NA MWAMVITA MTANDA
YANGA
imezindua kwa kishindo tamasha lake lililopewa jina la Wiki ya Wananchi, ambapo
wapenzi, wanachama na mashabiki wa klabu hiyo nchi nzima watafanya shughuli za
kijamii.
Tamasha hilo
lililozinduliwa jana Dar es Salaam, litafikia tamati Agosti 4, Uwanja wa Taifa
jijini humo, ambapo kikosi cha timu hiyo kitakachoshiriki Ligi Kuu Tanzania
Bara msimu ujao na mashindano mengine, ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika
kitatambulishwa.
Mbali ya kutambulisha wachezaji, timu hiyo itashuka dimbani kuumana na Kariobangi Sharks ya Ligi Kuu ya Kenya, katika mchezo wa kirafiki utakaopigwa kwenye uwanja huo.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Wiki ya Wananchi, Rogers Gumbo alisema, lengo la kunzisha tukio hilo kuwakutananisha wanachama wa Yanga na kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kufanya usafi na kutembelea wagojwa katika hospitali.
“Hii wiki ni muhimu sana kwetu tena ya kihistoria tangu kuanzishwa kwa klabu hii, hivyo naweza kusema itasaidia kuwajenga Wanayanga na kutambua majukumu yao katika jamii,”alisema Gumbo.
Rogers alisema baadhi ya wanachama wa klabu hiyo leo watasafiri kwenda Zanzibar ambako watakutana na wadau na mashabiki wa huko na kufanya mkutano mkubwa wa wanachama.
Alisema wakiwa huko, watawatembelea wagonjwa na kufanya usafi katika maeneo mbalimbali.
Alisema Wiki ya Wananchi itaenda sambamba na burudani za ngoma za asili.