32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Sura mbili vigogo wanaorudisha mabilioni kwa DPP

Na KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MSAMAHA uliotolewa kwa watuhumiwa wa kesi za uhujumu uchumi na kutakatisha fedha unaonekana kugubikwa na changamoto zinazopunguza kasi ya utekelezaji wake.

Wakati siku saba nyingine ukiacha zile za mwanzo zilizotolewa na Rais Dk. John Magufuli zikielekea kufikia ukingoni Jumatano, imebainika kuwa miongoni washtakiwa wengi wameandika ‘barua  kuomba msamaha’ na si ‘barua za kuomba msamaha na kukiri makosa yao na kurejesha fedha’.

Ushauri alioutoa Rais Magufuli kwa Mkurugenzi wa Mashataka nchini (DPP), Biswalo Mganga unaelekeza watuhumiwa hao kuandika barua kukiri makosa yao  na kuomba msamaha na kisha kurejesha kiasi cha fedha wanachodaiwa.

Kinachothibitisha kuwapo kwa hali hiyo ni  kutokana na yale yaliyojitokeza juzi Ijumaa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambako  utekelezaji wa msamaha huo  ulikwama kwa watuhumiwa takribani 50 waliotoka katika Gereza la Segerea na Keko.

Miongoni mwa watuhumiwa hao na wale waliofikishwa kabla baadhi walibainika kuomba msamaha pasipo kukiri makosa yao.

Hali hiyo ni kama aliiona mwanzo Rais magufuli mwenyewe baada ya utekelezaji wa ushauri wa siku saba alizozitoa mwanzo.

Wakati DPP akimkabidhi taarifa ya utekelezaji wa ushauri huo Septemba 22 mwaka huu, Rais Magufuli  alisema wapo watuhumiwa wanaodanganywa kwamba msamaha huo ni wa uongo na kwamba mtuhumiwa anakuwa amejishtaki mwenyewe.

Rais Magufuli aliwataka watuhumiwa hao wasiamini maneno hayo kwa kuwa msamaha ukitolewa lazima uwe msamaha.

MTANZANIA Jumapili limebaini kuwa baadhi ya watuhumiwa bado wanahofu hiyo na ndiyo msingi wa kuandika barua za kuomba msamaha pasipo kukiri makosa yao kwa kuwa wanaamini rekodi zao zinaweza kuwahukumu.

Mfano wa watuhumiwa hao ni raia wa China, Cheng Guo anayeshtakiwa kwa kusafirisha nyara za Serikali aliyechafua hali ya hewa baada ya kukana kuandika barua ya kuomba msamaha na kukiri makosa ya kusafirisha nyara hizo zenye thamani ya Sh 267,407,400.

Mshtakiwa huyo anayedaiwa kusafirisha meno ya tembo na kucha za Simba alikuwa miongoni mwa washtakiwa wengi waliotolewa gerezani kuletwa mahakamani kwa ajili ya kukiri makosa kutokana na barua walizoandika.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon aliiwakilisha Jamhuri mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi alidai mshtakiwa aliandika barua ya kuomba msamaha.

“Uliandika barua ya kukiri makosa? alihoji Hakimu Shaidi.

Mshtakiwa alijibu hapana, hakuandika barua ya kukiri makosa, yeye aliandika barua ya kulalamika upelelezi kuchelewa na kuomba msamaha.

“Sijaandika barua ya kukiri makosa, sina hela za kulipa,”alidai.

Jambo jingine linalowatia hofu baadhi ya watuhumiwa, ni kutojua kile kitakachoamriwa mbele ya mahakama baada ya kukiri na kuomba msamaha na kwa kuzingatia pia kwamba Rais Magufuli mwenyewe na hata DPP wamesisitiza mchakato huo lazima umalizike kupitia mahakamani walikoingilia.

Aidha kauli ya DPP wakati akitoa taarifa ya utekelezaji kwamba  mtu mmoja aliyekubali kuitikia wito huo baada ya kukiri kosa mahakamani na kulipa Sh bil 1.4 moja kwa moja lakini bado Mahakama ikamtoza faini ya sh milioni tano kutokana na kukiri kosa ndiyo ambayo baadhi ya watuhumiwa wanaona inawafanya washindwe kubashiri  kile ambacho mahakama nayo itaamua baada ya kukiri makosa yao.

Hoja ya kutojipanga kwa ajili ya kutekeleza masharti ya msamaha huo nayo imeonekana kujitokeza kwa baadhi ya watuhumiwa waliofikishwa mahakamani hapo.

Baadhi ya washtakiwa wamesema hawakuwa wamefanya mawasiliano na ndugu zao kwa ajili ya kukamilisha urejeshaji wa fedha walizokiri kulipa.

Mahabusu wengi waliokuwa wakipanda kizimbani walikuwa wakilalamika kwamba wengine ndugu zao wako mikoani hawana taarifa pamoja na kwamba waliandika barua.

Miongoni mwa washtakiwa ambao hawakupata muda wa kujipanga kwa utekelezaji ni Michael Wambura ambaye aliweka wazi mahakamani kwamba hakuwa ameweka mambo yake sawasawa.

Katika barua yake kwa kujua kwamba kosa la kutakatisha adhabu yake ya chini ni faini Sh milioni 100 alisema hana uwezo wa kuwa na fedha  hizo, uwezo wake ni Sh milioni 85 hivyo anasubiri huruma ya DPP, Jumatatu  akiri  na kurejesha kiasi atakachokubaliwa.

Baada ya Rais John Magufuli kutangaza msamaha huo, DPP amekuwa akipokea barua nyingi ofisini kwake ambazo ameweza kuzishughulikia na kuyafikisha majalada ya baadhi ya watuhumiwa hao mahakamani Ijumaa.

Wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa siku saba za mwanzo za msamaha ambapo watuhumiwa 467 wameandika barua, DPP alisema kuwa wanalazimika kukaa kusoma na kuchambuan kwa kina majalada ya watuhumiwa waliopokea wito huo  ili kuangalia yapi wanakubaliana nayo na  yapi ya kurekebisha mashataka  na kwenda nayo mahakamani kwa mujibu wa sheria ili watuhumiwa hao waweze kulipa mahakamani na isitokee katika siku zijazo wakatumia mbinu nyingine kuishtaki serikali.

MAHAKAMA KUZIDIWA

Aidha kutokana na mwitikio wa msamaha huo kuwa mkubwa, kabla na baada ya siku saba za sasa, kuna uwezekano wa Mahakama kuzidiwa kutokana na muda  mchache  na barua kuwa nyingi.

Siku ya Ijumaa watuhumiwa walikuwa wengi na kufanya mahakama ifanye kazi hadi muda wa jioni.

Gazeti hili lilishuhudia baadhi ya kesi zikichukua muda mwingi hasa kwa upande zile zenye mashtaka mengi.

Mshtakiwa ama washtakiwa wanapoingia mahakamani husomewa upya mashtaka yanayomkabili ama kuwakabili kulingana na walichokubaliana na DPP.

Mshatakiwa anakiri makosa hayo, anasomewa maelekezo ya awali, kama kuna vielelezo vinatolewa kisha mahakama inatoa adhabu ya faini kwa mujibu wa sheria na adhabu ya kifungo endapo atashindwa kulipa faini.

Adhabu ya chini kwa makosa ya kutakatisha fedha ni faini Sh milioni 100 na adhabu ya juu kwa faini ni Sh milioni 500 .

MAHAKIMU

Aidha kutokana na zoezi hilo kuwa ni la muda maalum baadhi ya wadau wa mahakama wanaona kuna haja ya kuweka utaratibu maalum kwa mahakimu wa kesi husika.

Hilo linatokana na kile kilichotokea Ijumaa kwenye kesi ya vigogo wa NIDA ambao kesi yao haikuweza kusikilizwa kwa sababu Hakimu Mkazi Mwandamizi, Salum Ally hakuwepo.

Kwa sababu hiyo wadau hao wameshauri kuangalia namna nyingine ya kuharakisha utekelezaji wa ofa hiyo kwa kuyagawa mafaili kwa mahakimu wengine ikitokea muhusika hayupo vinginevyo mtuhumiwa atakosa kupata haki hiyo ya kusamehewa kama alivyoomba.

Aidha kwa siku mbili za mwishoni mwa wiki ambazo watuhumiwa walianza kufika kukiri baada ya barua zao kupitiwa kumeonekana ongezeko kubwa la wananchi wanaofurika mahakamani kufatilia ndugu na jamaa zao.

Ni mazingira kama hayo pia wadau hao wanaona kuna haja pia kwa Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi katika mahakama zote ambazo zinatekeleza ofa kwa ajili ya usalama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles