29.9 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Tahea yataka uwekezaji kwa wanawake, wasichana kujenga jamii yenye haki sawa kwa wote

Na Mwandishi wetu, Mwanza

ILI kupata mustakabali bora, kujenga jamii yenye usawa, haki na ustawi kwa wote, Serikali, taasisi binafsi, wadau na jamii wameshauriwa kuwekeza kwa wanawake na wasichana.

Wito huo ulitolewa wilayani Misungwi mkoani hapa na Meneja miradi wa Shirika linalojishughulisha na uchumi wa nyumbani (Tahea) mkoa wa Mwanza, Mussa Masongo ikiwa ni sehemu ya ujumbe wa shirika hilo katika kuadhimisha kilele cha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani inayooadhimishwa Machi 8, kila mwaka.

Meneja Miradi wa Tahea Mussa Masongo akitoa ujumbe wa Shirika hilo katika kuadhimisha kilele cha Siku ya kimataifa ya Wanawake Duniani iliyofanyika kimkoa wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza.

Ambapo mwaka huu maadhimisho hayo mkoa wa Mwanza yalifanyika Machi 8, katika Uwanja wa Amani wilayani Misungwi yakibebwa na kauli mbiu ya ‘Wekeza kwa wanawake kuharakisha maendeleo ya taifa na ustawi wa jamii’.

Masongo amesema shirika hilo ambalo linafadhiliwa na shirika la kimataifa la WE EFFECT ni mdau wa maendeleo ya wanawake na kwamba maadhimisho hayo yanapaswa kutumika kutafakari changamoto zinazoendelea kuwakabili wanawake katika nyanja za uchumi, siasa, elimu, kilimo, biashara na uongozi.

Ameongeza kwamba kama wadau hao wote watawekeza kwa wanawake na wasichana kupitia elimu bora, afya, kuwawezesha kiuchumi na kuwapa fursa za ujasiriamali na ajira basi taifa litakuwa limewekeza katika mustakabali bora wa jamii na kujenga kwa pamoja jamii yenye usawa, haki na ustawi kwa wote.

“Katika siku hii muhimu Tahea tunatoa wito kwa serikali, mashirika ya kijamii, sekta binafsi na jamii kwa ujumla kuwekeza katika wanawake kwa kutoa elimu bora kwa wasichana na wanawake na kuhakikisha afya bora kwa wanawake na watoto,” amesema Masongo na kuongeza;

“Pia kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuwapa fursa za ujasiriamali na ajira, kupambana na unyanyasaji kwa wanawake na watoto na kuhamasisha usawa wa kijinsia katika ngazi zote za maamuzi kwa sababu tunaamini katika uwezo wa wanawake kuleta mabadiliko chanya katika jamii na tunajitahidi kuwawezesha kupitia miradi yetu mbalimbali,”amesema Masongo.

Akizungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake mkoani Mwanza, Mwenyekiti wa Kamati ya maadhimisho hayo, Zeyana Seif amesema wanawake ndiyo kundi kubwa linalokabiliwa na changamoto nyingi na kushindwa kushiriki katika shughuli za maendeleo, ikiwemo upatikanaji wa maji, upungufu wa mabweni kwa wanafunzi wa kike, mila, desturi na mfumo dume unaowakandamiza.

“Changamoto ya upatikanaji maji inamchukulia mwanamke muda mwingi na kushindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, upungufu wa mabweni unawafanya watoto wa kike kushindwa kutimiza ndoto zao, pia kusitishwa kwa mikopo yya halmashauri kumewaathiri wanawake tunaiomba Serikali irejeshe mikopo hii,” amesema Zeyana.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza CPA Amos Makalla( aliyevaa suti na miwani) akisalimiana na baadhi ya wanawake waliohudhuria maadhimisho ya kilele cha siku ya mwanamke mkoani humo yaliyofanyika Wilayani Misungwi.

Hat hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, CPA Amos Makalla amewatoa wasiwasi wanawake na wasichana mkoani hapa akisisitiza kwamba Serikali imeanza kuzitafutia mwarobaini changamoto zinazowakabili ikiwemo maji, afya na mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu ambayo inatafutiwa utaratibu mzuri ili ilete manufaa kwa wakopaji.

“Serikali imetoa fedha nyingi katika miradi ya afya na maji ambapo kwa sasa upatikanaji wa maji maeneo ya vijijini ni asilimia 70 na lengo ni kufikia asilimia zaidi ya 80 ifikapo mwaka 2025. Lakini tunaona miaka 63 baada ya uhuru hali ya usawa wa kijinsia ni ya kuridhisha katika nyanja zote na tumeshuhudia wanawake wanapewa kazi na wanachapa kazi,” amesema Makalla.

“Watu wengi hawajui ukatili wanadhani ni kuua ama kujeruhi tu, natoa wito kwa wadau wote kuhamasisha jinsia zote zinazofanyiwa ukatili zijitokeze kutoa taarifa, pia asasi za kiraia ziendelee kutoa elimu na machapisho ya aina za ukatili na namna ya kuzuia huku wananchi nao wapende kusoma na kufahamu kuhusu ukatili ili wajue namna ya kuukemea,” amesema CPA Makalla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles