23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mkurugenzi mpya NEC awapa neno wanaohoji uteuzi wake

Na GRACE SHITUNDU-DAR ES SALAAM

MKURUGENZI mpya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Dk. Wilson Mahera  ambaye uteuzi wake umezua mjadala kutokana  na kuhusishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM),  amesema kwa sasa hana  chama na anajipanga kuwajibu wanaomuhisha na jambo hilo.

Dk. Mahera, ambaye awali alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Arusha, amerithi mikoba ya Dk. Athumani Kihamia baada ya kuteuliwa wiki hii na Rais Dk.John Magufuli kushika nafasi hiyo.

Tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo, kumekuwa na mjadala mkali  huku baadhi ya wanasiasia wakipinga uteuzi wake kwa hoja kwamba Dk. Mahera kwa nafasi hiyo mpya hawezi kutenda haki kwani ni kada wa CCM na rekodi zinaonyesha  amewahi kugombea ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya  CCM (NEC) akitokea Mkoa wa Mara.

Kwa sababu hiyo wanaona ni kinyume na Katiba nafasi hiyo kushikiliwa na mtu kama yeye hasa kwa kuzingatia hata nafasi aliyotoka ya Ukurugenzi wa Halmashauri ya Arusha tayari ilikuwa imepingwa mahakamani.

MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Dk. Mahera ambaye tangu hoja hizo zielekezwe kwake hajawahi kuzungumza chochote.

Katika mazungumzo yake na MTANZANIA Jumapili  alisema kwamba yeye ni  mkurugenzi na sio mwanachama wa chama chochote.

“Hayo mambo sitaki kuyaongelea sasa hivi  lakini  kifupi tu, mkurugenzi yoyote yule hana chama.

“Kama ambavyo sikuwa mwanachama wakati nikiwa Mkurugenzi Mtendaji katika Halmashauri ya Arusha hata sasa mimi si mwanachama wa chama chochote,”alisema Dk. Mahera.

Alipoulizwa anazungumziaje mjadala unaondelea kuhusu kuhusishwa na CCM, Dk Mahera alisema kwa sasa hawezi kuzunguzia chochote.

‘Hayo mambo siwezi kuyazungumzia kwa sasa lakini nikipata muda nitakuja kuyatolea ufafanuzi,” alisema.

Kama ilivyo kwa Dk.Mahera, hatua ya Rais Magufuli kumteua  Omary Ramadhani Mapuri kuwa Kamishna wa NEC nayo imekuwa ikipingwa vikali.

Hoja hiyo iliwahi kumlazimisha Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Semistocles Kaijage kuitolea ufafanuzi baada ya kuulizwa na wahariri katika mkutano wa NEC na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura miezi kadhaa iliyopita.

Jaji Kaijage alilazimika kuzungumzia uteuzi wa Mapuri ambaye alipata kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Waziri wa Mambo ya Ndani na baadae balozi baada ya kuulizwa ni namna gani NEC inajitenga na malalamiko kwamba baadhi ya watendaji wake ni makada wa chama hicho tawala.

Katika majibu yake Jaji Kaijage alisema; “NEC hakuna mwanachama hai wa chama chochote, kuna historia kwamba ulitoka hapa ukaenda pale, ulikuwa hivi na ukawa hivi, lakini hakuna utaratibu kwamba utabaki katika nafasi hiyo hiyo, hiyo ni historia tu.

“Mimi niwahakikishie tu kama kuna mtu alikuwa mwanachama wa chama fulani anabanwa na masharti ya Katiba, na wale ambao wamepata kuwa viongozi wa vyama vya siasa kuna fomu maalumu ya kujaza. Kuna kiapo ‘una-declare’  kuondoka, hakuna hata shabiki ndani ya tume, Katiba na sheria zinatubana,” alisema Jaji Kaijage.

Miongoni wa wanasiasa wanaopinga uteuzi wa sasa wa Dk. Mahera ni Mbunge wa Kigoma Mjini, (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe ambaye amesema  amewaelekeza wanasheria wa chama chake kutizama namna ya kuchukua hatua dhidi ya uteuzi huo wa Dk. Mahera.

“Nimewaelekeza Wanasheria wa chama chetu kutazama namna ya kuchukua hatua za kisheria dhidi ya uteuzi wa kada wa CCM kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ( NEC ) licha kuwepo shauri mahakama ya rufaa kuhusu suala la makada wa CCM kutosimamia chaguzi,”

“Tumeshangazwa na uteuzi huo kwani rekodi zinaonyesha kwamba mkurugenzi huyo amewahi kugombea ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya  CCM (NEC) akitokea Mkoa wa Mara.

“Na jambo hilo la uteuzi wa wasimamizi  ambao wenye vyama vya siasa lipo mahakamani, na mahakama kuu ilitoa amri katika shauri alilofungua Bob Wangwe kuwa wasimamizi wa uchaguzi hawapaswi kuwa wanachama, makada au mashabiki wa vyama vya siasa,” alisema Zitto.

Alisema kutokana na hali hiyo ACT Wazalendo inashauriana na vyama vingine vya upinzani kuhusu hatua za kisheria za kuchukua na tayari kimemuagiza Wakili Jebra Kambole atazame misingi ya kisheria ili kuzuia uteuzi huo wa Mkurugenzi mpya wa NEC.

Akihojiwa na gazeti moja la kila siku ( sio Mtanzania) aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu alisema Katiba imekataza watu wanaohusika na uchaguzi kuwa wafuasi wa chama kama Mwenyekiti na makamishna wote wa Tume ya Uchaguzi pamoja Mkurugenzi wa Uchaguzi.

“Kama ilivyo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Serikali za Mitaa, Mwenyekiti na makamishna wa NEC nao ni ‘watu wanaohusika na uchaguzi’ na wamekatazwa na Katiba kuwa wanachama wa vyama vya siasa.

Pia Katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, Lissu aliandika kwamba kwa mujibu wa Katiba ya nchi, wote hawa wanatakiwa na Katiba kuwa ‘nyutro.’

Aliwataja wengine wasiotakiwa kuwa na vyama vya siasa ni pamoja na wakuu wote wa majeshi yetu ya ulinzi na usalama, wakuu wa kamandi au vikosi au taasisi nyingine za kijeshi na maafisa wengine wa kijeshi wanaopewa kamisheni zao na Rais. .

“Wanajeshi wote hawa, kama ilivyo kwa wanajeshi wengine wote, nao wamekatazwa na Katiba ya nchi yetu kuwa wanachama wa vyama vya siasa” alisema.

“Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi (TISS) na Naibu wake. Jaji Mkuu, Majaji wa Rufani, Jaji Kiongozi na majaji wa Mahakama Kuu, Msajili wa Mahakama ya Rufaa na wa Mahakama Kuu na wasajili wengine wote wa Mahakama ya Rufaa na wa Mahakama Kuu na Mtendaji Mkuu wa Mahakama. . “Wote hawa wamekatazwa na Katiba ya nchi, Sheria mahsusi pamoja na mila na desturi za kimahakama kuwa wanachama wa vyama vya siasa. Nao wanatakiwa kuwa ‘nyutro.’”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles