Na MWANDISHI WETU
SPIKA Mstaafu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho ameisifu serikali kwa juhudi zake za kupambana na dawa za kulevya na vitendo vya rushwa vilivyokuwa vikishamiri nchini.
Hayo aliyasema mwishoni mwa wiki kwenye mahafali ya nne ya Chuo Kikuu cha Bagamoyo yaliyofanyika Kawe Beach Dar es Salaam huku akishuhudia utolewaji wa Shahada ya kwanza ya Udaktari wa Falsafa (PhD).
Alisema ni jambo ambalo linatakiwa kuungwa mkono na kila mmoja Tanzania ibakie kuwa nchi safi bila dawa za kulevya.
Alisema kitendo cha kuendelea kutoa huduma ya elimu katika mazingira magumu, tena kwenye majengo ya kupanga, inaonyesha dhamira ya dhati kuhusu namna ya kuendeleza na kukuza elimu nchini.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Costa Mahalu alisema wahitimu 499 wamefanikiwa kumaliza masomo yao kwenye fani mbalimbali, wanafunzi 45 ngazi ya cheti na Stashahada 47.
Wengine ni shahada 334, Shahada ya Uzamili 71 na Shahada ya Udamivu ni mmoja licha ya uongozi wa chuo hicho kukabiliana na changamoto nyingi ndani ya miaka mitano.
Alisema anashukuru kwa kupata kibali cha kufikia hatua hiyo ya kufanya mahafali, lakini bado kuna changamoto ya majengo kwa kuwa bado wapo kwenye majengo ya kupanga.
Alisema iwapo serikali itabariki upo uhakika wa mahafali ya mwakani kufanyika kwenye majengo ya chuo yanayojengwa Kiromo wilayani Bagamoyo.
Alisema chuo kimekuwa na malengo ya kuwasomesha wahitimu wa chuo kwa kuwapeleka vyuo vingine katika shahada ya uzamivu kupunguza tatizo la wahadhiri ambalo vyuo vingi nchini vinakabiliana nalo.
Awali, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Dk.William Kudoja alisema wanaendelea na utaratibu wa kuongeza kozi baada ya kukamilisha ujenzi wa majengo ya chuo Bagamoyo.
Waliwaomba wadau ikiwamo serikali, kuhakikisha wanasaidia kukamilisha majengo yao wenyewe na kuepuka gharama kwenye majengo ya kupanga.