24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

Stars watua, serikali yatoa tamko

Na Theresia Gasper-Dar es Salaam

KIKOSI cha Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kiliwasili jana kutoka nchini Misri ambako walikuwa wakishiriki Michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon), huku serikali ikitoa tamko kuhusu matokeo waliyopata.

Timu hiyo ilipokelewa na Watanzania mbalimbali  kwenye Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere wakiongozwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt, Harrison Mwakyembe na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda.

Katika michuano hiyo, Taifa Stars ilikuwa  kundi C  na  timu za Kenya ‘Harambee Stars’, Senegal na Algeria na ilishindwa kutamba  baada ya kutolewa hatua ya makundi ikifungwa mechi zote tatu.

Timu hiyo ilianza kufungwa na Senegal mabao 2-0, kisha kufungwa mabao 3-2 na Kenya, kabla ya Algeria kuichapa mabao 3-0.

Akizungumza katika mapokezi hayo, Dkt. Mwakyembe, alisema anaamini baada ya miaka miwili Tanzania itakuwa imepiga hatua kubwa katika michezo, hivyo matokeo hayo yasiwape shida wapenzi wa soka.

“Tumecheza na timu bora ambazo zina wachezaji wakubwa lakini vijana wetu walipambana walionyesha kujituma, hivyo tunatakiwa kuwapa moyo na pongezi kwa walichofanya,”alisema.

Upande wake Makonda amabaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya saidia Taifa Stars, alisema kwa watu wanaofahamu michezo watafahamu kuwa Tanzania ilipofikia ni mwanzo mzuri na  wataendelea kujipanga zaidi.

“Michuano hii imetufundisha mengi, kuna haja ya kukuza vipaji kuanzia ngazi za chini ili baadaye tuweze kupata wachezaji wazuri ambao  wataunda timu bora ya Taifa,” alisema.

Aidha alisema kuna ofisi moja ilichangisha fedha kwa ajili ya Taifa Stars, lakini  fedha hizo hazikufishwa mahali husika na kuwataka wazipeleke  au kuingiza katika akaunti ya Baraza la Michezo la Taifa(BMT) iliyotajwa awali na Waziri Mwakyembe.

Wakati huo huo, Katibu mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidau, alisema baada ya siku mbili watakaa kikao cha viongozi pamoja na benchi la ufundi, kujadili kilichotokea na kuanza maandalizi ya michuano ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan).

Alisema Stars inatarajia kuaza kusaka nafasi ya kufuzu michuano hiyo kwa kukutana na Kenya  Julai 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa , Dar es Salaam.

“Baada ya wachezaji kuwasili wataenda Hoteli ya Serena kupata chakula cha mchana, kisha  kambi itavunjwa rasmi na tutawaita baada ya siku chache kujiandaa na mechi dhidi ya Kenya,” alisema Kidau.

Taifa Stars ilifuzu Afcon ya mwaka huu baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Kundi L kwa pointi zake nane, nyuma ya Uganda walioongoza kwa pointi zao 13 wakizipiku Lesotho iliyomaliza na pointi sita na Cape Verde pointi tano. 

Mara ya kwanza kushiriki Afcon ilikuwa mwaka 1980 na  ilifungwa mechi mbili, 3-1 na Nigeria na 2-1 na Misri kabla ya kutoa sare ya 1-1 na Ivory Coast na kuishia  hatua ya makundi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles