25.4 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

TAASISI YA  RAIS MSTAAFU  JK NA  UTAWALA BORA

TUMEPOKEA  taaarifa ya kuzinduliwa  kwa Bodi ya Taasisi ya Jakaya Kikwete kwa mtazamo chanya. Taasisi hiyo tunadhani itaweza kuleta mabadiliko yenye  tija  kwa nchi yetu. Kama ilivyoonekana katika  vyombo vya habari, uzinduzi wa bodi hiyo ambayo ina watu makini wanaoweza kweli kuiongoza taasisi hiyo  kuelekea katika mafanikio makubwa.

Tunao uzoefu wa viongozi au watu maarufu kuanzisha taasisi au taasisi kuanzishwa kwa majina yao. Taasisi hizo nyingine huwa ni mifuko ya fedha ambazo hutumika kuendeleza njozi  za mhusika.  Zipo taasisi  za aina hizo nyingi sana ulimwenguni.

Hapa nchini mwetu tunafahamu Taasisi ya Mwalimu Nyerere  ambayo imejikita katika kudumisha aliyoyaamini Mwalimu Julius Nyerere Baba wa Taifa katika kukuza amani, umoja na maendeleo yanayowagusa watu barani Afrika kwa kuzingatia haki kwa kila mtu. Pia ipo Taasisi ya Benjamin William Mkapa  ambayo yenyewe iko katika  masuala ya afya wakishughulika na  Virusi vya Ukimwi na Ukimwi  lakini kwa mtazamo wa huduma  za afya kwa ujumla wake pamoja na afya ya uzazi na afya ya watoto Tanzania..

'JK avalia njuga utawala bora, elimu, afya na vijana' ni moja  ya vichwa vya habari katika moja ya magazeti yaliyotoa taarifa ya Taasisi ya  Rais Mstaafu Jakaya Kikwete. Masuala yote yaliyotajwa hapo kama vipaumbele vya taasisi hii ni vya muhimu sana kwetu . Vijana wapo wengi nchini na takwimu zinaonyesha ni wengi kuliko watu wa makamo na wazee. Na wana changamoto nyingi sana ikiwamo elimu na kazi. Kwa hiyo kuvalia njuga suala la vijana ni mahali pake.

Suala la elimu nalo ni muhimu kwani elimu ndio msingi wa karibu kila kinachofanyika na huweza kufanya  mabadiliko ya mtu binafsi hadi kubadilisha  jamii kwa ujumla. Afya nayo ni muhimu kwani  ikitetereka kwa mtu huathiri mambo mengi ya mtu katika ubinafsi wake lakini pia jamii inayomzunguka. Pia zipo changamoto nyingi tu katika eneo hilo. Utawala bora ndio uliotajwa kwanza  katika  kichwa  hicho cha habari. Na ndipo hoja ya leo ilipojikita.

Utawala bora ni dhana  inayotokana na aina ya utawala. Kwa lugha ya Kiingereza dhana hii hutofautishwa na maneno mawili yanayoweza kuwa yanaonekana yanawiana yaani  "Government na Gavernance". Neno la awali linahusu mfumo wa utawala yaani Serikali wakati  la pili ni nafasi au wajibu wa Serikali katika kukabili masuala ya umma na nafasi za wahusika wengine  ambao nao pia wana wajibu mkubwa katika kushughulikia  changamoto zilizoko katika jamii zetu.

Kutokana na dhana hii ndipo suala la utawala bora huinuka. Dhana hii ina misingi yake ambayo ni ya muhimu sana katika ujenzi wa jamii zenye uwezekano wa kupata maendeleo endelevu. Kwa taasisi iliyoamua kuvalia njuga  suala la utawala bora nina hakika ni kwa vile katika  uchambuzi wao wameona jinsi suala hilo lilivyo na nafasi katika kujenga yale yote yanayotarajiwa kuwa vipaumbele kwa taasisi hiyo.

Misingi ya utawala bora ni mingi kutegemeana na  muktadha wa anayeshughulika na dhana hii. Nitajaribu kuiangalia michache nikioanisha na hali halisi katika jamii yetu na kuona jinsi taasisi ya  JK ilivyo na umuhimu wake kwa jamii ya Watanzania na kuwa imekuja kwa wakati wake. Moja ya misingi hiyo ni utawala wa sheria. Msingi huu unaangalia zaidi  mifumo ya kisheria  ambayo inapaswa kuwa yenye haki na inayotekelezwa bila upendeleo  pamoja na kuwa na  heshima ya haki za binadamu.  Utawala wa sheria hutokana na Katiba  ambayo ndio  sheria mama. Wakati taasisi hii inavyoanza kazi zake suala la mchakato wa Katiba liko pembeni si kwa maana kuwa hatuna Katiba bali Katiba iliyopo inahitaji kubadilishwa. Bahati nzuri sana Rais Mstaafu JK aliasisi mchakato wa Katiba bali bahati mbaya haukutimilika kabla hajaondoka madarakani.

Katika mambo yaliyokuwa yamejitokeza katika mchakato huo ni uhuishwaji wa haki za binadamu katika  Katiba na pia uwepo wa tunu ambazo zilitoa mwelekeo wa jinsi utawala wa nchi utakavyoimarishwa ili kweli uwe bora. Kwa kuzorota au kusimama kwa mchakato huo yapo masuala mengi katika  eneo la utawala wa sheria nayo yamesimama na watawala wanapata upenyo kwa kutokutekeleza na wakihojiwa majibu ni kuwa hayo yatatekelezwa Katiba Mpya itakapokamilika.

Ingefaa  taasisi  hii ikapata fursa ya kushawishi  uendelevu wa mchakato wa Katiba ili suala hili la utawala wa sheria lianzie na sheria hii kuu yaani Katiba.

Tukingalia  msingi mwingine ni sauti za wananchi na kukubalika kwa mamlaka  inayoongoza. Haya  yanasimamiwa na nafasi waliyonayo wananchi ya  ushiriki katika masuala yanayowahusu. Hivyo basi kwa msingi huu wa utawaa bora  wanawake kwa wanaume  wanapaswa kuwa na sauti katika kuamua mambo yanayowagusa na sauti hii inapaswa iwe moja kwa moja au kupitia wawakilishi. Ushiriki huu unajengwa kwenye uhuru wa kujumuika na uhuru wa kujieleza na uwezo wa watu wenyewe  kushiriki kwa tija.

Eneo hili nalo lina uhitaji mkubwa kuangaliwa na taasisi hii kwani  tumeanza kuona shida katika suala zima la ushiriki na hata sauti watu wanazopaswa kuwa nazo. Iwapo tunashiriki kwa njia ya kuwakilishwa wawakilishi wetu wanapaswa kutusikiliza sisi na kuwajibika zaidi kwetu tunaowakilishwa. Shida kubwa hapa kwetu ni jinsi vyama vya siasa vinavyokuwa na kauli kubwa kuliko wale wanaowakilishwa ambao wengi hawamo kwenye  hivyo  vyama. Pale wawakilishi hususani wabunge wanapobanwa kwa misingi ya chama na si kwa kusimama kutetea yale ya wanaowakilishwa  hapo msingi huu unakuwa mashakani na ndio maana ipo haja kwa taasisi kama hii kuangalia changamoto gani zinazogusa hali hii na kurekebisha au kuchangia katika kurekebisha kwa wao wanaojaribu kufanya hivyo hata sasa.

Msingi mwingine wa muhimu pia ni ule wa uwajibikaji na uwazi. Utawala bora unahitaji wafanya  uamuzi serikalini, kwenye sekta binafsi na asasi za kiraia  wawajibike kwa umma na kwa wadau katika eneo lao. Kuna wakati si Serikali, sekta binafsi au asasi za kiraia huonekana wakiwajibika kwa umma. Mara nyingi tunaona uwajibikaji huwa zaidi kwa waliowapatia fedha na si kwa wananchi ambao fedha zozote zinazopatikana ni kwa ajili yao au manufaa yao. Kwenye suala la  uwazi  hili linahusu habari zinavyotiririka kuwafikia watu. Habari hizi ni zile muhimu kwa watu wanaotegemea kutoka kwa Serikali walioiweka madarakani na kwa wawakilishi waliowapa dhamana. Inapotokea kuwa kupata taarifa zinazoigusa jamii inakuwa ngumu hapa utawala bora unakuwa mashakani.

Kumekuwa na kilio kikubwa cha suala la Bunge kuoneshwa moja kwa moja. Wananchi hapa walikuwa wakipata habari zinazoendelea kwa wawakilishi wao na hivyo kufuatilia  na kutoa maoni na hata mawazo  na kukosoa  ikibidi. Mfumo huu umebadilishwa bila hata kuwashirikisha wananchi ambao ndio wadau wakuu. Hata pale wawakilishi walipotoa maoni na kudai hali ibadilike watawala hawakuona  sababu  ya kuwasikiliza wananchi au wawakilishi wao. Masuala kama haya ndio yanapaswa kujengewa hoja na taasisi mbali mbali ikiwamo taasisi hii ya JK ambayo imeamua kujikita katika masuala ya utawala bora.

Utawala bora ukisimama katika  misingi yake yote mengine yatawezekana kirahisi sana na hivyo basi tuwatakie kila  la heri Bodi ya Taasisi hii ya Jakaya Kikwete katika jukumu hili zito na adhimu. Utawala bora  ni nguzo katika kuleta maendeleo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles