23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, June 16, 2024

Contact us: [email protected]

Taifa Stars kazi moja

>>Ndayiragije hakuna namna nyingine zaidi ya Kenya kupigwa

Na MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM

TIMU ya Taifa Tanzania, ‘Taifa Stars’,  leo itashuka dimbani kuumana na Kenya ‘Harambee Stars’, katika mchezo wa kuwania tiketi kufuzu fainali za  mataifa ya Afrika,  kwa wachezaji wanaocheza Ligi za ndani (Chan), utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Huo utakuwa mchezo wa pili kwa timu hizo kukutana katika mashindano mawili tofauti  yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja.

Awali zilikutana katika hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon), zilizofanyika nchini Misri.

Katika mashindano hayo, zilipangwa kundi moja na mabingwa, Algeria  na Senegal iliyomaliza nafasi ya pili.

Katika mchezo huo, Stars ilikubali kichapo cha mabao 3-2,  mbele ya Harambee Stars ambayo ilitoka nyuma na kuzawasisha kabla ya kufunga la ushindi. Mchezo huo uliochezwa  Juni 27, kwemye Uwanja wa Juni 30, jijini Cairo.

Mchezo huo ni muhimu kwa Stars kushinda,  ili kujiweka katika  mazingira mazuri ya kumaliza kazi ugenini katika mchezo wa marudiano utakaochezwa Agosti 4, jijini Nairobi, Kenya.

Lakini pia, Stars italazimika kupigana kwa nguvu,  ili kupata ushindi na  kuvunja uteja  kwa Harambee ambayo rekodi zinaonyesha imeshinda mara nyingi timu hizo zilipokutana.

Tizo hizo zimekutana mara 49 katika mechi za mashindano tofauti,  Kenya imeshinda michezo 21, sare 14 na Stars ikishinda 14.

Timu itakayoibuka mshindi wa jumla katika michezo hiyo miwili, itakutana na Sudan,  ambapo mbabe atatinga moja kwa moja hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Mara ya mwisho kwa Stars kufuzu CHAN ilikuwa mwaka 2009 , ambapo fainali hizo zilifanyika nchini Ivory Coast, Stars wakati huo ilikuwa ikinolewa na kocha Mbrazil, Marcio Maximo.

Katika kikosi cha sasa, kuna wachezaji wawili ambao walikuwepo Stars iliposhiriki fainali hizo kwa mara ya mwisho mika 10 iliyopita hawa ni beki mabeki, Erasto Nyoni na Kelvin Yondani.

Kuelekea mchezo,  Stars itakosa huduma ya kiungo wake,  Mudathir Yahya kutokana na kukosa ufiti, baada ya kuwa nje ya uwanja akiuguza majeraha ya kifundo cha mkuu ‘enka’, aliyoyapata wakati wa fainali za Afcon.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa muda wa Stars, Ettiene Ndayiragije  alisema amekiandaa kikosi chake kikamilifu ili kupambana na kupata matokeo mazuri dhidi ya Kenya leo.

Alisema amewafuatilia vizuri wapinzani wao hao na kubaini wanacheza soka la nguvu, hivyo amewapa mbinu za kutosha wachezaji wake za kuhakikisha wanashinda mchezo huo na kulipa kisasi cha kufungwa Misri.

“Hii ni nafasi yetu ya kulipiza kisasi baada ya kupoteza kule Misri ambako tulipotea kidogo tu, naamini kwa maandalizi tuliyofanya tutapata matokeo mazuri.

“Tutahakikisha tunacheza kwa nguvu na kasi pia, lakini pia nimewaandaa wachezaji kisaikolojia kupambana kwa ajili ya kuisaidia timu kushinda, tuna wachezaji wengi wazuri na wenye vipaji,  kikubwa mashabiki wajitokeze kwa wingi kutupa sapoti,” alisema Ndayiragije.

Mchezo huo utachezeshwa na  Brian Miiro (Uganda) ambaye amepewa jukumu la kusimamia na kutafsiri sheria 17, akisaidiwa na Ronald Katenya ambaye atakua msaidizi  wa kwanza, Lee Okello msaidizi wa pili na Alex Muhabi ambaye atakuwa kamshina wa mchezo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles