22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 14, 2024

Contact us: [email protected]

Lukuvi aondoa wote ardhi

NA MUNIR SHEMWETA, MVOMERO

Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi William Lukuvi ameagiza kuhamishwa watumishi wote wa sekta ya ardhi katika mkoa mzima wa Morogoro sambamba na kuanzishwa ofisi ya Ardhi Kanda ya Mashariki katika mkoa huo.

Uamuzi huo unafuatia kukithiri kwa migogoro ya ardhi katika mkoa huo licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali katika kutatua migogoro ya ardhi katika mkoa huo.

Lukuvi alitoa maagizo hayo tarehe 17 Mei 2019 alipokuwa alizungumza na wananchi wa Sokoine katika Kata ya Dakawa wilaya ya Mvomero mkoa wa Morogoro wakati wa ziara yake ya kutatua migogoro ya ardhi katika wilaya ya Kilosa na Mvomero.

Lukuvi alisema, baada ya kutembelea wilaya ya Kilosa amebaini watendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa huo wamejisahau na njia pekee ya kufanya ni kuwaondoa  watumishi wote wa sekta hiyo na kuwapeleka maeneo mengine kwa lengo la kupata watendaji wapya.

“Majaribio mengi yamefanyika katika mkoa wa Morogoro kama vile kupanga na kupima kila kipande cha ardhi, utoaji hati za kimila pamoja na uamuzi wa Rais John Pombe Magufuli  kufuta mashamba makubwa yasiyoendelezwa lakini mambo katika sekta ya ardhi kwenye mkoa huo hayaendi”  alisema Lukuvi

Aidha, Waziri Lukuvi alisema, kutokana na mkoa wa Morogoro kuendelea kuwa na migogoro ya ardhi kwa muda mrefu ameamua kuirejesha kanda ya Mashariki ambayo sasa itakuwa kanda maalum ya ardhi kwa mkoa huo itakayokuwa na  wataalamu wote wa sekta ya ardhi  akiwemo Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Kanda,  Wapima, Wathamini pamoja na Wataalamu wa Mipango Miji.

Kwa mujibu wa Lukuvi,  kwa sasa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ina kanda nane  za ardhi nchini na kuanzishwa kanda hiyo kutawafanya wananchi wa mkoa huo kutokuwa  na sababu ya kuhangaika mpaka Dodoma kushughulikia masuala ya ardhi.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, kuanzishwa kwa kanda maalum Morogoro kutaufanya mkoa huo kuwa mkoa pekee Tanzania wenye kanda ya ardhi na kubainisha kuwa ofisi hiyo  itatakiwa kuanza kazi mapema mwezi Julai 2019.

Aidha, Lukuvi ambaye katika ziara hiyo aliambatana na Kamishna wa Ardhi nchini Mary Makondo, Kaimu Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Samwel Katambi, Mthamini Mkuu wa serikali Evalyne Mugasha na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Kati Ezekiel Kitlya alisema, pamoja na uamuzi huo, ameamua kupeleka timu ya wataalamu 15 kutoka Wizarani kufanya uhakiki wa mashamba yaliyofutwa katika wilaya za Kilosa na Mvomero kwa lengo la kupima na kupanga upya mashamba ili kugawa upya mashamba hayo kwa wananchi wanaostahili na mengine kutolewa kwa  Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Vile vile, Waziri Lukuvi amepiga marufuku wamiliki wa mashamba yaliyofutwa na Raisi kurejeshewa kinyemela mashamba hayo kwa kisingizio  cha kuyaendeleza na kusisitiza kuwa iwapo wamiliki wa awali wanayataka mashamba hayo itabidi waombe upya na kama watapatiwa mashamba basi watapewa kulingana na uwezo wao.

Awali Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili katika halmashauri ya wilaya ya Mvomero Rugembe Maiga alimueleza Waziri Lukuvi kuwa migogoro mikubwa ya ardhi katika wilaya ya Mvomero iko katika mipaka ya vijiji  na mashamba na kubainisha kuwa wilaya hiyo ina jumla ya mashamba 12 yaliyofutwa na Raisi. Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mvomero Yusufu Athuman alisema wilaya hiyo inazo changamoto kubwa katika masuala ya ardhi kwa kuwa wanachi wa wilaya hiyo wana uhitaji mkubwa wa ardhi na sehemu kubwa ya ardhi katika wilaya hiyo iko kwa watu wachache

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles