22.3 C
Dar es Salaam
Saturday, July 13, 2024

Contact us: [email protected]

Siasa, utawala wa sheria katikati ya Rotich kusimama kizimbani

Na MWANDISHI WETU

HABARI kubwa iliyotikisa nchini Kenya na duniani kwa ujumla wiki hii ni kukamtwa kwa aliyekuwa Waziri wa Fedha, Henry Rotich, na kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka 24 ikiwamo matumizi mabaya ya ofisi, kupanga udanganyifu na kushiriki kwa miradi pasipo kuwa na mipango.

Rotich anashitakiwa pamoja na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Kamau Thugge, na maofisa wengine 26 wa serikali. Miongoni mwa mashitaka yanayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha ni sakata la mabilioni ya ujenzi wa mabwawa ya Kimwarer na Arror yaliyopo kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Kufikishwa mahakamani kwa Rotich na wenzake ilikuwa suala la muda tu kwa sababu Machi 6 mwaka huu, waziri huyo wa zamani alifika mbele ya wapelelezi katika makao makuu ya Ofisi za Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) na kuhojiwa kwa siku nzima kuhusu mradi huo wa mabwawa. Rotich alitakiwa kueleza nini anachokifahamu kuhusu utata unaozunguka mradi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer.

Siku iliyofuta mawaziri wengine, Mwangi Kiunjuri (Kilimo), Peter Munya (Afrika Mashariki) na Adan Mohamed (Viwanda) pia walihojiwa. Kiunjuri, moja wa waziri wengine wanaokalika kuti kavu, wakati wa sakata hilo alikuwa Waziri wa Ugatuzi maarufu serikali za majimbo na alikwapo wakati mikataba ikitolewa kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa hayo kwa Kampuni ya CMC Di Ravenna, yenye makazi yake nchini Italia.

Ofisi ya DCI iliwahoji makatibu wakuu wote wa zamani na wa sasa kuanzia siku ambayo wazo la kujenga mabwawa hayo ilibuniwa. Sakata hilo ambalo Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Noordin Haji, amelieleza kama kesi ya ufisadi mkubwa nchini Kenya katika siku za hivi karibuni, ilisababisha Kenya kuomba msaada kutoka Italia, Uingereza na Dubai hatimaye kupata ushahidi unaohitajika kuanza mashtaka.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka unaoongozwa na Taib Ali Taib, akisaidiana na Alexander Muteti, Victor Owiti na Emily Kamau huku kikosi cha upande wa utetezi kinawajumuisha Katwa Kigen, Kioko Kilukumi, Philip Nyachoti, Kipchumba Murkomen, Kevin Anami, Mwai Mugo, Stephen Kimathi, Mahat Samane na Jinaro Kibet.

DPP Haji aliagiza kukamatwa kwa maofisa hao wakuu serikalini baada ya kufanya uchunguzi uliodumu kwa miezi tisa kuhusu ujenzi wa mabwawa hayo uliokadiriwa kugharimu Shilingi za Kenya bilioni 65.

Rotich ni nani?

Rais Uhuru Kenyatta alipokuwa Waziri wa Fedha katika serikali ya mseto kufuatia machafuko ya Uchaguzi Mkuu 2007, alimvuta Rotich karibu kufanya naye kazi kutokana na uelewa wake wa masuala ya uchumi.

Kabla ya kuletwa karibu na Uhuru, Rotich alihudumu akiwa mwanauchumi katika Shirika la Fedha Duniani (IMF) ofisi zake za Nairobi mwaka 2004 baada ya kufanya kazi kwa muda mchache na Benki Kuu ya Kenya. Katika azma ya kukonga nyoyo za Wakenya wakati anasoma bajeti yake ya kwanza akiwa Waziri wa Fedha, Rotich alimwaga fedha kwa miradi kama vile Galana Kulalu irrigation scheme na Standard Gauge Railway ambayo ingebadilisha sura ya Kenya.

Lakini kitendo chake cha kukopa mamilioni ya fedha huku kukiwa hakuna maelezo yanayokidhi kuhusu matumizi ya fedha yenyewe, kuliacha maswali mengi na kutumbukiza taifa katika wimbi la madeni makubwa.

Haishangazi wakati DPP akitangaza kukamatwa kwa Rotich na wenzake sababu kubwa iliyokuwa inajitokeza ni kivipi mabilioni ya fedha kutoka kodi ya wananchi na nyingine za kukopa yanakosa maelezo ya kina ya namna zilivyotumika.

“Ungetarajia hakuna tatizo kwa miradi ambayo ipo kisheria na imefuata taratibu zote lakini kiasi kikubwa cha fedha kilichotumika na malipo kinyume ya sheria yote yakifanyika machoni mwa maofisa wa Serikali wakishirikiana na taasisi binafsi ziliibua maswali mengi,” alisema Haji.

Rotich ambaye ni mzaliwa wa Elgeyo Marakwet, sehemu ambayo mradi huo wa mabwawa ungejengwa, sasa anajikuta katikati ya siasa na kesi ya ufisadi inayomkabili. Wakazi wa eneo hilo ambao waliondolewa na kuahidiwa kulipwa hadi sasa wanalalamika kwamba ahadi haijatekelezwa.

Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa hususan anapotoka Naibu Rais, William Ruto, wametafsiri kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa Rotich kumefanyika kisiasa lengo likiwa ni kumdhoofisha Ruto anayetajwa kuwania urais 2022.

Seneta wa Elgeyo Marakwet, ambaye pia ni kiongozi wa walio wengi Bunge la Seneti, Kipchumba Murkomen, amepinga kukamatwa kwa Rotich akisema haileti picha halisi ya mapambano dhidi ya ufisadi mbali kuwadanganya Wakenya kuonyesha vita dhidi ya ufisadi imeshika kasi.

“Nikiangalia ushahidi uliopo na mambo yanayoendelea nyuma ya pazia, nikiangalia watu waliokamatwa, waliyoachwa, namna walivyokamatwa na sababu zinazotolewa ikiwamo miradi inayohujumiwa, nimefikia hitimisho kwamba tunachokifanya ni kuwadanganya Wakenya,” alisema.

Rotich na wenzake kwasasa wapo nje kwa dhamana, japo DPP alipinga mahakama kuwapa washukiwa dhamana. Kutokana na mahakama kuwazuia kurudi kazini, Rais Uhuru amemteua Waziri wa Kazi, Ukuru Yatani, kukaimu nafasi ya Waziri wa Fedha huku akifanya mabadiliko katika nafasi za makatibu wakuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles