kujipima nguvu tangu kilipochuana na Nigeria Agosti 3, mwaka huu katika mchezo wa mwisho wa Kundi G wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon).

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas, alithibitisha kupokea mwaliko huo na kudai kuwa mwishoni mwa wiki hii Mkwasa atatangaza kikosi kitakachoingia kambini kujiandaa na mchezo huo.

“Tumeukubali mwaliko wa kucheza nchini Zimbabwe Novemba 13, mwaka huu, hivyo kikosi kitakachotangazwa kitaingia kambini kuanza maandalizi kabla ya kwenda jijini Harare,” alisema.

Mchezo huo ni muhimu kwa Tanzania ambayo mwezi uliopita ilizidi kushuka katika ubora wa viwango vya Shirikisho la Kimataifa (Fifa) na kushika nafasi ya 114, huku Zimbabwe ikiwa nafasi ya 110.

Taifa Stars inakutana na Zimbabwe baada ya kushindwa kujipima nguvu na Ethiopia mwezi uliopita katika mchezo uliopangwa kwa mujibu wa kalenda ya Fifa kutokana na vurugu zilizokuwa zikiendelea nchini humo.

Katika hatua nyingine, timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, imeingia kambini jana kuanza mazoezi ya siku saba kabla ya kwenda Korea Kusini Novemba 8, mwaka huu kushiriki mashindano ya timu za vijana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles