23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Damu kusimamisha upasuaji Muhimbili  

Kaimu Balozi wa Marekani nchiniNA HADIA KHAMIS, DAR ES SALAAM

ZAIDI ya watoto 80 wako katika hatari ya kutofanyiwa upasuaji wa moyo kutokana na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kukabiliwa na uhaba mkubwa wa damu katika benki yake.

Hayo yalibainishwa jana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCT), Prof. Mohammed Janab, katika hafla ya kutambulisha madaktari kutoka Marekani waliokuja kwa ajili ya upasuaji huo.

Prof. Janab alisema mtoto mmoja hutumia chupa sita hadi nane za damu wakati wa upasuaji, hivyo kwa idadi ya watoto 80 inahitajika zaidi ya chupa 600 ili kuokoa maisha yao.

Kwa mujibu wa Prof. Janab, kwa sasa akiba ya damu iliyopo katika Benki ya Damu ni chupa 250 tu na upo upungufu wa chupa 350.

“Tunakabiliwa na uhaba mkubwa wa damu katika benki yetu ya damu, kwa kipindi cha wiki moja tumeanza kuwafanyia watoto wenye matatizo ya moyo upasuaji, lakini damu haitoshelezi ni vyema Watanzania wakajitokeza kuchangia damu,” alisema Prof. Janab.

Alisema upasuaji wa moyo unahitaji kuwapo damu nyingi na kuwaomba Watanzania kujitokeza kuchangia ili kuokoa maisha ya watoto hao.

Prof. Janab alisema kufanyika kwa upasuaji huo nchini kumeokoa fedha nyingi kwani watoto hao wangesafirishwa nje ya nchi zingetumika zaidi ya Sh milioni 10 hadi 60 kwa kila mtoto ili kukamilisha upasuaji wake.

“Watoto hawa watafanyiwa upasuaji kupitia msaada wa Taasisi ya Muntada Aid kutoka Marekani, hivyo ni vyema kuwachangia damu ili kuwapa moyo wahisani hao,” alisema.

Prof. Janab alisema kuanzia Januari mwaka huu hadi Machi, taasisi hiyo kwa kushirikiana na jopo la wataalamu kutoka nchi mbalimbali, wameweza kuwafanyia upasuaji wa moyo wagonjwa 90 na hali zao zinaendelea vizuri.

Alisema kwa kipindi cha Aprili mosi hadi kufikia jana, tayari wamewafanyia upasuaji wagonjwa 45 wakiwamo watoto wadogo na watu wazima.

Naye Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Matt Sutheland, alisema hii ni mara ya pili kwa nchi yake kuisaidia Taasisi ya Jakaya Kikwete kwa lengo la kuokoa maisha ya watoto walio na ugonjwa wa moyo.

Balozi Sutheland alisema ni wajibu wa kila mtu kuwasaidia watoto wenye matatizo ya moyo ili waweze kuishi na kusogeza ndoto zao kwani mtoto ndiyo jicho la pili katika nchi.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Jakaya, Dk. Tulizo Sanga, alisema ni vyema wajawazito kuhakikisha wanapata chanjo kamili katika kipindi chote cha ujauzito.

Dk. Sanga alisema wajawazito kutozingatia taratibu za chanjo pamoja na kumeza dawa ovyo bila ushauri wa daktari wakati wa ujauzito, husababisha kujifungua watoto wenye ugonjwa wa moyo.

Utafiti uliofanywa duniani mwaka 2012 hadi 2015 umeonyesha kuwa zaidi ya wagonjwa 400 hadi 600 wanaosafirishwa nje ya nchi kutoka katika nchi za Afrika, asilimia 50 wamekumbwa na tatizo la ugonjwa wa moyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles