24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI INAPOTEZA FEDHA, MUDA LOLIONDO

Na MASYAGA MATINYI 


KWA wiki kadhaa sasa kamati iliyo chini ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, imekuwa katika ziara yenye lengo la kutafuta suluhu kwenye maeneo kadha wa kadha ndani ya Pori Tengefu Loliondo. 

Maeneo hayo ni yale yenye mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miongo miwili ukihusisha Serikali, wenyeji wa eneo hilo, wawekezaji, wanaharakati wa ndani na nje ya nchi na asasi za kiraia (NGOs). 

Kamati ya sasa iliundwa baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kufanya ziara ya kikazi mkoani Arusha Desemba, mwaka jana, ziara iliyomfikisha hadi Loliondo. 

Mbali ya Waziri Mkuu kuagiza kuundwa kwa Kamati hiyo ya Mkuu wa Mkoa, pia aliagiza maeneo yote ya uhifadhi yaainishwe na kuwekewa alama za mipaka, hatua ambayo ni muhimu sana kwa mustakabali wa uhifadhi nchini.  

Mgogoro wa Loliondo kama ilivyobainishwa awali ni wa muda mrefu, ingawaje ulichukua sura mpya mwaka 2008 baada ya Serikali kufanya oparesheni kuwaondoa wananchi waliokuwa wamevamia maeneo ya uhifadhi.

Baada ya kufanyika kwa oparesheni hiyo ambayo ilifuata taratibu zote, ikiwamo kuwapa taarifa kabla wananchi waliokuwa wamevamia maeneo ya uhifadhi kupitia serikali za vijiji na viongozi wa kimila, kukaibuka tuhuma nzito za ukiukwaji wa haki za binadamu uliodaiwa kufanywa na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliofanya kazi hiyo. 

Baada ya kelele nyingi kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchini, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii wakati huo, mama Shamsa Mwangunga, aliunda kikosi kazi kuchunguza tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu, lakini pia kikosi kazi hicho kilitakiwa kufanya utafiti na kuishauri Serikali nini cha kufanya ili kumaliza mgogoro huo. 

Kikosi hicho kiliundwa na maofisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Maliasili na Utalii, Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi, Tume ya Haki za Binadamu, TAMISEMI, Jeshi la Polisi, pia vyombo vya habari vilikuwa na mwakilishi.

Kikosi kazi hicho kilikaa Loliondo kwa takribani wiki mbili, ambapo katika kipindi hicho kilifika katika maeneo yote yenye mgogoro na kuonana na wahusika wote akiwamo binti aliyedaiwa kubakwa na askari wa FFU, tuhuma ambayo ilipigiwa kelele sana na kwa kiasi kikubwa ililichafua Jeshi la Polisi. 

Miongoni mwa wadau waliohojiwa na kikosi kazi hicho ni pamoja na madiwani, Mbunge, wazee wa kimila, wanawake walioguswa na oparesheni, viongozi wa vijiji, uongozi wa wilaya, NGOs zote, wawekezaji wote katika eneo hilo na polisi walioshiriki katika oparesheni hiyo na wanahabari walioripoti tukio hilo. Hakuna mhusika ambaye hakuhojiwa. 

Ripoti ya kikosi kazi hicho ipo Wizara ya Maliasili na Utalii na ndani ya ripoti hiyo utakuta tuhuma karibu zote zilizotolewa hazikuwa kweli, hakuna binti aliyebakwa, haki za binadamu hazikukiukwa na kubwa zaidi ilipendekezwa eneo hilo linalokadiriwa kuwa na ukubwa wa kilometa za mraba 4000, ligawanywe kama njia ya kuepuka mgogoro mwingine siku za usoni. 

Ushauri huo ulitokana na dalili za wazi kabisa za uharibifu mkubwa wa mazingira na uvamizi wa maeneo ya uhifadhi kwa ajili ya malisho ya mifugo na kilimo wakati huo, lakini kwa kuwa ushauri huo haukufanyiwa kazi, matokeo yanaonekana dhahiri hii leo, Loliondo imeharibika kabisa. 

Kwa wale ambao wamekuwa wakiufuatilia mgogoro wa Loliondo, sidhani kama kuna kamati au tume ambayo ilifanya kazi au itafanya kazi zaidi ya iliyofanywa na kikosi kazi hicho. 

Kama ilivyo sasa, kelele hazikuisha wakati huo, hivyo zikaundwa kamati zingine kwenda Loliondo ikiwamo Kamati ya Waziri Mkuu iliyojumuisha maofisa kutoka wizara kadhaa, pia Kamati ya Bunge ya Maliasili na Mazingira nayo ikaenda Loliondo. 

Lakini mwisho wa siku ushauri ukawa ule ule, kwamba eneo hilo ligawanywe. Kilometa za mraba 1,500 zitengwe kwa shughuli za uhifadhi na nyingine wapewe wananchi na kujipangia matumizi yake. 

Jambo la msingi hapa ni kwamba, kamati zote zilizokwenda Loliondo zilitumia mamilioni ya fedha za walipa kodi, pia zilitumia muda mwingi wa watendaji, muda ambao ungeweza kutumika kufanya shughuli zingine za maendeleo. 

Katika hali ya kushangaza kabisa, baada ya kamati zote kwenda Loliondo na kutoa mapendekezo, Serikali ilikaa kimya bila kufanyia kazi ushauri wa kitaalamu uliokuwa na lengo la kumaliza mgogoro na kulihifadhi eneo hilo muhimu kwa ikolojia ya Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Eneo la Loliondo linalopakana na Serengeti lina umuhimu wa pekee, kwa sababu ndipo vilipo vyanzo vya maji ukiwamo mto Grumeti, pia ni eneo la mapito na mazalia ya wanyamapori.

Ikolojia ya Serengeti au Hifadhi ya Taifa Serengeti imezungukwa na Hifadhi ya Masai Mara (Kenya) kwa upande wa Kaskazini, hifadhi za Ikorongo na Grumeti upande wa Magharibi, Hifadhi ya Maswa upande wa Kusini/Magharibi, Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro upande wa Kusini/Mashariki na Pori Tengefu Loliondo upande wa Mashariki. 

Maeneo yote haya yanayopakana na Serengeti yamehifadhiwa isipokuwa Loliondo, pamoja na ukweli kuwa Loliondo ina umuhimu kwa kipekee kulinganisha na maeneo mengine. 

Kwa kawaida watendaji au wataalamu serikalini huwa hawabadiliki kama viongozi wa kisiasa, ambao hubadilika kutokana na mabadiliko yatokanayo na uteuzi mbalimbali au uchaguzi, kwa lugha rahisi Serikali kwa maana ya watendaji ni ile ile. 

Hata kama Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) isingekuwa madarakani hii leo, watendaji wa wizara na asasi zingine za umma wangebaki kuwa wale wale. 

Jambo la kujiuliza kwa nini Serikali inaendelea kupoteza fedha na muda mwingi wa watendaji wake kwa suala la Loliondo, suala ambalo limeshafanyiwa kazi na utafiti kwa kina kabisa? 

Mathalan, sidhani kama Kamati ya sasa chini ya Mkuu wa Mkoa itakuja na lolote jipya, pia hata baadhi ya wajumbe wa kamati sidhani kama wana mchango wowote ule, kwa sababu suala la Loliondo ni suala la kitaalamu, si suala la kisiasa. 

Hivyo mtu kama Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Lekule Laizer na wanasiasa wengineo ni vigumu kujua wamo kwenye kamati kufanya nini. Ni vema kuwaacha wanasiasa wafanye siasa na wataalamu wafanye kazi za kitaalamu, tukifikia hatua hiyo, nchi itasonga mbele kimaendeleo kwa kasi tunayoitamani. 

Kama Serikali iliona kuna umuhimu mkubwa, basi kazi inayofanywa sasa na Kamati ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha ilipaswa kufanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi, Wizara ya Kilimo na Mifugo na TAMISEMI, ingawaje la msingi zaidi ilikuwa Serikali kutekeleza mapendekezo ya tume za awali. 

Lakini kwa utaratibu huu wa kila mara kuunda tume kufanya kazi ambazo zilishafanyika, utaendelea kugharimu fedha nyingi na muda, na kamwe suluhu haitapatikana Loliondo, na miaka michache ijayo hatutakuwa na Loliondo tena.

Pia Serikali lazima iingie ndani na kwenye vilindi vya mgogoro huu na kupambana na watu hasa NGOs ambazo kuendelea kwa mgogoro Loliondo, ndio zinapata uhalali wa kuendelea kuwapo na kupata fedha. 

Hata sinema za kijinga ambazo kwa siku kadhaa sasa tunashuhudia kina mama wa kabila la Wamasai wakilala barabarani kuzuia misafara ya viongozi wanaokwenda eneo hilo, ni matokeo ya uchochezi unaofanywa na NGOs na wanaharakati wengine wenye nia ovu. 

Ni wakati sasa Serikali ifanye maamuzi magumu yenye tija kwa Taifa, kwa kufuata na kutekeleza ushauri wa kitaalamu katika kupata suluhu ya kudumu Loliondo, ili kulinda uhifadhi na kusimamia maslahi ya wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles