32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Tabia za watu hujidhihirisha kulingana na mazingira

Na Christian Bwaya



KASSIM yuko kwenye mazungumzo na rafiki zake. Kwa kawaida baada ya saa za kazi, hukutana na marafiki zake kwenye mgahawa mmoja mjini kwa ajili ya kupata kinywaji huku wakibadilishana mawazo. Wakati wakiendelea na mazungumzo, mara simu yake inaita. Kuitazama ni namba ya mtu asiyemfahamu.

Anaipuuza na kuendelea na mazungumzo yake. Kwa kawaida, Kassim huwa anathamini sana mazungumzo yake na watu huhakikisha anakuwa na uzingativu wote. Huweka simu mbali isipokuwa inapokuwa lazima.

Simu inaendelea kuita. Safari hii anahisi pengine ni muhimu kuipokea. Anawaomba radhi rafiki zake kisha anaipokea. Hata hivyo, aliyepiga simu mara anakata. Kassim anairudisha mfukoni na kuendelea na mazungumzo.

Simu inaendelea kuita, anaipokea, lakini inakata bila kufahamika ni nani anayepiga. Anasonya kuonesha kukerwa na huyo anayemsumbua. Kwa mara ya tatu anakasirika. Anaandika ujumbe wa matusi kwa huyo anayemsumbua na kuendelea na mazungumzo yake.

Mara ujumbe mfupi wa maandishi unaingia, anausoma na ghafla uso wake unabadilika. Anajiuliza atakuwa mgeni wa nani? Kumbe amemtukana mchungaji wake aliyekuwa anajaribisha simu yake mpya, siku yake inakuwa imeharibika. “Ningejua ni nani nisingemtukana,” anajisemea.

Hajafanya tofauti na wanavyofanya watu wengi. Mara nyingi sura za watu hubadilika badilika kulingana na mazingira. Unapokuwa mbele ya bosi unaonesha uungwana, wengi huwa makini na maneno wanayozungumza wakiogopa kuchafua heshima waliyojijengea kwa bosi. Lakini wanapokuwa na wafagiaji wa ofisi hujiachia. Tabia huwa tofauti na ile wanayoionesha kwa bosi. Unaweza kukasirika hovyo, kutukana, kuonesha dharau kwa sababu hakuna cha kupoteza.

Mabadiliko haya ya sura ni mbinu za kuendana na matakwa ya mazingira. Inafahamika kwamba ili kukidhi mahitaji yako na yale ya watu wanaokuzunguka ni muhimu kuvaa sura inayotarajiwa. Kwa mfano, unapozungumza na bosi, kwa kawaida, unavaa sura ya kazi ili uonekane ni mtu makini. Kwa kuwa unafahamu bosi asingependa utani, unakuwa makini mnapokuwa naye ili kukidhi kile anachokitarajia kwako.

Lakini wengi huwa wanaigiza umakini pindi wanapokuwa na mabosi, wanaweza kuwa watu wa masihara wanapokuwa na watu wengine wanaofanana nao. Wanaweza kutaniana, kufanyiana masihara kwa sababu ile hofu ya kuharibu kazi inatoweka.

Tena wakati mwingine wanapoonekana makini sana, wenzao wanawashangaa. Itakuwa bahati mbaya bosi akiwakuta kwenye mazingira haya ambayo kwa vyovyote vile yatamfanya aufahamu upande mwingine wa maisha yenu.

Kama nilivyo tangulia kusema, mabadiliko haya yana umuhimu wake katika maisha ya kila siku. Usipojua namna ya kuvaa sura inayoendana na mazingira uliyopo, unaweza kupata shida kuishi na watu.

Tena wakati mwingine unaweza kudanganya ili ujenge sura inayohitajika. Chukulia mfano umeudhiwa na rafiki yako wa karibu kwa sababu unafikiri amefanya kitu cha kijinga. Moyoni unajua amefanya kitu cha kijinga lakini kwa kuwa unathamini urafiki wenu, huwezi kumwambia moja kwa moja. Unaweza hata kumwambia amefanya kitu sahihi kwa sababu tu unaogopa kuharibu uhusiano wenu.

Lakini kwa upande mwingine hulka hii ya kubadilisha sura ili kukidhi mazingira inaweza kukuingiza kwenye matatizo. Kwanza, watu wanaweza kushindwa kukuelewa vizuri kwa sababu haueleweki wewe ni mtu wa aina gani hasa. Ukirejea kwenye kisa cha Kassim hapo juu, rafiki zake wanaweza kushangaa kugundua kuwa naye anaweza kuwa anaweza kutukana ingawa anapokuwa nao anaonekana kuwa na busara. Ndio maana, wakati mwingine, unaweza kujikuta umeingia mkenge unapozoeana na mtu na kugundua kuwa sura aliyokuonesha wakati urafiki unaanza haikuwa yake halisi. Badala ya upendo uliouona awali, kumbe mwenzeko ni mtu mkatili na mwenye chuki. Upendo ulikuwa ni namna tu ya kukupata.

Vile vile, wakati mwingine, kubadilika badilika kunaweza kuchukuliwa kama dalili za kutokujiamini. Kisaikolojia, watu wanaojiamini na kukubali vile walivyo, hawana haja ya kuwa kinyonga ili kuwaridhisha watu. Mara nyingi watu hawa hubaki vile walivyo bila kujali wako na nani. Uungwana wanaounesha wanapokuwa na bosi, ndio uungwana huo huo wanaouonesha wanapokuwa na wafanyakazi wenzao.

Ucheshi wanaouonesha wanapokuwa na marafiki, ndio huo huo wanaouonesha wanapokuwa na familia zao. Ndio kusema, kwa mtu anayejiamini, ni rahisi kutabirika.  Ingawa ni kweli kunaweza kuwepo mabadiliko Fulani madogo madogo yanayokidhi mazingira fulani, lakini mtu anayejiamini hubaki kuwa yule yule.

Ni kurudie wewe msomaji. Je, ulivyo kazini, ndivyo ulivyo nyumbani kwako? Unavyoongea na watu wenye nyadhifa na nafasi fulani katika jamii ndivyo unavyoongea na watu wasio na cheo wala umaarufu? Je, unavyofahamika kwenye macho ya umma ndivyo ulivyo unapokuwa mwenyewe?

Christian Bwaya ni mnasihi na mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi. Wasiliana naye kwa 0754870815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles