Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania(TACAIDS) imepongezwa kwa kufanya kazi nzuri na kutekeleza majukumu kwa kufuata utaratibu na kanuni zilizowekwa katika mipango yake ya utekelezaji wa shuhghuli za Tume.
Akifungua kikao cha 49 Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dk. Hedwiga Swai, amesema kuwa pamoja na mambo mengine lakini ameanza kwa kuwapongeza TACAIDS kwa kazi nzuri wanayoifanya katika utekelezaji wa majukumu ya tume.
“Nawapongeza kwa utekelezaji wa shughuli zenu kwa kufuata utaratibu na kanuni, hongereni sana, nimepata taarifa kuwa mmepata hati safi ya ukaguzi wa CAG kwani sio jambo dogo lakini naomba mwendelee kufanya hivyo msije sifiwa baada mkarudi nyuma.hongera sana Dk. Maboko na timu yako kwa ujumla,” amesema Dk. Hedwiga.
Dk. Hedwiga amesema amefurahishwa na jinsi ambavyo Tume imeendelea kufatilia madeni ya wafanyakazi na waliowengi wamelipwa madeni yao, jambo linaleta amani kwa watumishi kwani mtu akipata haki yake kunakuwa hakuna manung’uniko.
Naye mjumbe wa Kamisheni hiyo, Peter Maduki ameitaka tume kuhakikisha inaboresha uandishi wa taarifa kwa kuhakikisha kuwa taarifa ziwe na takwimu, Mafanikio na changamoto zinazojitokeza ili kamisheni ione namna ya kutoa mchango wake.
Kikao cha Kamisheni kinafanyika kwa mujibu wa sheria ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania Na. 22 ya mwaka 2001 na marekebisho yake Na.6 ya mwaka 2015 kikiwa na lengo la kufatilia utekelezaji wa majukumu ya TACAIDS katika Mwitikio wa Taifa.
Baada ya kikao hicho Mwenyekiti alipata nafasi ya kukutana na baadhi ya watumishi wa Tume pamoja na wafanyakazi hodari na kuwatunuku vyeti pamoja na zawadi, ambapo mfanyakazi hodari wa jumla kutoka TACAIDS ni Mhasibu Mkuu CPA(T) Karlson Konga.
Akiwakabidhi vyeti hivyo Dk. Hedwiga amewataka wafanyakazi wa TACAIDS kudumisha umoja na ushirikiano kwani ni kitu muhimu sana katika utekelezaji wa majukumu yao.