NA AZIZA MASOUD,DAR ES SALAAM
SPIKA wa Bunge Job Ndugai amesema suala la kumuita Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Afrika(PAP) Steven Masele katika Kamati ya Maadili lipo katika mamlaka ya kiti chake hivyo hakuwa na sababu ya kujadiliana na wabunge wengine.
Kauli ya Spika Ndugai imekuja wakati juzi kukiwa na malalamiko ya wabunge juu ya mamlaka ya spika kumuita mbunge huyo ambaye uteuzi wake ulishirikisha bunge zima.
Akizungumza na Shirika la Utangazaji la BBC Idhaa ya Kiswahili ambapo mwandishi alimuuliza kama kabla ya kumuita kwenye kikao aliwashirikisha watu waliomteua.
“Suala hilo lipo katika mamlaka ya spika,kumuita mtu ni kumpa haki ya yakusilizwa hivyo watu wanapaswa waelewe vizuri kwa sababu wahusika wanaweza wakachukua hatua za kinidhamu lakini bado wananchi wakawauliza kama tulimisikiliza na ili mtu umsikilize lazima aitwe,kwa hiyo kuitwa ni jambo la kawaida na ni kwa mamlaka ya spika.
“Atafika hapa atakwenda kukutana na wabunge wenziye ambao watamuuliza maswali yatakayokuwapo na yeye atapata haki ya kujielezea ndani ya bunge si nje,kama haki ni ya kwako ivi kwa nini wenzako wakuonee, ”alisema Ndugai.
Alisema hawajakurupuka kumuita mbunge huyo kwakuwa ameitwa kwa mambo ya hapa nyumbani ambayo yanahusisha utovu wa nidhamu na si hayo yanayoendelea katika bunge la Afrika.
“Yeye anaunganisha hilo na matendo ambayo anayafanya ambayo pia yanatudhalilisha kama nchi,lakini hatujamuita kwa mambo ya Afrika Kusini sisi tumemuita kwa mambo ya hapa nyumbani ya utovu mkubwa wa nidhamu,watanzania watulie baada ya muda suala hilo litaletwa bungeni wataelezwa anatuhumiwa nini na majibu yake yalikuwa ni nini kwa sababu lazima liletwe bungeni hilo suala,”alisema Ndugai.
Alisema kiutaratibu mbunge unapopata wito wa kwenda katika kamati ya maadili anapaswa kuupa kipaumbele kwakuwa muhimili wenye nguvu kisheria
“Unapopata wito kwa kawaida wa kwenda kwenye kamati ya maadili ya bunge ambao ni muhimili wenye nguvu kisheria unapaswa kuacha chochote unachokifanya ili uupe wito huo kipaumbele cha hali ya juu.
“Na Masele mpaka hivi sasa hajaitikia wito huo ambao tunahesabu kama ukaidi anapaswa harudi haraka ili aweze kufika kwenye kamati hiyo kwa ajili ya kujibu tuhuma zilizopo dhidi yake,”alisema Ndugai.
Alipoulizwa kwamba anadhani kwa nini amekaidi amri yake Ndugai alijibu kuwa kudhani kwamba mbunge huyo amekaidi amri hiyo si sawa.
“Nikidhania itakuwa sio sawa sawa tumsubiri aje na atajieleza kule kwa nini amekaidi,”alisema Ndugai.
Alipoulizwa kuhusu tetesi ya kwamba serikali ilimwamuru Masele aendelee na kazi zake nchini Afrika Kusini taarifa ambayo inakinzana na amri yake alisema hawezi kuisemea serikali.
“Mimi siisemei serikali kama kweli serikali imemwambia kwamba yeye akaidi wito wa spika basi kwenye kamati ya maadili ataeleza hilo,lakini jambo kama hilo uwezekano wake ni mdogo sana kwa kweli kwa ujumla wake halipo na ni moja ya sababu kwa nini tunamwita ,huyu ni kiongozi ambaye ana mapungufu yakinidhamu anaweza kusema uongo ambao hata mtu mwingine wa kawaida huwezi kufanya ,”alisema Ndugai.
Alipoulizwa endapo mbunge huyo atakaidi wito wake wa kuja Tanzania alisema asingeweza kukaidi zaidi kwa sababu lazima arudi Tanzania.
“Hawezi kukaidi zaidi kwa sababu ni lazima arudi Tanzania labda aamue kuwa mkimbizi na akirudi Tanzania lazima afike kwenye kamati ya maadili huu ni wito wa kisheria kama ilivyo wito mwingine wa mahakamani,tunachomuitia hapa ni tabia yake ya uchonganishi na ugonganishi kwa viongozi.
Alipotakiwa kutoa mfano wa tabia za uchinganishi anazozifanya mbunge huyo Ndugai alisema,“hatuwezi kuingia uko lazima kwanza aende kwenye kamati atakapotoka ndo mtaona fitina yenyewe ikoje ambayo ni kama kukosa sifa kubwa sana kwa kiongozi yeyote yule,”.
Wakati Ndugai akitoa ufafanuzi huo juzi Masele siku aliongea na chombo kimoja cha habari na kudai kuwa hajamuelewa kiongozi huyo hasa kwa hatua yake ya kusitisha uwakilishi wake huku akimtuhumu kwa ukosefu wa nidhamu.