29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

SUMAYE ATINGISHWA TENA

AZIZA MASOUD NA RAMADHAN LIBENANGA

-DAR ES SALAAM/MOROGORO

WAZIRI Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, amepokonywa na Serikali shamba la ekari 326 lililopo wilayani Mvomero mkoani Morogoro na kutakiwa kutokanyaga katika eneo hilo.

Taarifa za Sumaye kupokwa shamba hilo, zilianza kusambaa mapema jana asubuhi kupitia andiko lake alilolituma kupitia kundi la WhatsApp la viongozi wenzake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kabla ya baadae kulithibitisha.

Tukio hilo, Sumaye mwenyewe amelielezea kama kisasi cha kisiasa ambacho hakiwezi kumlazimisha kurudi Chama Cha Mapinduzi (CCM) na zaidi akisema anamwachia Mungu kwa kuwa yeye hatakiweza.

Sumaye ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, alihama CCM wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 sambamba na Waziri Mkuu mwenzake wa zamani, Edward Lowassa ambaye aligombea urais.

Hili ni shamba la pili kwa Sumaye kunyang’anywa na Serikali baada ya lile la ekari 33 lililopo Mabwepande – nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Oktoba 27, mwaka jana, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alitangaza kuwa wapo katika hatua ya kulifuta shamba hilo kwa madai  ya kutoliendeleza na kutoa  barua ya notisi ya siku 90.

 

ANDIKO LA SUMAYE

“Mmeamkaje? Kwangu mambo siyo mazuri, mtakumbuka baada tu ya kuingia upinzani, Serikali ilitishia muda mrefu kuchukua mashamba yangu bila sababu za msingi, hata wakati wa kampeni baadhi ya viongozi wa CCM walitamka hadharani kuwa huyu dawa yake ni kumnyang’anya mashamba yake,” ndivyo linavyoanza kusomeka andiko la Sumaye kwenda kwa viongozi wenzake wa Chadema.

“Shamba la Mabwepande ekari 33 wameagiza wiki hii halmashauri iligawe kwa wavamizi na wengineo. Jana (juzi) nimepokea barua kuwa shamba la Mvomero ekari 326 limetwaliwa na rais na sitakiwi kukanyaga hapo,”  linasomeka andiko hilo.

Sumaye alisema Serikali imefanya uamuzi huo kwa madai kuwa shamba hilo halijaendelezwa.

Kwa mujibu wa andiko lake, shamba hilo lina majengo, mazao, mashine mbalimbali, visima virefu vya maji, umeme na mifugo mchanganyiko zaidi ya 200.

“Shamba lenye vitu vyote hivyo halijaendelezwa? Mbaya zaidi katika kupinga dhamira hizo, nilifungua kesi Mahakama Kuu kwa mashamba yote na mahakama zimeweka zuio la kutokuingiliwa mashamba hayo mpaka mashauri ya msingi yatakapoamuliwa,” amesema katika andiko lake.

Sumaye alishangaa mahakama kutengwa kwenye uamuzi huo wa sasa, akisema utawala huu haufuati sheria.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili kwa simu jana, Sumaye alirejea kile alichokiandika katika andiko lake hilo, akishangaa hatua ya mashamba yote hayo kuchukuliwa wakati wanasheria wake wamekwishaweka zuio  mahakamani linaloitaka Serikali kutochukua uamuzi wowote hadi malalamiko ya awali yatakaposikilizwa.

Pengine kutokana na hayo, Sumaye alikumbusha kile alichodai kupata kuambiwa na mwana CCM mmoja ambaye hakumtaja jina kuwa “atafilisiwa mpaka atakapotembelea ndala ndiyo atakumbuka kurudi CCM”.

Hata hivyo, alisema jambo hilo  litawezekana kama Mungu ni wa CCM.

“CCM sirudi pamoja kuwa najua nitateseka na familia yangu. Kisasi hiki mimi sitakiweza, namwachia Mungu ndiye atakayetufuta machozi mimi na familia yangu,” alisema.

Sumaye aliliambia gazeti hili kuwa tayari suala hilo amekwishalifikisha kwa wanasheria wake ambao alisema wamemshauri awape muda ili waweze kulifuatilia ndipo wampe maelekezo ya kufuata.

 

DC MVOMERO

MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mohamed Utali, ambaye alisema kuwa bado hajapata taarifa rasmi kuhusu uamuzi huo.

“Bado sijapata taarifa rasmi kuhusu uamuzi huo na  endapo tutapatiwa tutatoa  taarifa kwa vyombo vya habari,” alisema kwa kifupi Utali pasipo kufafanua lolote kuhusu shamba hilo.

 

BARAZA LA MADIWANI

Hata hivyo, taarifa zilizolifikia gazeti hili, juzi kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kiliarifiwa juu ya uamuzi huo wa Serikali kuchukua shamba la Sumaye.

Inaelezwa katika kikao hicho chini ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mvomero, Jonas Zeeland, baadhi ya madiwani waliipongeza Serikali kwa uamuzi wake huo wa kulirejesha shamba hilo kwa wananchi.

Walisema shamba hilo lilikuwa halina uwekezaji wowote na kusababisha malalamiko kwa wananchi.

 

MWENYEKITI HALMASHAURI MVOMERO

Zeeland ambaye pia alizungumza na MTANZANIA Jumapili jana kuhusu kikao hicho, alisema madiwani wa  Baraza la  Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, moja ya kilio chao ni kuwapo kwa mashamba ya wawekezaji yasiyoendelezwa, likiwamo la Sumaye.

 

KAULI YA LUKUVI

Alipotafutwa kwa simu Waziri Lukuvi kuzungumzia suala hilo, alijibu kuwa aulizwe Sumaye mwenyewe.

“Muulize Sumaye mwenyewe, mimi silijui, nipo kwenye mkutano sasa hivi, nitafute baadae,” alisema.

Baadae Lukuvi alipiga simu chumba cha habari na kusema kuwa suala hilo atalifafanua kesho katika mkutano na waandishi wa habari mjini Morogoro.

“Leo acha nimwache alichosema, mimi nitalizungumzia vizuri Jumatatu saa nne asubuhi,” alisema Lukuvi.

 

LOWASSA

MTANZANIA Jumapili lilipowasiliana na Lowassa ili kufahamu mawazo yake kuhusu uamuzi huo ambao umemfika mtu wake wa karibu wa siasa za upinzani, aliyeunganishwa naye na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 baada ya majina yao kukatwa kuwania urais kupitia CCM, alisema kwa kifupi tu kwamba masuala hayo yapo mahakamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles