32.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 12, 2024

Contact us: [email protected]

RC Makonda: Nitakamata mwenyewe wanafunzi wachafu

msaadaNa Asifiwe George, Dar es Salaam

BAADHI ya viongozi wa serikali hapa nchini, wamekuwa wakipigia debe suala la usafi wa mazingira hasa katika Jiji la Dar es Salaam akiwemo Rais Dk. John Mafuguli, ambaye alionyesha mfano katika siku ya sherehe za Uhuru ambapo aliungana na Watanzania kufanya usafi katika maeneo mbalimbali nchini.

Pia jitihada hizo zimeonekana kuwa endelevu ambapo viongozi wengi wamekuwa wakihamasisha suala la usafi katika maeneo mbalimbali lengo likiwa ni kuondokana na magonjwa ya milipuko.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amewataka wanafunzi wa shule za msingi Wilaya ya Kinondoni kuwa mabalozi wa usafi na kuacha kutupa taka ovyo barabarani na kuahidi kuwa atakayembaini kuwa mchafu yeye mwenyewe atamkamata.

Makonda alitoa kauli hiyo hivi karibuni, wakati akikabidhiwa madawati 500 yenye thamani ya Sh milioni 82.5 na Kampuni ya Simu za mkononi ya Tigo Tanzania.

Katika makabidhiano hayo yaliyofanyika katika Shule ya Msingi kawawa iliyopo Kigogo Luhanga, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaama, makonda alisema; “Tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa Kampuni ya  Tigo kwa kuwa mdau muhimu kwetu katika jitihada  zinazoendelea za kujaribu kupunguza tatizo la ukosefu wa  madawati ya kutosha katika shule za msingi za mkoa wetu  wa Dar es Salaam.

“Ni dhahiri kwamba msaada huu wa madawati 500 utawawezesha mamia ya wanafunzi wetu kupata sehemu za kukaa na hivyo kujipatia elimu katika mazingira bora zaidi.”

IMG_2914Makonda pia alisisitiza suala la usafi kwa wanafunzi ambapo anasema; “ni aibu wanafunzi wa shule ya msingi kutoka Wilaya ya Kinondoni kuwa wachafu na kufeli katika masomo yenu, mnatakiwa kuwa mabalozi wa usafi kuanzia nyumbani kwenu, shuleni hata mnapoona makopo yamezagaa barabarani muyaokote na watakaokuwa wachafu mimi mwenyewe nitawakamata,” anasema Makonda.

Anasema wanafunzi 1500 watanufaika na madawati hayo ambapo kutokana na ubora wake yatadumu kizazi na kizazi, hivyo anawataka wasiwe miongoni mwa wanaoshindwa kufikia malengo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwamo ya madawati.

Makonda anasema madawati hayo yataboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto katika Wilaya ya Kinondoni na kuwataka wadau wengine kuunga mkono ili kuweza kupunguza changamoto ya madawati katika Jiji la Dar es Salaam.

Anasema madawati hayo yamegawanywa katika shule 10 ambazo ni Kawawa, Makabe, Upendo, Bunju ‘A’, Sakasala, Malamba Mawili, Tegeta ‘A’, Mbezi juu, Mtongani na Wazo hili ambapo kila shule itapata madawati 50.

Ukosefu wa madawati katika shule ni moja ya changamoto inayozikabili shule nyingi nchini pamoja na kwamba Serikali imekuwa na mipango mikakati ya kuhakikisha kwamba kila shule inakuwa na madawati ya kutosha.

Makonda anasema usafi wa mazingira ni njia ya kuendeleza afya kwa kuzuia mawasiliano ya binadamu na athari za taka. Athari hizo zinaweza kuhusu mwili, mikrobiolojia, biolojia au kemikali vikolezo vya ugonjwa.

Anasema taka ambazo zinaweza kusababisha matatizo ya afya ni kinyesi cha binadamu na wanyama, taka ngumu, maji machafu, taka za viwandani, na taka za kilimo.

“Usafi kama njia ya kuzuia maradhi unaweza kutumika kwa ufumbuzi (kama majitaka na tiba ya maji machafu), teknolojia rahisi kama vyoo, au matendo ya usafi binafsi (kama uoshaji wa mikono kwa sabuni).

“Upungufu wa usafi wa mazingira ni sababu kuu ya maradhi duniani kote. Uboreshaji wa mazingira una manufaa makubwa kwa afya ya wote katika kaya na katika jamii,” anasema Makonda.

Makonda anaongeza kuwa usafi wa mazingira unahusu pia udumishaji wa ratiba ya usafi, kwa njia ya kutenga siku maalumu mara moja kwa wiki kusafisha maeneo yote ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa taka na maji machafu.

Mbali na sula la usafi Makonda anasema walimu wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwa ni pamoja na upandaji wa madaraja hivyo aliwataka walimu wote kukutana Machi 26 mwaka huu ili kujadili changamoto zinazowakabili.

Anasema sababu zinazosababisha walimu kutopanda madaraja ni kutokana na kuwapo kwa mafisadi walioweka wafanyakazi hewa kwa faida ya matumbo yao.

Anaeleza kuwa kazi ya ualimu ni wito hivyo wataendelea kufuatilia walimu hewa ikiwa ni pamoja na kila shule kupeleka idadi ya walimu wake na kuwahakikishia kuwa changamoto hiyo inakwisha.

Naye Mkurugenzi Mkuu waTigo, Diego Gutierrez, anasema mchango wa madawati hayo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya kampuni hiyo ya kuunga mkono jitihada mbalimbali za kuleta maendeleo ya elimu nchini.

Anasema huo ni mchango kwa ajili ya kuisaidia Serikali kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madawati katika shule za msingi nchini.

“Mchango huu ni sehemu ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Tigo katika kusaidia utekelezaji wa miradi yenye tija kubwa kwa jamii, Tunaamini kwamba kupitia msaada huo tunatoa mchango wetu katika kujenga viongizi wa baadaye wa Taifa hili na wataaluma mbalimbali wakiwamo madaktari, wahandisi na wengineo,” anasema Gutierrez.

Pia hivi karibuni Tigo imechangia madawati 400 yenye thamani ya Sh milioni 60 kwa shule 10 za mzingi mkoani Morogoro ambapo walikabidhi tena msaada kama huo katika shule za msingi za mikoa ya Shinyanga, Mbeya na Iringa.

Ofisa elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Raymond Mapunda, anasema pamoja na kupata msaada huo lakini kuna upungufu wa madawati 66,000 na wanafunzi 82,000 hawana pa kukaa.

“Kutokana na changamoto hii tunawaomba wadau kujitokeza ili kuweza kumaliza changamoto hiyo na wanafunzi wetu wasome bila usumbufu,” anasema Mapunda.

Anasisitiza kuwa suala la usafi wa mazingira shuleni ni jambo la muhimu, lakini ipo changamoto ya maji hivyo wapo katika utekelezaji wa kuchimba visima vitatu katika baadhi ya shule za msingi latika Wilaya ya Kinondoni ambazo maji yanapatikana kwa shida.

Suala la uchafu kwa wanafunzi limekuwa ni la kawaida kwani si ajabu kukutana na mwanafunzi hata wa darasa la kwanza kumuona amejaa vumbi mwili mzima.

Hivi majuzi katika maadhimisho ya uboreshaji wa mazingira katika shule za msingi na sekondari kwa Manispaa ya Ilala, Mkuu wa wilaya hiyo, Raymond Mushi, alisisitiza usafi wa mazingira huku akishauri kwamba uendane na utoaji wa elimu bora kwa kuweka mazingira rafiki ya kufundishia.

“Mazingira rafiki kwa wanafunzi yanawafanya kupenda shule hatimaye kuachana na utoro jambo ambalo litaongeza ufaulu katika mitihani ya mwisho,” anasema Mushi.

Anasema asasi pamoja na sekta za umma zinapaswa kuhakikisha suala la elimu ya mazingira na usafi linapewa kipaumbele katika maeneo yao ya kazi.

Anasisitiza kuwa kila mtu kwa nafasi yake anatakiwa kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira kulingana na sheria zinavyoelekeza na watu waliopewa mamlaka ya kusimamia mazingira kuhakikisha zinafanya kazi kwa bidii.

“Uchafu wa mazingira huathiri watu wote hivyo, ni vema kila mtu akafanya usafi kwa nafasi yake bila kumsubiri mtu mwingine,” anasisitiza Mushi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles