26.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Haya hapa mazingira hatarishi kwa usalama wa mtoto

Na Christian BwayaTUMEKUWA tukisikia matukio ya watoto kudhalilishwa na watu wao wa karibu. Hapa tunazungumzia matukio kama kuingiliwa kimwili, kushikwa isivyo stahili, kutomaswa na vitendo vingine vinavyoashiria ngono.

Matukio kama haya huwaathiri mno watoto kimwili, kisaikolojia na hata kiroho. Watoto wengi wanaoingiliwa kimwili, kwamfano, hujenga hofu, hushindwa kuwaamini tena watu ambao kimsingi wangepaswa kuwaamini, hujichukia na matokeo yake mtazamo wao kuhusu wao na maisha kwa ujumla hubadilika.

Tafiti zinaonesha kuwa mara nyingi matukio haya huhusisha watu wanaoishi na mtoto. Hawa ni watu ambao kwa namna moja au nyingine walitarajiwa kuwa walinzi wa mtoto ndio hao hao wanaogeuka kuwa watu hatari kwa ustawi wa mtoto. Ikiwa unataka kuwalinda watoto na vitendo hivi, unayo kila sababu ya kutambua viashiria vya hatari kwa mtoto ili uweze kuchukua hatua stahiki kabla mambo hayajawa mabaya. Makala haya yanaangazia baadhi ya viashiria vya hatari kupima kiwango cha usalama katika ngazi ya familia.

Mtoto anamwamini nani?

Kama nilivyotangulia kusema, mara nyingi mtu anayeaminiwa na mtoto ndio huyo huyo anayeweza kugeuka kuwa tatizo kwa siri. Ikiwa unataka kumlinda mwanao na udhalilishaji usichukulie kirahisi rahisi imani kubwa anayokuwa nayo mwanao kwa mtu anayeishi hapo nyumbani.

Wabaini watu ambao mwanao hujisikia huru kuwa nao. Anaweza kuwa baba, mjomba, msaidizi wa kazi au ndugu mwingine yeyote. Mfundishe mwanao kujenga mipaka nao. Hakikisha anaelewa kuwa pamoja na kuwapenda, bado kuna vitu hapaswi kuvifanya akiwanao. Mfano, kuvua nguo mbele yao, kuwakalia, kukaa nao mahali pa faragha. Mtoto akijenga tabia hii mapema itamsaidia kuelewa pale mtu huyo anapoanza kuvuka mipaka hiyo.

Mtoto anaelewa kuhusu udhalilishaji?

Matukio mengi ya udhalilishaji huanza hatua kwa hatua. Wakati mwingine mdhalilishaji humwaminisha mtoto kuwa yuko salama lakini kumbe safari ya udhalilishaji ndio kwanza inakuwa imeanza.
Kukabiliana na tatizo ni muhimu kutathmini uelewa wa mtoto kuhusu udhalilishaji. Watoto wengi wanaodhalilishwa, wakati mwingine, huwa hawana uelewa wa kutosha unaosaidia kutambua hali isiyo ya kawaida.

Elimisha wanao wafahamu, kwa mfano, kuwa kushikwa shikwa na mtu mwingine ni udhalilishaji. Mtu mwingine yeyote hata awe rafiki wa baba na mama hawezi kumshika kwenye maeneo Fulani ya mwili. Kuna maneno ambayo hakuna mtu anaweza kumwambia bila kujali hadhi yake na nafasi yake kwenye jamii. Mtoto anayeelewa hivyo anaweza kuwa mwepesi kutoa taarifa pale hali hiyo inapojitokeza.

Mtoto huenda wapi asipokuwa nyumbani?

Wakati mwingine mtoto hupata matatizo kwa sababu ameenda mahali hatarishi na mtu anayemwamini. Usipojua ameenda wapi hiyo inaweza kuwa sehemu ya tatizo. Jiulize, mtoto asipokuwa nyumbani anakuwa wapi? Je, anacheza wapi na nani? Marafiki zake wanapendelea nini? Je, anapotoka nyumbani, huambatana na mtu mzima yupi? Haya ni mambo ya msingi kuyafahamu ikiwa unalenga kumlinda mwanao na hatari ya udhalilishaji.

Mtoto hulala na nani?

Wakati mwingine mazingira anamolala mtoto yanaweza kuwa kichocheo cha udhalilishaji. Jiulize, nani analala na mwanao? Je, umeruhusu watoto wa kike na wa kiume kulala pamoja? Je, msaidizi wa nyumbani anayelala na mtoto ni mtu salama? Je, unaruhusu baba kulala na mwanao wa kike?

Christian Bwaya ni mnasihi na mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi. Wasiliana naye kwa 0754870815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles