TUMEPOKEA taaarifa ya kuzinduliwa kwa Bodi ya Taasisi ya Jakaya Kikwete kwa mtazamo chanya. Taasisi hiyo tunadhani itaweza kuleta mabadiliko yenye tija kwa nchi yetu. Kama ilivyoonekana katika vyombo vya habari, uzinduzi wa bodi hiyo ambayo ina watu makini wanaoweza kweli kuiongoza taasisi hiyo kuelekea katika mafanikio makubwa.
Tunao uzoefu wa viongozi au watu maarufu kuanzisha taasisi au taasisi kuanzishwa kwa majina yao. Taasisi hizo nyingine huwa ni mifuko ya fedha ambazo hutumika kuendeleza njozi za mhusika. Zipo taasisi za aina hizo nyingi sana ulimwenguni.
Hapa nchini mwetu tunafahamu Taasisi ya Mwalimu Nyerere ambayo imejikita katika kudumisha aliyoyaamini Mwalimu Julius Nyerere Baba wa Taifa katika kukuza amani, umoja na maendeleo yanayowagusa watu barani Afrika kwa kuzingatia haki kwa kila mtu. Pia ipo Taasisi ya Benjamin William Mkapa ambayo yenyewe iko katika masuala ya afya wakishughulika na Virusi vya Ukimwi na Ukimwi lakini kwa mtazamo wa huduma za afya kwa ujumla wake pamoja na afya ya uzazi na afya ya watoto Tanzania..
'JK avalia njuga utawala bora, elimu, afya na vijana' ni moja ya vichwa vya habari katika moja ya magazeti yaliyotoa taarifa ya Taasisi ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete. Masuala yote yaliyotajwa hapo kama vipaumbele vya taasisi hii ni vya muhimu sana kwetu . Vijana wapo wengi nchini na takwimu zinaonyesha ni wengi kuliko watu wa makamo na wazee. Na wana changamoto nyingi sana ikiwamo elimu na kazi. Kwa hiyo kuvalia njuga suala la vijana ni mahali pake.
Suala la elimu nalo ni muhimu kwani elimu ndio msingi wa karibu kila kinachofanyika na huweza kufanya mabadiliko ya mtu binafsi hadi kubadilisha jamii kwa ujumla. Afya nayo ni muhimu kwani ikitetereka kwa mtu huathiri mambo mengi ya mtu katika ubinafsi wake lakini pia jamii inayomzunguka. Pia zipo changamoto nyingi tu katika eneo hilo. Utawala bora ndio uliotajwa kwanza katika kichwa hicho cha habari. Na ndipo hoja ya leo ilipojikita.
Utawala bora ni dhana inayotokana na aina ya utawala. Kwa lugha ya Kiingereza dhana hii hutofautishwa na maneno mawili yanayoweza kuwa yanaonekana yanawiana yaani "Government na Gavernance". Neno la awali linahusu mfumo wa utawala yaani Serikali wakati la pili ni nafasi au wajibu wa Serikali katika kukabili masuala ya umma na nafasi za wahusika wengine ambao nao pia wana wajibu mkubwa katika kushughulikia changamoto zilizoko katika jamii zetu.
Kutokana na dhana hii ndipo suala la utawala bora huinuka. Dhana hii ina misingi yake ambayo ni ya muhimu sana katika ujenzi wa jamii zenye uwezekano wa kupata maendeleo endelevu. Kwa taasisi iliyoamua kuvalia njuga suala la utawala bora nina hakika ni kwa vile katika uchambuzi wao wameona jinsi suala hilo lilivyo na nafasi katika kujenga yale yote yanayotarajiwa kuwa vipaumbele kwa taasisi hiyo.
Misingi ya utawala bora ni mingi kutegemeana na muktadha wa anayeshughulika na dhana hii. Nitajaribu kuiangalia michache nikioanisha na hali halisi katika jamii yetu na kuona jinsi taasisi ya JK ilivyo na umuhimu wake kwa jamii ya Watanzania na kuwa imekuja kwa wakati wake. Moja ya misingi hiyo ni utawala wa sheria. Msingi huu unaangalia zaidi mifumo ya kisheria ambayo inapaswa kuwa yenye haki na inayotekelezwa bila upendeleo pamoja na kuwa na heshima ya haki za binadamu. Utawala wa sheria hutokana na Katiba ambayo ndio sheria mama. Wakati taasisi hii inavyoanza kazi zake suala la mchakato wa Katiba liko pembeni si kwa maana kuwa hatuna Katiba bali Katiba iliyopo inahitaji kubadilishwa. Bahati nzuri sana Rais Mstaafu JK aliasisi mchakato wa Katiba bali bahati mbaya haukutimilika kabla hajaondoka madarakani.
Katika mambo yaliyokuwa yamejitokeza katika mchakato huo ni uhuishwaji wa haki za binadamu katika Katiba na pia uwepo wa tunu ambazo zilitoa mwelekeo wa jinsi utawala wa nchi utakavyoimarishwa ili kweli uwe bora. Kwa kuzorota au kusimama kwa mchakato huo yapo masuala mengi katika eneo la utawala wa sheria nayo yamesimama na watawala wanapata upenyo kwa kutokutekeleza na wakihojiwa majibu ni kuwa hayo yatatekelezwa Katiba Mpya itakapokamilika.
Ingefaa taasisi hii ikapata fursa ya kushawishi uendelevu wa mchakato wa Katiba ili suala hili la utawala wa sheria lianzie na sheria hii kuu yaani Katiba.
Tukingalia msingi mwingine ni sauti za wananchi na kukubalika kwa mamlaka inayoongoza. Haya yanasimamiwa na nafasi waliyonayo wananchi ya ushiriki katika masuala yanayowahusu. Hivyo basi kwa msingi huu wa utawaa bora wanawake kwa wanaume wanapaswa kuwa na sauti katika kuamua mambo yanayowagusa na sauti hii inapaswa iwe moja kwa moja au kupitia wawakilishi. Ushiriki huu unajengwa kwenye uhuru wa kujumuika na uhuru wa kujieleza na uwezo wa watu wenyewe kushiriki kwa tija.
Eneo hili nalo lina uhitaji mkubwa kuangaliwa na taasisi hii kwani tumeanza kuona shida katika suala zima la ushiriki na hata sauti watu wanazopaswa kuwa nazo. Iwapo tunashiriki kwa njia ya kuwakilishwa wawakilishi wetu wanapaswa kutusikiliza sisi na kuwajibika zaidi kwetu tunaowakilishwa. Shida kubwa hapa kwetu ni jinsi vyama vya siasa vinavyokuwa na kauli kubwa kuliko wale wanaowakilishwa ambao wengi hawamo kwenye hivyo vyama. Pale wawakilishi hususani wabunge wanapobanwa kwa misingi ya chama na si kwa kusimama kutetea yale ya wanaowakilishwa hapo msingi huu unakuwa mashakani na ndio maana ipo haja kwa taasisi kama hii kuangalia changamoto gani zinazogusa hali hii na kurekebisha au kuchangia katika kurekebisha kwa wao wanaojaribu kufanya hivyo hata sasa.
Msingi mwingine wa muhimu pia ni ule wa uwajibikaji na uwazi. Utawala bora unahitaji wafanya uamuzi serikalini, kwenye sekta binafsi na asasi za kiraia wawajibike kwa umma na kwa wadau katika eneo lao. Kuna wakati si Serikali, sekta binafsi au asasi za kiraia huonekana wakiwajibika kwa umma. Mara nyingi tunaona uwajibikaji huwa zaidi kwa waliowapatia fedha na si kwa wananchi ambao fedha zozote zinazopatikana ni kwa ajili yao au manufaa yao. Kwenye suala la uwazi hili linahusu habari zinavyotiririka kuwafikia watu. Habari hizi ni zile muhimu kwa watu wanaotegemea kutoka kwa Serikali walioiweka madarakani na kwa wawakilishi waliowapa dhamana. Inapotokea kuwa kupata taarifa zinazoigusa jamii inakuwa ngumu hapa utawala bora unakuwa mashakani.
Kumekuwa na kilio kikubwa cha suala la Bunge kuoneshwa moja kwa moja. Wananchi hapa walikuwa wakipata habari zinazoendelea kwa wawakilishi wao na hivyo kufuatilia na kutoa maoni na hata mawazo na kukosoa ikibidi. Mfumo huu umebadilishwa bila hata kuwashirikisha wananchi ambao ndio wadau wakuu. Hata pale wawakilishi walipotoa maoni na kudai hali ibadilike watawala hawakuona sababu ya kuwasikiliza wananchi au wawakilishi wao. Masuala kama haya ndio yanapaswa kujengewa hoja na taasisi mbali mbali ikiwamo taasisi hii ya JK ambayo imeamua kujikita katika masuala ya utawala bora.
Utawala bora ukisimama katika misingi yake yote mengine yatawezekana kirahisi sana na hivyo basi tuwatakie kila la heri Bodi ya Taasisi hii ya Jakaya Kikwete katika jukumu hili zito na adhimu. Utawala bora ni nguzo katika kuleta maendeleo.