MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema) maarufu kwa jina la Sugu, amewashangaza wabunge wenzake baada ya kuwanyooshea kidole cha kati akiwa bungeni.
Sugu alifanya hivyo baada ya kuwasilisha taarifa ya kambi yake kuhusu Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Udhibiti wa Matumizi ya Dawa na Mbinu za Kuongeza Nguvu katika Michezo, lililowasilishwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.
“Ni heri ya sisi tunaotoka na kwenda kushinda library, kuliko wabunge wa CCM wanaoshinda kutwa nzima canteen (mgahawa wa Bunge).
“Mheshimiwa Spika naomba taarifa yangu iingie katika kumbukumbu sahihi za Bunge (Hansard), kwani sintaisoma na hii ni kwa sababu haturidhishwi na misimamo ya kidikteta ya Naibu Spika, tutaendelea kutoka,” alisema.
Wakati anaondoka katika ‘podiam’ Sugu alionyesha kidole cha kati, kitendo kilichowachefua baadhi ya wabunge ambapo walisimama na kuomba mwongozo juu ya kitendo hicho.
Mbunge wa Viti Maalumu, Jackline Ngonyani, Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtuth Mapunda, waliomba mwongozo wakitaka uhalali wa Sugu kunyoosha kidole cha kati ambacho ishara yake ni matusi.
Hata hivyo, Naibu Spika alisema hawezi kutolea mwongozo suala hilo hadi atakapojiridhisha kupitia kamera.
MTANZANIA lilipomfuata Sugu ili kujua alikuwa na maana gani kufanya hivyo, alisema alikua akijibu mapigo ya Mapunda anayedai alianza kumchokoza bila kufafanua uchokozi wake.