27.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

SPIKA NDUGAI: NITAPELEKA BARUA NEC

Na PATRICIA KIMELEMETA


SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amesema wakati wowote kuanzia sasa ataiandikia barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iweze kuandaa ratiba ya uchaguzi mdogo katika Jimbo la Longido mkoani Arusha.

Uamuzi wa uchaguzi mdogo katika jimbo hilo umekuja baada ya Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali rufaa iliyokatwa na aliyekua mbunge wa jimbo hilo,  Onesmo ole Nangole, kupinga uamuzi wa awali wa mahakama hiyo uliotengua matokeo yaliyompa ushindi mbunge huyo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Spika Ndugai alisema kwa mujibu wa sheria za uchaguzi,  anapaswa kuandika barua hiyo     kuiarifu NEC juu ya kuwapo  nafasi ya kiti cha ubunge katika jimbo hilo baada ya Mahakama ya Rufaa kuwaandikia barua ya kutengua nafasi ya ubunge.

Alisema   barua hiyo itawasilishwa hivi karibuni kwenye ofisi ya tume iweze kuandaa ratiba ya uchaguzi  na kuweka utaratibu wa wagombea watakaoshiriki kwenye uchaguzi huo, jambo ambalo linaweza kuvisaidia vyama vya siasa kuandaa wagombea.

 “Kwa sasa nipo kwenye mchakato wa kuandika barua kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi iweze kuandaa utaratibu wa kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa jimbo la Longido, jambo ambalo linaweza kuwasaidia vyama vya siasa kuandaa wagombea,” alisema Ndugai.

Alisema  kutokana na hali hiyo, uchaguzi mdogo utafanyika  baada ya tume hiyo kumaliza mchakato huo ambao kwa mujibu wa sheria unatarajiwa kufanyika ndani ya siku 90.

Alisema mpaka sasa jimbo hilo halina mwakilishi, hivyo basi kufanyika kwa uchaguzi huo ni muhimu wananchi waweze kupata mwakilishi wao bungeni ambaye ataweza kutetea maslahi ya wapiga kura wake na taifa kwa ujumla.

Juzi, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi, Ramadhan Kailima alisema  anasubiri barua ya utenguzi huo kutoka kwa spika wa bunge iweze kufanya maandalizi ya uchaguzi mdogo wa jimbo hilo.

Alisema kulingana na sheria ta taifa ya uchaguzi kifungu namba 37(3) sura ya 343, endapo mbunge atajiuzulu, kufariki dunia na kutenguliwa na mahakama au kwa sababu nyinginezo, Spika atamuarifu Mwenyekiti wa Tume na kutangaza kwenye gazeti la serikali kwamba kuna nafasi katika kiti cha ubunge.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles