29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge aeleza alivyokwepa mtego wa rushwa

jobNa Mwandishi Wetu

MMOJA wa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ambaye kamati yake imetuhumiwa kuhusika na rushwa, ameeleza jinsi alivyotaka kupewa fedha zinazodaiwa kuwa za rushwa na moja ya idara za Serikali, lakini akazishtukia na kuzikataa.

Mbunge huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, amesema wakiwa katika moja ya vikao vya kamati aliitwa na kiongozi wake na kuambiwa wameitiwa ‘lunch’ (chakula cha mchana), lakini si kwa maana ya kupatiwa chakula, bali fedha.

“Nilikuwa kwenye majukumu yangu, nilipoambiwa kuna ‘lunch’, yaani fedha kutoka kwenye moja ya idara tulizokuwa tunazikagua, niliwasiliana na Katibu wa kamati yetu kumuuliza kama jambo hilo lipo sawa sawa na akanishauri kwamba nisishiriki,” alisema Mbunge huyo.

Siku tatu baada ya kuibuka kwa kashfa ya rushwa miongoni mwa wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) tayari imewaita kuwahoji wabunge waliokuwa wanaunda kamati tano zilizofanyiwa mabadiliko na Spika Job Ndugai.

Zaidi ya wabunge saba tayari wameitwa na kuhojiwa na Takukuru, wakiwamo wale waliotajwa kuhusika kuomba rushwa na ambao hawajatajwa.

Baadhi ya wabunge walioitwa kuhojiwa Takukuru juzi licha ya kuwasilisha barua ya kujiuzulu kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai baada ya kusikia tuhuma hizo ni pamoja na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe na wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe.

Taarifa za kuwepo kwa rushwa zimeibuka hivi karibuni, huku Spika wa Bunge, Ndugai, akifanya mabadiliko ya baadhi ya wajumbe wa kamati na kuwaondoa baadhi ya wenyeviti wa kamati hizo.

Katika mabadiliko hayo yaliyowagusa wabunge 27 na kamati tano za Bunge, Spika Ndugai ametoa maelekezo ya kujazwa kwa nafasi zao zilizoachwa wazi na wenyeviti na makamu wenyeviti mara moja.

Hata hivyo, akizungumza hivi karibuni, Ndugai alisema mabadiliko hayo hayana uhusiano na tuhuma za rushwa.

“Tumefanya mabadiliko ya kamati kwa lengo la kuboresha tu utendaji, ni kama kocha una timu yako unataka kukiimarisha tu kikosi, wala siyo tuhuma za rushwa,” alisema Ndugai.

Kwa upande wake Zitto, alithibitisha kupata wito kutoka makao makuu ya Takukuru ili kuhojiwa juu ya sakata hilo na akapongeza kuwa endapo vyombo vya Serikali vitakuwa makini kushughulikia tuhuma zote zinazoelekezwa kwa wanasiasa na watumishi wengine wa umma, itasaidia kuongeza uwajibikaji na kupunguza uzushi kwa wananchi.

“Nimepata wito huo kupitia Ofisi ya Bunge. Nasikia Bashe ameitwa pia. Nafurahi wito wetu wa uchunguzi umechukuliwa kwa uzito unaostahili na tutatoa ushirikiano wote kwa vyombo vya uchunguzi ili kumaliza zoezi hili kwa haraka na kwa ufanisi,” alisema Zitto.

Alipoulizwa na gazeti hili sababu ya kukimbilia kujiuzulu mapema, Zitto alijibu kupitia mtandao wa Whatsapp kuwa uamuzi huo ulilenga kuvishinikiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi ili kubaini ukweli.

“Kujiuzulu kwangu ni kushinikiza uchunguzi. Ni namna tu ya kutaka jambo hilo lipewe uzito unaostahili…Kwa uelewa wangu, najua hakuna lolote. Nilikuwa kwenye kamati siku nzima sikuona linalozungumzwa.

“Kama kuna watu walikuwa na mchezo, hilo silijui. Muhimu kwangu ni kwa kamati yetu kuchunguzwa na kama kuna waliofanya kinachofanywa wachukuliwe hatua,” alisema Zitto.

Hadi kufikia Machi 24, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilikuwa imeshawahoji wabunge zaidi ya saba.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu zoezi hilo, Mkurugenzi wa Takukuru, Kamishna Valentino Mlowola, alikataa kuzungumzia mwendelezo wake, akisema yuko kanisani.

“Leo ni lini?” aliuliza Kamishna Mlowola na mwandishi alipomjibu kuwa ni Ijumaa, alisema: “Naomba tuheshimiane, nipo kanisani kwa sasa.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles