ELIMU ni ufunguo wa maisha ni kaulimbiu iliyoanza kusikika tangu tulipopata uhuru wa nchi yetu, ambayo inabeba dhima kubwa na pana zaidi kuliko inavyodhaniwa na wengi wetu.
Taasisi ya Dar es Salaam Mentally Handcapped Children support group ilisajiliwa Juni, 1993 ikiwa na malengo ya kusaidia watoto wenye ulemavu wa akili, hasa katika sekta ya elimu.
Mariamu Zialor ni Mratibu wa taasisi hiyo, anasema mwaka 1993 waligundua kulikuwa na uhaba wa shule zilizokuwa zikitoa elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu.
“Shule maalumu moja iliyokuwa Mtoni ililea na kutoa elimu kwa wanafunzi 50, Shule ya Msingi Wailes ilikuwa na madarasa mawili ilikuwa inatoa huduma ya mafunzo ya awali kwa watoto 40, na Shule ya Msingi Uhuru mchanganyiko ilikuwa na madarasa mawili ya watoto 30 wenye mahitaji maalumu, hasa wenye ulemavu wa akili,” anasema Mariamu.
Anasema baada ya utafiti huo waligundua mahitaji ya watoto wenye ulemavu wa akili ni makubwa na kwamba wazazi wanapokwenda shule za msingi kuwaandikisha hujibiwa kuwa hakuna huduma hiyo.
“Tuligundua pia hakukuwa na walimu wenye ujuzi wa kufundisha watoto hao na hakuna madarasa ya kusomea,” anasema.
Anasema Mwalimu Dietric Mkwera, aliyekuwa anafundisha kitengo maalumu cha watoto wenye ulemavu wa akili katika Shule ya Uhuru Mchanganyiko alisaidia kutoa elimu kwa taasisi hiyo kuhusu mahitaji ya watoto wenye ulemavu hasa wenye ulemavu wa akili.
“Kuanzia hapo tukahamasika na kujikita kutoa msaada kwa kundi hili la wenye ulemavu hasa wa akili kwa kuwa wenye ulemavu wa macho na wasiosikia pamoja na wale wa viungo wamekuwa wakipewa kipaumbele kupata elimu kuliko hawa wenye ulemavu wa akili,” anasema Mariam.
Mariamu anasema kundi hilo walikuwa wananyanyapaliwa kuanzia nyumbani, mtaani, na katika jamii.
“Watu wengi wamekuwa wakijiuliza kama mwenye ulemavu wa akili ataweza kusoma hadi kiwango gani na je, ataweza kufanya kazi?” anasema.
Anasema baada ya kutambua umuhimu wa elimu na changamoto wanazokabiliana nazo watoto wenye ulemavu wa akili ndipo taasisi hiyo iliamua kuanza mchakato wa kujenga miundombinu na kutoa misaada kwa watoto wenye ulemavu huo.
“Tulianza kujenga madarasa kwa ajili ya watoto hao ambapo hadi mwaka jana tumeweza kuzifikia shule za msingi 16,” anasema.
Anasema katika ujenzi huo wamekuwa wakijenga jengo lenye madarasa matatu na vyoo viwili maalumu kwa wanafunzi hao.
“Kila darasa lina uwezo wa kuchukua watoto 10, si kwa sababu ni dogo bali ndio utaratibu wa kufundisha watoto wenye ulemavu wa akili, wakizidi hapo katika darasa moja kazi ya kufundisha inakuwa ngumu kwa mwalimu.
“Kwa kuwa kuna upungufu mkubwa wa walimu maalumU ambao wamesomea kufundisha watoto hao tumeshuhudia watoto 20 ndani ya darasa moja jambo ambalo ni changamoto kwa sababu mwalimu anashindwa kuwasaidia wanafunzi wake na kuchelewesha maendeleo yao kimasomo,” anasema.
Anasema mwanafunzi mwenye ulemavu wa akili ana uwezo tofauti na mwenzake na kasi ya kuelewa ni tofauti na huwa hawatulii, mwalimu anapata changamoto kufundisha zaidi ya watoto 10 katika darasa moja.
Upatikanaji wa fedha
Akizungumzia upatikanaji wa fedha za miradi hiyo, anasema walianza kwa kujitolea wenyewe pamoja na kuomba msaada katika taasisi mbalimbali za kibiashara na serikali.
“Tulipoanza kufanya kazi hii haikuwa ngumu kuomba msaada kutoka taasisi za kibiashara, za serikali na za binafsi kwa kuwa hakukuwa na taasisi nyingi ambazo zilikuwa zikifanya kazi kama hii.
“Tuliweza kuandaa chakula cha usiku au cha mchana na kualika wachangiaji ambapo kwa kipindi cha kwanza tuliwapata wengi,” anasema Mariamu.
Mahitaji
Mariamu anasema awali Mwalimu Mkwera ndio aliyewafahamisha shule zenye mahitaji.
“Kuna baadhi ya shule ambazo zilikuwa na watoto hawa lakini hazikuwa na madarasa, walimu na miundombinu rafiki kwao. Baadaye tulikuwa tunatafutwa na walimu wakuu waelewa kutueleza kuwa shule zao zinahitaji miundombinu ya madarasa, vyoo na walimu.
“Tunapokubali ombi tunawaeleza walimu wakuu watuandikie barua ya ombi kwa kuipitisha kwa ofisa elimu manispaa, mratibu wa elimu maeneo yao na mhandisi wa manispaa anashirikishwa wakati wa ujenzi,” anasema Mariamu.
Anasema baada ya kupokelewa ombi hilo shule husika hutengewa bajeti ya chakula kwa watoto na kuandaliwa walimu wa elimu maalumu wakati ujenzi ukiendelea.
Naye Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Rose Rupia, anaeleza shule zilizonufaika na mradi huo ambapo anasema shule nyingi za jiji la Dar es Salaam zimepata huduma hii.
“Shule ambazo zimenufaika ni Uhuru Mchanganyiko, Umoja, Gongo la Mboto na Kipawa ambayo hata hivyo hatujui walikohamishiwa watoto hao baada ya shule hiyo kuvunjwa kupisha ujenzi wa uwanja wa ndege,” anasema Rose.
Anasema shule zingine zilizopata huduma hiyo ni Shule ya Msingi Msewe, Kawe A, Kigamboni, Mjimwema, Msasani, Mbagala Kuu, Mbagala Majimatitu, Kilimani, Mbuyuni, Rutihinda, Kibamba, na Tandika.
“Tunajivunia kuongezeka kwa idadi wa watoto wenye ulemavu wa akili wanaopata huduma ya elimu ya msingi ambayo ni haki yao kutoka 120 tulipoanza kazi hii hadi kufikia 430 walioandikishwa shule maalumu kwa Mkoa wa Dar es Salaam.
“Wanafunzi wamefaidika kwa kupata elimu hii kutoka kwa walimu maalumu ambapo sasa wana uwezo wa kufanya kazi ndogo ndogo na kuwa msaada nyumbani kuliko awali walikuwa mzigo kwa wazazi,” anasema Rose.