31 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 3, 2023

Contact us: [email protected]

Wananchi Kilimanjaro wahimizwa kuchangamkia matibabu bure

Na Mwandishi wetu, Kilimanjaro

WAKAZI wa Mkoa wa Kilimanjaro na mikoa ya jirani wametakiwa kuchangamkia fursa ya huduma mbalimbali za afya ambazo zimeanza kutolewa bure kuanzia leo Novemba 25 hadi Desemba mosi, katika viwanja vya Mandele kata ya Pasua, Manispaa ya Moshi.

Wito huo umetolewa leo Novemba 25, na Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Anna Mghwira wakati akizindua maadhimisho ya siku ya UKWIMU duniani ambapo kitaifa yatafanyika mkoani humo yakiwa na kauli mbiu ya ‘Mshikamano wa Kimataifa, Tuwajiike kwa Pamoja’.

Dk. Mghwira amesema lengo la lengo la maadhimisho hayo ni sehemu ya kuwakumbuka wapendwa wetu waliotangulia mbele za haki kwa sababu ya ugonjwa huo.

“Kuanzia leo Novemba 25, hadi Desemba mosi, huduma za afya mbalimbali zitakuwa zinatolewa bila malipo kwenye viwanja vya Mandela, niwahimize wakazi wakazi wote wa mkoa wa Kilimanjaro na Mikoa ya jirani kutochezea fursa hii kwani afya ni uhai.

“Mkoa wetu wa Kilimanjaro umepata fursa ya kuwa mwenyeji katika maadhimisho ya mwaka huu ambayo yanabebwa na kauli mbiu isemayo ‘Mshikamano wa Kimataifa, – Tuwajibike kwa Pamoja’ nitafurahi kuona uwanja huu unajaa kila siku kwa ajili ya kupata huduma na ushauri wa kiafya unaotolewa hapa,” amesema Dk. Mghwira.

Amezitaja huduma zinazopatikana uwanjani hapo bila malipo kuwa ni pamoja na upimaji wa hiari VVU, uchunguzi wa kifua kikuu, kisukari, shinikizo la damu, saratani ya shingo ya kizazi na uwiano wa uzito na urefu.

Amesisitiza kuwa hamasa ya upimaji wa hiari VVU inawalenga watanzania wote kutambua hali zao za maambukizi ya VVU, hususani vijana wenye umri wa miaka 15-24 na watu wa makundi maalum walio kwenye hatari zaidi ya kuambukiza au kuambukizwa VVU wakiwemo wanaojihusisha na biashara ya ngono na majidunga.

“Natoa msisitizo kwa wanaume kujitokeza kwa wingi katika kupima ili kujua hali za maambukizi kwa sababu takwimu za upimaji wa kawaida zinaonyesha idadi ndogo ya 45% ya wanaume hujitokeza kupima VVU, kwa sababu wanaume wengi hutafsiri majibu ya vipimo vya wenzi wao kwamba ndio majibu yao badala ya wao kwenda kupima.

“Nitoe rai kwa wananchi kujitokeza katika kupima ambapo watakaogundulika kuwa na VVU watapata ushauri nasaha na kuanza kutumia dawa za ARV mapema ambapo kutumia dawa za ARV huwezesha kufubaza na kuimarisha kinga dhidi ya magonjwa nyemelezi,wajawazito kupunguza hatari ya kuambukiza watoto pamoja na kupunguza hatari ya kuambukiza VVU kwa wenzi wa ngono.” Amesema Dk. Mghwira.

Aidha amezungumzia kiwango cha maambukizi ya VVU katika mkoa wa Kilimanjaro kuwa yameendelea kupungua kutoka aslimia 7.3 mwaka 2004 hadi asilimia 2.6 mwaka 2017, kiwango hiki kipo chini ya wastani wa maambukizi ya kitaifa ambacho ni asilimia 4.8

Uzinduzi huo ulitanguliwa na matembezi ya hisani kwa ajili ya kutangaza na kuhamasisha uchangiaji wa Mfuko wa udhamini wa kudhibiti UKIMWI-(AIDS TRUST FUND).

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Dk. Anna Mghwira akiongiza matembezi ya hisani kwa ajili ya kuhamasisha uchangiaji wa mfuko wa udhamini wa kudhibiti UKIMWI(ATF) kulia Kwake ni, Mwasaga Wiliam mjumbe wa Bodi ya Mfuko wa udhamini wa kudhibiti UKIMWI na kushoto kwake ni Dk. Leonard Maboko Mkurugenzi Mtendaji TACAIDS, Matemebezi hayo yamefanyika leo mkoani Kilimanjaro Novemba 25, 2020.

Akizungumzia umuhimu wa Mfuko wa udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (ATF) Dk, Mgwira amesema mfuko huo ni muhimu katika kukabiliana na upungufu wa rasilimali za udhibiti UKIMWI pamoja na kupunguza utegemezi kwa wahisani.

“Nawaomba wananchi wenzangu tuchangie mfuko huu kupitia namba ya airtel money 0684 90 90 90 uchangiaji huu uwe endelevu tushikamane tuwajibike kwa pamoja.

“Takwimu zinaonyesha kuwa vijana wenye umri wa miaka 15-24 ndio wanaochangia asilimia 40 ya maambukizi mapya, hivyo kupitia maadhimisho haya vijana wataweza kupata elimu sahihi na njia za kujikinga dhidi ya maambukizi mapya ya VVU kupitia kijiji cha vijana ambacho kitakuwepo kwenye uwanja wa maadhimisho.

“Pia kutakuwa na mdahalo wa wanavyuo wenye lengo la kubadilishana uzoefu wa namna ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU katika mazingira ya vyuoni na nje ya vyuo ambalo litawahusisha vijana,” amesema Dk. Mghwira.

Ameongeza kuwa kutakuwa na kongamano kubwa la kisayansi litakalohusu masuala ya UKIMWI litakalofanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia kessho Novemba 26-27 ambapo katika kongamano hilo wataalamu watajadili mafanikio, changamoto na namna ya kukabiliana na changamoto hizo katika kudhibiti maambukizi mapya ya VVU.

“Japokuwa kiwango cha maambukizi kwa mkoa wetu wa Kilimanjaro kipo chini ya wastani wa Kitaifa haimaanishi kuwa tuko salama hivyo kwa pamoja tunapaswa kuongeza juhudi ili tufikie lengo la maambukizi sifuri ifikapo mwaka 2030.

“Kwa mujibu wa utafiti huu kiwango cha kufubaa kwa VVU kwa mkoa wa Kilimanjaro ni asiimia 67 dhidi ya asilimia 52 ya kitaifa hivyo matokeo haya yameuweka mkoa wa Kilimanjaro kuwa wa pili kitaifa kwa kuwa na kiwango cha juu cha kufubaza kwa VVU ukitanguliwa na mkoa wa Lindi.

“Changamoto kubwa kwa mkoa wa Kilimanjaro katika kudhibiti maambukizi mapya ya VVU ni huduma ya tiba na matunzo ambapo baadhi ya WAVIU kutokuwa na ufuasi mzuri wa dawa za ARV pindi afya zao zinapoonekana kuimarika.

“Natoa rai kwa WAVIU wote waliokwisha anza kutumia dawa za ARV, wazingatie ufuasi mzuri wa dawa,nawaagiza wadau wote mhakikishe mnawashirikisha vyema WAVIU hasa waliojiweka wazi juu ya hali zao  katika kuhamasisha WAVIU wasiokuwa na ufuasi mzuri wa matumizi ya dawa za kufubaza (ARV),” amesema Dk. Mghwira.

Aidha, ametoa shukrani kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia TACAIDS kuupa mkoa wetu heshima ya kuwa mwenyeji wa wiki ya maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani kufanyikia kitaifa mkoani Kilimanjaro.

Ameahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau pamoja na wafadhili wa ndani na nje ya katika Mwitikio wa VVU na UKIMWI na kuhakikisha dawa zinaendelea kuwepo bila kukosekana.

Naye, Mwenyekiti wa Baraza la watu wanaoishi VVU (NACOPHA) ameishukuru serikali kwa kuendelea kutambua haki za watu wanaoishi na VVU ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwapa huduma stahiki, na uhakika wa dawa za kufubaza VVU(ARV) ni hatua kubwa katika kuhakikisha tunadhibiti maambukizi mapya na kufikia zero mwaka 2030.

Mkurungezi Mtendaji wa TACAIDS, Dk. Leonard Maboko ameushukuru Mkoa wa Kilimanjaro kwa ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha maandalizi ya maadhimisho haya yanafanikiwa.

Dk. Leonard Maboko Mkurugenzi Mtendaji Tume ya kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) akisalimia wananchi walioudhuria uzinduzi wa maadhimisho ya kilele cha siku ya UKIMWI, duniani

Amewaomba wadau kuendelea kuonesha ushirikiano katika kuhakikisha maadhimisho haya yanaleta chachu ya mabadiliko katika kudhibiti maambukizi mapya ya VVU pamoja na kutoa elimu ya VVU na UKIMWI kwa wananchi.

Kilele cha maadhimisho hayo Disemba mosi, ambapo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atakuwa mgeni rasmi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles