24.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 19, 2024

Contact us: [email protected]

Sumaye ailipua Serikali ya JPM

fredrick-sumaye*Asema inafanya mambo gizani, kidikteta

*Nape ajivua lawama Bunge ‘Live’

NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

WAZIRI Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, ameilipua Serikali ya Rais Dk. John Magufuli akisema kuwa imezuia matangazo ya moja kwa moja ‘Live’ ya Bunge kutokana na woga wa mambo yake kujulikana na wananchi.

Mbali na hilo, alisema utawala unaovinyima uhuru vyombo vya habari na kufanya mambo yake gizani haufai kwakuwa unakiuka Katiba ya nchi ambayo inatoa fursa na haki kwa wananchi kupata taarifa bila vikwazo.

Sumaye aliyasema hayo jana Dar es Salaam kwenye kongamano la maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.

Waziri mkuu huyo wa zamani ambaye alikihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na upinzani kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana, alisema nchi yoyote yenye utawala bora inapenda mambo yake inayofanya kwa ajili ya wananchi yajulikane wazi.

Alisema ukiona Serikali inataka kuficha mambo yake, lazima kuna mambo inayoyafanya ambayo hayafai na isingependa jamii iyafahamu, jambo ambalo ni kinyume na nchi zinazofuata mfumo wa demokrasia.

“Ukiona Serikali yoyote inapambana na vyombo vya habari na kuvinyima uhuru wa kufanya kazi yao ni lazima kuna tatizo.

“Kwa upande wa watawala, hiyo ni tabia ya kidikteta kwa sababu mfumo wa Serikali kama ni wa demokrasia ambao wananchi ndiyo waliopiga kura kuiweka madarakani, hakuna sababu ya kuficha mambo, na kwa faida ya nani?

“Ukiwa kiongozi wa umma na hasa uliyeingia madarakani kwa kura za wananchi, wapo watakaokusema vizuri na wapo ambao hawaridhiki na huduma zako lazima watakusema vibaya, lazima uwasikilize wote ili ufanye marekebisho pale unapokwenda vibaya.

“Kiongozi mwenye tabia za kidikteta hataki kusikia kingine zaidi ya sifa zake tu, huyo ni mtu hatari na katika nchi ya namna hiyo hakuna uhuru wa habari wala uhuru wa kutoa maoni kwa woga wa kupotezwa kusikojulikana,” alisema.

Sumaye aliongeza kuwa hakuna Serikali duniani ambayo watu hawataisema kwa sababu ndiyo inayotekeleza majukumu mbalimbali yahusuyo wananchi.

“Kwa mantiki ileile, Rais wa Tanzania anaweza akasemwa na atasemwa ama kwa kusifiwa au hata kwa kukosolewa kwa lengo jema ili arekebishe kasoro za utawala wake.

“Rais ni binadamu sio malaika kwamba haiwezekani akosee, akikosea akubali kukosolewa kama ilivyokuwa kuanzia Serikali ya Julius Nyerere,” alisema.

 

Bunge ‘Live’

Aidha Sumaye aliponda hatua ya Serikali kuzuia matangazao ya moja kwa moja ya Bunge ‘Live’ kupitia Televisheni ya Taifa (TBC), akisema haiendani na matakwa ya demokrasia na ni uvunjaji wa Katiba ya nchi.

“Hivi Serikali yetu tukufu inaogopa nini wananchi kusikiliza ya Bunge wakati Bunge ndicho chombo kinachofanya kazi kwa niaba ya wananchi?… Tusiwaadhibu wananchi kwa jambo ambalo wao wala wabunge wao hawajafanya kosa,” alisema Sumaye.

Akifafanua zaidi, alisema kuzuiliwa Bunge kwa kisingizio cha gharama, ni uongo kwani kuna vyombo vingine viko tayari kuonyesha bila kujali hiyo gharama, lakini imekuja hoja nyingine kuwa Bunge litaanzisha televisheni yake na vyombo vyote vitajiunga kuchukua matangazo huko.

“TBC ni chombo cha Serikali kinachoendeshwa na kodi zetu. Je, leo unaponunua mitambo mingine kwa kuanzisha televisheni nyingine ya Bunge, hayo ni matumizi mazuri ya fedha za walipa kodi?” alihoji.

Aidha Sumaye aliwataka waandishi wa habari kufuata miiko na maadili ya kazi zao kwa kuandika habari zenye uhakika ambazo hazina madhara, zilizoshiba na zenye kufanyiwa uchunguzi wa kina.

“Ukiandika habari za uongo bila kuthibitisha ni makosa, ukiandika kwa kumwandika mtu kwa makosa kwa lengo la kumchafua au vibaya kwa sababu umehongwa fedha ni vibaya.

“Ukiacha kuandika kwa sababu tu umehongwa fedha nayo ni makosa, ukiacha kuandika kwa sababu umetishiwa nayo ni makosa pia hivyo ni vema mkazingatia maadili,” alisema Sumaye.

 

WADAU WA HABARI

Naye Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Siasa walioandaa kongamano hilo, George Maziku, alisema waandishi wa habari wanafanya kazi katika mazingira magumu ambayo hadi sasa mengi hayajatafutiwa ufumbuzi.

 

KIBANDA

Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2016), Absalom Kibanda alisema kitendo cha wizara kusimamisha kipindi cha Bunge katika televisheni ni kuwanyima uhuru wa habari wananchi kwa sababu  bila ya vyombo vya habari hata Rais Magufuli asingefahamika na kufikia nafasi aliyopo sasa.

Kibanda aliyasema hayo wakati akihojiwa na kituo kimoja cha redio nchini.

Alisema kupitia vyombo vya habari kumewezesha kupatikana viongozi mbalimbali wa chama na Serikali ambao wameleta mapinduzi makubwa ya demokrasia na siasa ndani ya nchi hii.

“Uwepo wa uhuru wa vyombo vya habari utasaidia kuzalisha kina Zitto Kabwe wengi na kina Magufuli, lakini kutokuonekana kwa Bunge moja kwa moja wananchi watashindwa kujenga uaminifu kwa viongozi wao waliowateua,” alisema Kibanda.

 

PROFESA BAREGU

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu, alisema ipo haja ya kufanya mabadiliko ya sheria ya mwaka 1976 ambayo ilitoa madaraka makubwa kwa kiongozi kufungia magazeti au chombo cha habari, na kuendelea kuwapo itazidi kuminya uhuru wa habari.

Alisema zipo sheria nyingine zilizopitishwa mwaka jana kama sheria ya mitandao, takwimu ambazo kuwapo kwake kunaonyesha dhahiri zilipitishwa kwa ajili ya kubana uhuru wa habari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles