30.8 C
Dar es Salaam
Saturday, January 28, 2023

Contact us: [email protected]

WAFANYAKAZI WA MANJI KORTINI

Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam


SERIKALI imewafikisha mahakamani wafanyakazi wengine wawili wa Kampuni ya Quality Group    kuwaunganisha katika kesi inayowakabili wenzao 14.

Wafanyakazi hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu   Dar es Salaam jana na kusomewa mashtaka yanayowakabili, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha.

Wakili wa Uhamiaji, Method Kagoma aliwataja washtakiwa kuwa ni Meneja Miradi Jose Kiran (40) na Katibu muhtasi, Prakash Batt (35) ambao wote ni  raia wa India.

Kagoma alidai washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka manne.

Inadaiwa Februari 13, mwaka huu, katika ofisi za Kampuni ya Quality Group wilayani Ilala, Dar es Salaam, washtakiwa wote wakiwa raia wa India, walikutwa wakiwa na vibali vya biashara vya kughushi.

Alidai siku hiyo walikutwa wakiishi nchini kinyume cha sheria. Pia wanadaiwa siku hiyo walikutwa wakifanya kazi kama washauri wa Quality Group bila ya kuwa na vibali vinavyowaruhusu kufanya hivyo.

Katika shitaka la nne, washtakiwa hao wanadaiwa wakiwa waajiriwa wa kampuni hiyo, waliwazuia maofisa wa uhamiaji kufanya kazi yao baada ya kukataa kuripoti Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji na kujaribu kutoroka nchini kwa kupitia mpaka wa Horohoro.

Washtakiwa walikana mashtaka hayo na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na kuomba kupangiwa tarehe ya usikilizwaji wa awali.

Hakimu Mkeha aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 7, mwaka huu na washtakiwa waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja atakayetia saini dhamana ya  Sh milioni tano.

Washtakiwa hao waliunganishwa katika kesi inayowakabili Meneja Msaidizi wa kampuni hiyo, Pintu Kumar (28) na wenzake 13, ambao wao walisomewa mashtaka matatu.

Washtakiwa wengine ni washauri wa kampuni hiyo,  Rajat Sarkar (35), Jagadish Mamidu (29), Niladri Maiti (41), Divakar Rajasekaran (37), Rajasekaran (37), Bijenda Kumar (43), Prasoon Kumar (46) , Nipun Bhatt (32) na Mhasibu Mohammad Shaikh (44).

Wengine ni washauri Anuj Agrwal (46), Varun Boloor (34), Arun Kateel (46), Avinash Chandratiwari (33) na Vikram Sankhala (50).

Washitakiwa hao 14 wanakabiliwa na mashtaka matatu yanayofanana na wenzao isipokuwa shtaka moja la kuwazuia maofisa uhamiaji kufanya kazi yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles