Na Beatrice Lyimo – MAELEZO, CHINA
BALOZI wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki amezitaka taasisi zenye dhamana ya kutafuta masoko ya bidhaa mbalimbali nchini ikiwemo Tantrade, Bodi ya Kahawa, Chai, Korosho, Nafaka na mazao mchanganyiko kushiriki maonesho mbalimbali yatakayofanyika nchini China ili kutafuta masoko mapya ya bidhaa zao.
Kairuki alisema hayo jana alipokutana na ujumbe wa Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi walipotembelea nchini hapa kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu baina ya China na Tanzania katika tasnia ya habari na mawasiliano.
“Uzoefu wa hivi karibuni umekuwa wa kukatisha tamaa kutokana na ubalozi kutafuta fursa mbalimbali kwa ajili ya bidhaa za Tanzania kutangazwa, lakini wadau wameshindwa kushiriki,” alisema Kairuki.
Alisema kumekuwapo na ongezeko la matumizi ya kahawa miongoni mwa watu wa Jamhuri ya China na kahawa ya Tanzania ni miongoni mwa zinazopendwa hivyo hiyo ni nafasi ya kupata soko la uhakika endapo itafanyika kampeni mahususi ya kuitangaza.
Pia alisema madini mbalimbali na vito kutoka Tanzania yana nafasi ya kupata soko nchini hapa endapo patakuwapo na mifumo mizuri ya kisasa ya kuendesha minada ya madini.
Mbali na hayo, Balozi Kairuki ametaja baadhi ya matarajio ya ubalozi wa Tanzania nchini hapa katika kipindi cha miaka minne ijayo ikiwepo kuongeza idadi ya sasa ya watalii kutoka 30,000 hadi 100,000 ifikapo mwaka 2020.
Alisema kuwa ubalozi unatarajia kuongeza uwekezaji kutoka China hususani kwenye ujenzi wa viwanda ikiwa na lengo la kati ya sasa hadi 2021 kuvutia viwanda 100 ili kufanya ongezeko la uwekezaji kutoka Dola za Marekani bilioni 3.6 za sasa hadi kufika bilioni 7 ifikapo 2021.
“Pia ubalozi unatarajia kuongeza idadi ya fursa za mafunzo kwa Watanzania katika fani mbalimbali hususani uhandisi ikiwa na lengo kuu la kuhakikisha Watanzania 1,000 wapate mafunzo ya uhandisi ifikapo mwaka 2021,” alisema.