22.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, July 23, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi waua majambazi wanne mapangoni

Ernest-ManguNA SUSSAN UHINGA, TANGA

JESHI la Polisi mkoani Tanga limewaua watu wanne wanaodhaniwa kuwa ni majambazi.

Watu hao waliuawa jana katika eneo la mapango ya Amboni wakati wa majibizano ya risasi kati yao na   polisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Leonard Paul, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo alipozungumza na waandishi wa habari.

“Pamoja na kufanikiwa kuwaua watu hao, pia tumefanikiwa kukamata vifaa mbalimbali vinavyosadikika vilikuwa vinatumiwa na wahalifu hao wakati wa kufanya matukio ya ujambazi,” alisema Kamanda Paul.

Alivitaja vitu vilivyokamatwa kuwa ni vocha 195 za mitandao ya simu mbalimbali, majambia saba, mapanga manne, msumeno mmoja, risasi 17 za   shotgun, sare za mgambo, kofia inayofanana na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na pikipiki  mbili.

Aliwataja majambazi waliouawa  kuwa ni Nassibu Bakari, Abuu Mussa, Abuu Kadati na Idrissa Berratu aliyedaiwa kuwa ni raia wa kigeni.

“Kabla ya kupambana na majambazi hao,   tuliwakamata watu wanne waliotaja walipo majambazi wenzao waliokuwa wameweka kambi kwenye mapango ya Amboni.

“Kwa hiyo, tulichokifanya ni kuvamia mapango hayo na tukawaua watu hao wanne na kumjeruhi mmoja baada ya majibizano makali ya risasi.

“Kwa bahati mbaya zaidi,  polisi wawili, walijeruhiwa ambao ni Gwantwa Mwakisole ambaye ni mkaguzi msaidizi na PC Charles.

“Kwa, hiyo namuomba sana Mungu awaponye haraka kwa sababu  baada ya kuanza kupatiwa matibabu, hali zao zinaendelea vizuri,” alisema Kamanda Paul.

Mapango ya Amboni mkoani Tanga yamekuwa ni kimbilio la majambazi na wamekuwa wakiyatumia kama maficho yao  wanapofanya uhlrifu.

Mwaka jana, majambazi hao ambao baadaye walidhaniwa kuwa ni kikundi cha wanamgambo wa Al Shabaab, walitikisa kwa uhalifu mkoani Tanga  na kulazimisha vyombo vya ulinzi kuongeza nguvu   kupambana nao.

Wakati wa kukabiliana na waharifu hao, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) lililazimika kwenda eneo la tukio ili kukabiliana na majambazi hao huku wakiwapo askari wa kikosi cha ardhini cha jeshi hilo.

Wakati wa mapambano hayo yaliyokuwa makali, askari kadhaa wa JWTZ na polisi, walijeruhiwa kwa risasi na majambazi hao.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wananchi waliokuwa wakiishi jirani na mapango hayo, wakiwamo waishio katika Kijiji cha Mleni, walilazimika kuhama makazi yao baada ya kuhofia usalama wa maisha yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles