23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Stewart alia na mabeki, Cecafa

azam fcNA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, amesema safu ya ulinzi ya timu hiyo ilicheza vibaya dhidi ya Simba juzi na kusababisha matokeo ya sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Licha ya sare hiyo, Azam imeendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 26, Yanga ikifuatia kwa pointi 24, Mtibwa Sugar 23 na Simba ikijikusanyia pointi 22 katika nafasi ya nne.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo juzi, Hall alisema tatizo la mabeki lilitokana na yeye kufanya mabadiliko mara mbili ndani ya saa 24 baada ya Aggrey Morris na David Mwantika waliokuwa majeruhi kufeli vipimo juzi asubuhi kabla ya mchezo na kulazimika kuwatumia Said Morad na Erasto Nyoni.

“Nguvu yetu kubwa ipo kwenye safu ya ulinzi, tulivunja rekodi kwenye michuano ya Kombe la Kagame kwa kutwaa ubingwa bila kuruhusu nyavu zetu kuguswa kwa sababu mabeki walikuwa imara.

“Kitu chochote kizuri unachokifanya kinaanzia kwa mabeki, kama wanakaba vizuri basi hata sehemu ya kiungo nayo itamiliki mpira.

“Kama safu ya ulinzi haikabi vizuri na ukashindwa kumiliki mpira basi huwezi kupata kitu, nadhani leo (juzi) safu yetu ya ulinzi ilicheza chini ya kiwango cha Azam, hasa kipindi cha kwanza na hata goli la pili tulilofungwa ilikuwa ni ukabaji mbaya,” alisema.

Kocha huyo raia wa Uingereza alijitetea kuwa mechi ya kwanza kwa timu baada ya mapumziko ya mechi za timu ya Taifa ni ngumu kwa makocha wengi.

“Azam tulikuwa na timu nne tofauti zilizokuwa na wachezaji wetu kwenye michuano ya CECAFA (Kombe

la Chalenji), idadi kubwa kuliko timu nyingine yoyote, wiki hii tulifanya mazoezi kama wageni, wachezaji wengi walikuwa nje ya timu kwa muda wa mwezi mzima,” alisema.

Alisema kila kitu hakikwenda vizuri, kutokana na kila mmoja kujiona mgeni jambo ambalo limechangia kuathiri kiwango chao katika mchezo wa juzi.

Kikosi cha Azam kitashuka tena dimbani Jumapili hii ugenini kuvaana na Majimaji katika Uwanja wa Majimaji, uliopo mjini Songea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles