Na TAUSI SALUM -DODOMA
MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Ncihi Kavu (Sumatra) imetangaza kusimamisha utaoji wa leseni kwa mabasi madogo ya abiria maarufu kama ‘vipanya’ yanayofanya safari zake kwenye wilaya mbalimbali mkoani Dodoma.
Akizunngumza na waandishi wa habari Dodoma jana, Ofisa Mfawidhi wa Sumatra, Mkoa wa Dodoma Konrad Shio, alisema kwa sasa mabasi hayo madogo hayatapatiwa leseni za kufanya safari katika maeneo ya wilayani na badala yake zitaanza kutumia mabasi ya Coaster kwa ajili ya njia hizo.
Alisema lengo la kusimamisha utoaji wa leseni kwa vipanya ni kuboresha usafiri katika maeneo ya wilayani ambako bado kuna changamoto kubwa ya usafiri.
“Hivi vipanya havitaruhusiwa tena kubeba abiria kwa ajili ya kwenda wilayani na badala yake tutatumia mabasi makubwa aina ya Coaster ambayo kimsingi ni makubwa na ni salama kwa ajili safari,” alisema Shio.
Aliyataja maeneo ambayo yalikua yakitumia usafiri wa vipanya kuwa ni Kibaigwa wilayani Kongwa, Gairo mkoani Morogoro na Chamwino.
Alisema pamoja na kusimamisha utoaji wa leseni kwa mabasi hayo madogo pia Sumatra imesimamisha utoaji wa leseni kwa magari ya Noah ambayo yalikuwa yanafanya safari katika maeneo ya Mtera na Mvumi.
“Hivi sasa Noah zilizopo leseni zake zikiisha hazipatiwi tena leseni badala yake tunataka hizi gari ndogo za Hiace ambazo tunaziondoa hapa jijini zipelekwe kule kwa ajili ya safari za maeneo ya Mtera na Mvumi,” alisema Shio.
Amelishauri Jeshi la Polisi mkoani hapa kuhakikisha linakuwa makini zaidi katika kusimamia sheria za usalama barabarani kudhibiti ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikipoteza uhai wa Watanzania.