Na Janeth Mushi
WADAU 400 wa Horticulture kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) na SADC wanatarajia kukutana katika mkutano Desemba tano 2020,jijini Dar Es Salaam,wenye lengo la kuhamasisha fursa za uwekezaji na masoko katika mazao ya horticulture.
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Mkurugenzi wa Asasi kilele inayojishughulisha na masuala ya horticulture yaani maua,mbogamboga,matunda,mimea itokanayo na mizizi na viungo,(TAHA),Dk.Jackline Mkindi.
Alisema kupitia mkutano huo wadau hao watajadiliana mazingira endelevu ya kibiashara baina ya nchi zilizomo ukanda wa nchi hizo,kubadilishana uzoefu katika masuala ya horticulture,mawazo ya kibiashara kati ya sekta binafsi na uma ili kuvutia uwekezaji na kutengeneza ushirikiano linganifu kati ya sekta hiyo nchini Tanzania na kanda hizo.
Dk.Jackline alitaja miongoni mwa wadau hao ni wazalishaji,wafanyabiashara,wasafirishaji,wasindikaji kutoka nchi za Rwanda,Kenya,Sudani,DRC Congo,Comoro,Malawi na wenyeji Tanzania.
Alisema mkutano huo wameuandaa kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine ambapo pamoja na masuala mengine watajadiliana juu ya fursa za uwekezaji,masoko na viwezeshi vingine vya kusaidia upatikanaji wa masoko kama sehemu ya kuendeleza na kukuza kilimo cha horticulture baina ya nchi hizo.