25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Kunywa pombe mwisho chupa tatu-Daktari

Na AVELINE KITOMARY

DAKTARI bingwa wa afya ya akili  na uraibu wa dawa za kulevya wa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, Dk. Sostesjofu Mongu ameeleza unywaji wa pombe unaofaa kiafya  ili kuepukana kuwa tegemezi  na magonjwa yasiyoambukiza.

Kwa mujibu  daktari huyo kiafya mwanamke anashauriwa  kunywa chupa saba za bia kwa wiki moja huku mwanaume akishauriwa kunywa chupa 14 za bia kwa wiki moja.

Katika mahojiano maalumu na MTANZANIA  yaliyolenga athari ya matumizi ya  pombe, Dar es Salaam jana, Dk Mongu alisema pombe ni kilevi chochote ambacho mtu akinywa kinabadilisha  mtazamo ,hisia  na mawazo ya mnywaji.

“Kiwango cha ulevi wa pombe inategemea na  ujazo wa pombe kuna za mill 100, zingine 250 hadi 500 kwahiyo kila pombe inaujazo wake na kiwango cha ‘alcohol’ inategemea na aina ya pombe.

“Tunasema kuna aina ya unywaji ambao unaboresha afya  huu ni unywaji usiokuwa na  madhara kwa lugha nyepesi tunaita unywaji wenye afya ambao unaboresha mzunguko wa damu.

“Kwa mwanamke kwa wiki moja anatakiwa asinywe zaidi ya chupa saba za bia na kwa mtoko mmoja anatakiwa kunywa chupa moja hadi tatu tu na kwa mwanaume kwa wiki asizidi chupa 14 na kwa mtoko mmoja anatakiwa kunywa chupa mmoja mpaka nne huo ndio unywaji salama kwa afya,”alibainisha.

Alisema unywaji wenye madhara ni ule ambao mtu akinywa siku ya pili anajikuta yuko polisi kwa kufanya uharibifu au hospitali kupata matibabu.

“Utakuta mtu anakunywa pombe hadi anajikuta anashindwa kufanya majukumu yako kwasababu alikunywa jana ametapika  anaamka anaumwa na unashindwa kwenda kazi ,unywaji wa aina hiyo tunasema huo ni unywaji  wenye madhara.

Alieleza aina nyingine ya tatu ya unywaji ni unywaji hatari ambapo husababisha madhara katika afya ya muhusika.

“Huu ni unywaji ambao kwa idadi  ya pombe unazokunywa inapelekea madhara kiafya unakunywa pombe lakini tayari umeshakuwa na tatizo la kiafya ,unakunywa pombe wakati tayari umeshapata magonjwa ya moyo,stroke,ugonjwa wa ini ,na kansa,”alifafanua.

Alisema  hatua ya nne,  ni utegemezi wa pombe kwamba mtu hawezi kufanya kitu chochote  hadi  apate pombe.

“Umeamka asubuhi huwezi kupata nguvu ya kupiga hata mswaki ,kwenda kazini lazima uhitaji pombe ,ukifikia kiwango cha utegemezi wa pombe maana yake hata kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii inakuwa shida  huwezi kwenda kwenye msiba,harusi,shughuli za uzalishaji kwasababu unakuwa umelewa muda wote.

“Mwisho wa siku kama huwezi  kuacha pombe unapata magonjwa yasiyoambukiza  na kwasababu  huwezi kuacha pombe na maradhi unayo unapunguza muda wa kuishi na mwisho wa siku ni kifo,”alisema.

Alisema ni muhimu jamii kuelewa unywaji gani  ambao hauna hatari na bila kupata maradhi .

“Unywaji wa pombe kupindukia unaathari katika familia  kwasababu kama ni mzazi anashindwa kuhudumia familia na kusahau majukumu yote hivyo familia itateseka hata akipata kazi anashindwa kufanya kwasababu ameshakuwa tegemezi.

Alibainisha kuwa asilimia 40 ya magonjwa yasiyoambukiza yanasababishwa na madhara ya matumizi mabaya ya pombe.

“ Ukienda MOI  utakuta kuna majeruhi ambao chanzo ni ulevi,Jamii sehemu kubwa inahitaji  elimu juu ya matumizi ya pombe serikali kupitia wizara ya afya ijaribu kuweka mtaala wa matumizi ya  vinywaji kama pombe, dawa za kulevya iwe inafundishwa shuleni na tupate wataalamu wa kutosha katika kuelimisha jamii ,”alishairi Dk Mungo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles