20.9 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

Nape aitaka Takukuru kumulika chaguzi

Nape NnauyeADAM MKWEPU NA AZIZA MASOUD

WAKATI klabu ya soka ya Yanga ikipeleka barua yenye vielelezo vya hujuma za kuvuruga uchaguzi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, ameitaka Taasisi hiyo kuwa macho kipindi hiki cha chaguzi mbalimbali zinazoendelea ndani ya klabu za michezo, kutokana na kuwapo kwa viongozi wasio waaminifu wanaotumia rushwa kusaka nafasi za kuongoza klabu hizo.

Kauli hiyo ilitolewa na Nape jana bungeni wakati akifunga hoja kupitisha azimio la wabunge la kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Udhibiti wa Matumizi ya Dawa na Mbinu za Kuongeza Nguvu katika Michezo.

Alisema katika vyama vya michezo kumekuwa na utaratibu wa watu kutumia fedha kugombea nafasi mbalimbali ndani ya klabu na kwamba baada ya kupata nafasi hizo wanatafuta njia za kurudisha fedha hizo jambo ambalo halikubaliki.

“Nawaomba Takukuru washughulikie suala hili, nikiwa kama kiongozi napingana vikali na watu wanaotumia njia za fedha kutafuta madaraka ili kuja kuumiza klabu kwa kutafuta kurudisha fedha zao, katika hili niko mstari wa mbele kupingana nalo,” alisema Nape.

Alieleza klabu hizo zinatakiwa kuongozwa na viongozi wanaokubalika kwa mashabiki na si waliotumia fedha kutafuta nafasi hizo, hivyo chini ya uongozi wake atakula nao sahani moja watakaotumia njia hizo.

“Ifike mahali klabu zetu tuziongoze kwa moyo wa upendo na si fedha, hasa kipindi cha chaguzi hizi kunakuwa na hila za hapa na pale lakini nawahakikishia waheshimiwa wabunge tutaleta heshima kubwa katika michezo kuanzia klabu hadi uwanjani,” alisema Nape.

Wakati huo huo klabu ya soka ya Yanga iliwasilisha barua na vielelezo vya hujuma za kuvuruga uchaguzi wa klabu hiyo jana Makao Makuu ya Takukuru.

Yanga ilifikia uamuzi huo baada ya kuwatuhumu baadhi ya wanachama, Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ na Serikali kuhujumu uchaguzi huo usifanyike kama ilivyopangwa.

Akizungumzia uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Jerry Muro, alisema ni mwanzo wa mafanikio ya uchaguzi huo ambao tarehe rasmi itajulikana baada ya mkutano wao wa kesho.

“Tuliahidi tutaleta barua na leo tumefanya hivyo, kwa sasa tutaiachia Takukuru ifanye kazi yake na tutajua nini kinaendelea baada ya kukamilika kazi hiyo.

“Kupitia uamuzi huu wa leo wagombea wanatakiwa kuwa makini kwa jambo lolote linaloashiria rushwa au hujuma zozote ili kukwamisha uchaguzi huu,” alisema Muro.

Naye Msemaji wa Takukuru, Mussa Misalaba, aliahidi kufanya uchunguzi juu ya  malalamiko hayo kwa mujibu wa sheria.

“Malalamiko yote yanayohusu tuhuma za rushwa tumeyapokea na baada ya uchunguzi kwa mujibu wa sheria kila kitu kitafahamika,” alisema Misalaba.

Rais wa TFF, Jamal Malinzi, leo atakutana na Sekretarieti ya klabu ya Yanga kuzungumzia mustakabali wa uchaguzi wa klabu hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles