25.2 C
Dar es Salaam
Monday, April 22, 2024

Contact us: [email protected]

SUMAYE, MBOWE WATINGA MAHAKAMANI

Na ASHURA KAZINJA – MOROGORO


WAZIRI Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, jana walikuwa miongoni mwa wanachama wa chama hicho, waliofika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, kusikiliza kesi za wabunge wao wawili.

Sambamba na wanasiasa hao, wengine waliokuwapo mahakamani hapo ni pamoja na wabunge wa chama hicho, John Heche wa Tarime Vijijini na Devotha Minja wa Viti Maalumu.

Sumaye, Mbowe na wabunge hao, walifika mahakamani hapo jana asubuhi wakati wabunge wawili wa Chadema, Suzan Kiwanga wa Mlimba na Peter Lijualikali wa Kilombero, walipofikishwa mahakamani na wenzao 37 wanaoshtakiwa nao.

Mbali na wanasiasa hao, mahakamani hapo kulikuwa na wafuasi wengi wa Chadema, ambao hawakuruhusiwa kuingia mahakamani kutokana na ulinzi mkali wa askari polisi.

Kiwanga, Lijualikali na wenzao hao 37, walifikishwa mahakamani hapo jana kusikiliza maombi ya dhamana yao waliyoomba kupitia kwa mawakili wanaowatetea tangu walipokamatwa mwishoni mwa mwezi uliopita.

Kesi ya wabunge hao na wenzao yenye namba 296, iko mbele ya Hakimu Ivan Msack.

Katika shauri hilo, upande wa mashtaka unaongozwa na Wakili wa Serikali, Sunday Hyera na Edga Bantulaki wakati upande wa utetezi unaongozwa na Wakili Peter Kibatala akishirikiana na Mawakili Bartholomew Tarimo, Ignas Punge na Fredirick Kiwelo.

Wakati kesi hiyo ikiendelea, ulitokea mvutano wa kisheria kuhusu dhamana ya washtakiwa na hivyo Hakimu Msack kulazimika kuahirisha shauri hilo hadi leo ili kutoa fursa kwa pande zote mbili kueleza hoja zao.

Mvutano huo ulitokana na hati ya kiapo iliyowasilishwa na upande wa mashtaka uliokuwa ukipinga washtakiwa wasipewe dhamana, lakini mawakili wa utetezi walipinga hati hiyo na kutaka wateja wao wapewe dhamana.

Akiwasilisha hoja za kupinga kiapo cha kuzuia dhamana, Wakili Tarimo aliiambia mahakama kwamba kina upungufu ndiyo maana waliwasilisha hati yao ya kutaka wateja wao wapewe dhamana.

Kiwanga, Lijualikali na wenzao hao, walifikishwa mahakamani hapo Novemba 30, mwaka huu wakikabiliwa na mashtaka manane likiwamo la uchochezi, kuchoma nyumba na ofisi ya Ofisa Mtendaji wa Kata ya Sofi, iliyoko Wilaya ya Malinyi, Mkoa wa Morogoro, Novemba 26, mwaka huu.

Baada ya kufikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka yao, washtakiwa hao waliyakana na kurudishwa mahabusu.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles