28.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 21, 2024

Contact us: [email protected]

FAINI YA MAGARI SAWA NA MSHAHARA YAZUA GUMZO

Na AGATHA CHARLES – dar es salaam

FAINI ya Sh 200,000 inayodaiwa kutozwa na Mamlaka ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa mujibu wa sheria imezua gumzo.

Juzi na jana katika mitandao ya kijamii hasa ule wa WhatsApp kumekuwa kukisambaa nakala ya risiti inayoonyesha Kampuni ya Tanzania Petroleum Service Ltd ililipa kwa Tanroads faini ya Sh 200,000 kwa kosa la kutofuata sheria na kuendesha gari kwa mwendo kasi barabarani.

Faini hiyo iliyolipwa Agosti 11, mwaka huu ilionyesha kuwa mhusika alitenda kosa la kushindwa kufuata ukomo wa mwendokasi eneo la Kibaha, Mkoa wa Pwani, ambalo faini yake ni kiasi hicho au jela mwaka mmoja ama vyote kwa pamoja.

Baadhi ya wadau wa vyombo vya usafiri waliweka mchanganuo wa fainio hiyo kwamba askari barabarani ni Sh 30,000, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) Sh 80,000 na Tanroads 90,000.

Ingawa sheria hiyo si mpya, kilichoonekana kushtua na kuzua gumzo ni mchanganuo huo na kiwango kikubwa cha faini.

Baadhi ya watu katika mjadala huo wamefananisha kiwango cha fedha kinachotozwa kama

adhabu kwa kosa hilo sawa na kima cha chini cha mshahara kwa baadhi ya watumishi.

 

Kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa umma ni takribani shilingi 300,000 kwa mwezi, huku baadhi ya sekta binafsi zikilipa chini ya hapo.

Kutokana na dhana hiyo, MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara wa Sumatra, Johansen Kahatano ambaye alisema faini hiyo haiwahusu wao bali ni ya Tanroads.

“Si kweli, Tanroads wana faini zao, ile ni ya Tanroads, sisi hatuna faini za barabarani hivi sasa,” alisema Kahatano.

Kutokana na hilo, MTANZANIA Jumapili liliwasiliana na Tanroads kwa simu kupitia namba ilizozipata katika tovuti yao, ambayo ilipokewa na mtu aliyegoma kujitambulisha wala kuzungumzia chochote kwa madai kuwa si msemaji bali ni mfanyakazi wa kawaida.

Jitihada za kumpata Mkurugenzi Mtendaji wa Tanroads, Injinia Patrick Mfugale hazikuzaa matunda.

Hata hivyo, gazeti moja la kila siku (si MTANZANIA) liliwahi kumkariri mwezi huu, Kaimu Meneja wa Tanroads Mkoa wa Pwani, Mhandisi Zuhura Amani akifafanua kuhusu faini hiyo.

Alisema mkoa huo ulikuwa katika mpango wa kuendesha operesheni ya kudhibiti mwendo kasi na madereva wanaopita magari ya wenzao (over-take) kinyume cha utaratibu ili kupunguza ajali za barabarani na kuwafanya wafuate sheria.

Katika gazeti hilo, Mhandisi Amani alisema hiyo ni utekelezaji wa sheria ya barabarani ya mwaka 2007, namba 13 inayoelekeza watumiaji wa barabara wanaoendesha vyombo vya moto kutii alama zilizowekwa.

Alisisitiza kuwa sheria hiyo inasema faini ya mwendokasi ni Sh 200,000 au kifungo cha mwaka mmoja ama vyote viwili kwa pamoja.

Katika sheria hiyo, Amani alisema wanaomwaga mafuta ama kufanya matengenezo barabarani na kuzuia magari mengine yasiweze kupita, faini kwa sheria ya Tanroads ni Sh milioni moja.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. acheni ufala… sasa ulitaka atozwe faini ambayo hatajisikia uchungu kulipa.Faini inabidi iwe kubwa na iwe fundisho kwamba watu wengine waogope kuvunja sheria

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles