33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Sitta: Nipeni miaka mitano

Mheshimiwa Samweli Sitta akiwa na viongozi wenzake wa CCM alipokuwa akitangaza nia ya Kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.NA WAANDISHI WETU, TABORA
IDADI ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaotangaza nia ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, imeendelea kuongezeka baada ya Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta naye kutangaza jana.
Waziri Sitta, alitangaza nia yake katika Ikulu ndogo ya Itetemea mkoani Tabora, huku akiomba chama chake kimpitishe na Watanzania kumpa miaka mitano tu ya kufanya mageuzi makubwa ya kiutawala.
“Tofauti na wenzangu wanaotaka urais kwa miaka 10, mimi nataka kutumikia nafasi hii kwa miaka mitano tu itakayoniwezesha kutatua changamoto zilizopo,” alisema.
Alitaja sababu tano zilizomsukuma kuwania nafasi hiyo, ambazo ni mifarakano ya Muungano, mchakato wa Katiba Mpya, mfumo wenye motisha kwa wote ili kuchochea uchumi endelevu na wa viwanda, mikakati ya kupambana na rushwa na kuimarisha uchumi wa CCM.
Sitta aliyejigamba kuwa na uzoefu mkubwa ndani ya CCM kwa kuwa mbunge miaka 30, alisema katika muda huo amejifunza mambo mengi katika uongozi wa kisiasa, hivyo hafikirii kushindwa katika kinyang’anyiro hicho.
“Kugombea nafasi ya urais wa nchi yetu, si jambo jepesi linahitaji tafakuri ya kina ukizingatia nafasi hii inabeba matumaini ya Watanzania wote milioni 45,” alisema.
Sitta aliyesimikwa kuwa mkuu wa wajukuu wa Chifu Abdallah Fundikira, alisema akichaguliwa kuwania urais na kukiongoza chama chake, atatumia uzoefu wa miaka tisa na miezi sita akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kuziunganisha shughuli za uchumi za chama na wawekezaji makini ili kupunguza utegemezi.
“Chama ili kiwe madhubuti ni wajibu wa mwenyekiti kuhakikisha vitengo na vitega uchumi vinakuwa na tija inayokiwezesha kuendesha shughuli zake kwa kujitegemea… chama tawala kilicho imara kiuchumi kitakuwa na watendaji wanaofanya kazi zao kwa kujiamini na kuisimamia Serikali ili itimize wajibu wake kwa wananchi.
“Kitakuwa na ufanisi zaidi kuendesha shughuli zake, bila kujidhalilisha kwa kuomba misaada kutoka kwa matajiri,” alisema.

MUUNGANO
Kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Sitta alisema ameona nyufa kutokana na kila pande kutoa kauli na vitendo vinavyoashiria utengano.
“Tunashuhudia wanasiasa wanatuhumu Zanzibar kuwa itanufaika kama ikijitenga na kuwa nchi bila ya kuwa sehemu ya Muungano… baadhi ya wabara wanasema watu wa Zanzibar ni wakorofi wasioridhika na kinachofanywa na Muungano na wanahisi mfumo uliopo unaipendelea… kiongozi anayeweza kutatua hili lazima awe na uelewa wa kutosha wa asili,” alisema.
Alisema ushiriki wake tangu awamu ya kwanza ya utawala wa taifa hili chini ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, unamuweka katika nafasi nzuri ya kuongoza mchakato utakaowezesha kuzijadili na kuzipatia ufumbuzi changamoto za Muungano.

MCHAKATO WA KATIBA
Kuhusu mchakato wa Katiba, alisema pamoja na kutokuwa na mwafaka kamili wa kutopatikana, Katiba Inayopendekezwa ina maeneo mengi ya msingi.
“Binafsi naamini pande zinazosigana kuhusu Katiba Inayopendekezwa zina wazalendo ambao wanaweza kukubaliana kuwa na kipindi cha mpito cha utulivu na maelewano kitakachotuwezesha kama taifa kusonga mbele,” alisema.
Alitoa ushauri kwa viongozi wa kisiasa na jamii, washawishike kukubali kutokuwa na mshindi wala mshindwa.

MOTISHA KWA WOTE
Sitta alisema atahakikisha anakuza uchumi kwa kasi na kupunguza umasikini unaowakabili Watanzania.
Alisema ili kukabiliana na tatizo hilo, bajeti ya Serikali itajengewa uwezo wa kutosheleza tena wenye ubora zaidi ili huduma za jamii kama vile afya, elimu na maji viweze kupatikana kirahisi.
Sitta alisema kuna kila sababu kuubadili mfumo wa uendeshaji nchi uwe ni wa motisha kwa wazalisha mali.
“Mifumo ya nchi zilizopiga hatua kubwa za maendeleo duniani ni ile iliyoweka mazingira chanya ya kuaminiana baina ya Serikali na sekta binafsi, hapa kwetu halijatimia.
“Watendaji serikalini wanawatazama wafanyabiashara, hawa hawana uzalendo na ni wakwepa kodi, wamejenga mazoea ya kutoa rushwa,” alisema.

RUSHWA
Alisema rushwa kubwa zimekuwa na athari kubwa kwa uchumi wa nchi, kutokana na mikataba mibovu ya huduma na mauzo, manunuzi hewa, manunuzi yaliyojaa unyonyaji, uteuzi wa wazabuni na upatikanaji wa ajira, vimesababisha hasara ya mabilioni ya fedha.
“Nitahakikisha hatuna budi kutunga sheria itakayotenganisha biashara na uongozi ili mtu achague kimoja kati ya biashara au uongozi wa siasa.
“Kama mfanyabiashara atataka kuingia katika uongozi wa siasa, itabidi akabidhi mali na biashara zake kwa mdhamini atakayeendesha biashara hizo wakati mhusika anatumikia umma,” alisema.
Alisema atahakikisha miiko ya uongozi inarejeshwa na kutungiwa sheria ili kudhibiti ufisadi, hatua ya pili itakuwa kutunga sheria mpya zilizo kali na ambazo zitakuwa na matokeo ya kumzuia mtu asitamani kusaka rushwa.
Sitta alisema mali za viongozi zitamkwe kwa uwazi, mali isiyolingana na kipato na kukosa maelezo ya kutosheleza itaifishwe, kesi za rushwa ziwe na utaratibu wenye uwazi, tume inayoshughulikia maadili ya viongozi ipewe nguvu kubwa za uchunguzi ambayo itafuatilia mali za viongozi bila kuzuiliwa na mamlaka yoyote.
Alisema tume hiyo itafanya kazi zake kwa kuweka mambo wazi kuhusu watuhumiwa, tuhuma zao, majibu yao na hatua zinazofuata.
Sitta alisema adhabu ya utoaji na upokeaji rushwa lazima iwe kali na iambatane na mali zilizothibitika kupatikana kwa rushwa kutaifishwa.

UZOEFU WAKE
Historia inaonyesha kuwa Sitta amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwamo Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) mwaka 1987, Katibu wa CCM Mkoa Iringa na Kilimanjaro.
Pia alikuwa Spika wa Bunge la Tisa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM mwaka 2005-2010.

Habari hii imeandaliwa na Shabani Matutu, Odace Rwimo na Thomas Murugwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles