30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Sintofahamu ya Ukuta

lowasaaaaa

Patricia Kimelemeta na Nora Damian,

VIONGOZI wa Serikali, dini na vyama vitano vya siasa vyenye uwakilishi bungeni, jana wamekutana kwa zaidi ya saa 10 kujadili mambo mbalimbali yakiwamo Operesheni Ukuta na wabunge wa upinzani kususia vikao vya Bunge.

Kikao hicho cha siri kilifanyika Dar es Salaam jana kikiongozwa na viongozi wa Baraza la Kikristo Tanzania (CCT), chini ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili na Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo na wale wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini chini ya Mwenyekiti wake, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum.

Katika kikao hicho kilichoanza saa tatu asubuhi, Serikali iliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, huku CCM ikiwakilishwa na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana na msemaji wa chama hicho, Christopher ole Sendeka ambao walifika saa 11 jioni.
Chadema iliwakilishwa na Makamu Mwenyekiti, Said Issa Mohamed na Naibu Katibu Mkuu, John Mnyika, NCCR-Mageuzi iliwakilishwa na Mwenyekiti James Mbatia, ACT-Wazalendo Mwenyekiti Anna Mghwira na CUF iliwakilishwa na Riziki Mngwai na Mbalala Maharagande.
Kikao hicho kilifanyika chini ya ulinzi mkali uliosababisha waandishi wa habari kutoruhusiwa kuingia ndani kwa madai kuwa kilikuwa cha faragha.

Kutokana na hali hiyo, waandishi hao walifukuzwa kwenye eneo hilo na kwenda kukaa nje kwa ajili ya kupiga kambi ili waweze kujua kitakachojiri ndani ya kikao hicho.

Ilipofika saa 10:45 jioni, Mnyika alitoka na kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu kilichojadiliwa ndani ya kikao hicho.

Alisema kuwa kikao hicho ni cha siri, lakini pamoja na mambo mengine walijadili ajenda ya wabunge wa upinzani kususia vikao vya Bunge, Rais John Magufuli kutumia madaraka yake vibaya kwa kupiga marufuku mikutano ya vyama vya siasa hadi mwaka 2020 na kupiga marufuku urushwaji wa moja kwa moja wa mijadala ya Bunge kupitia Televisheni ya Taifa (TBC).
Mnyika aliwaambia waandishi kuwa maazimio yaliyofikiwa ndani ya kikao hicho yatatolewa na viongozi wa dini ambao ndio waliokiitisha.

Alisema katika kikao hicho, aliwaambia viongozi hao kuwa wabunge wa upinzani walisusia vikao na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson kutokana na kutumia nafasi ya kiti vibaya kwa kuwadhibiti bungeni.

“Kutokana na hali hiyo, niliwaambia viongozi hao kukaa na Rais Magufuli na kumshauri kutokana na malalamiko yetu ili yaweze kufanyiwa kazi ili kunusuru mgogoro wa kisiasa uliojitokeza nchini,” alisema.

Alisema hoja hizo pamoja na nyingine ndizo zilizozaa maandamano na mikutano bila kikomo nchi nzima chini ya Operesheni Ukuta.

Mnyika alisema chama chao kimewaomba viongozi wa dini kukaa na Rais Magufuli ili kumweleza malalamiko yao na kuangalia namna ya kuyashughulikia ili kuepuka Operehseni Ukuta ambayo imepangwa kufanyika Septemba mosi.

Alisema pia, Waziri Nchemba ana mamlaka ya kisheria ya kutengua kauli ya Rais Magufuli ya kuzuia mikutano hiyo kutokana na mamlaka aliyonayo.

“Nilimwambia Mwigulu, wewe ni Waziri wa Mambo ya Ndani, una mamlaka ya kisheria ya kuruhusu kuendelea kwa shughuli za kisiasa nchini kwa sababu wewe ni waziri mwenye dhamana, usiogope madaraka yako, unapaswa kumshauri rais katika hili.

“Mwigulu alijibu kuwa suala la kuzuia mikutano ya wanasiasa ni la muda ili kuangalia usalama wa nchi, lakini itafika kipindi watawaruhusu kufanya hivyo, japo sijaridhika na majibu hayo,” alisema Mnyika.

Aliongeza kuwa Mwigulu alisema Serikali imepanga kulijibu suala hilo kwa undani katika kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa kilichoitishwa na Msajili, Jaji Francis Mutungi Agosti 29 na 30.

Katibu Mkuu wa CCM, Kinana na Msemaji wa chama hicho, Ole Sendeka walitoka kikaoni saa 1:35 usiku, lakini hata hivyo hawakuwa tayari kuzungumza na waandishi wa habari.

VIONGOZI WA DINI

Mwenyekiti Mwenza wa kikao hicho, Askofu Alinikisa Cheyo wa Kanisa la Moravian, alisema suala kubwa ambalo walijadiliana ni juu ya mahusiano ya wanasiasa.

“Tunahitaji amani katika nchi na hilo ndilo lilikuwa suala kubwa tulilojadili,” alisema Askofu Cheyo.

Naye Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema: “Tumejadili pia mwenendo wa Bunge letu na wabunge wa upinzani waliosusia vikao… mazungumzo bado yanaendelea.”

Taarifa za ndani ya kikao hicho zilieleza kuwa viongozi hao watakutana tena kwa ajili ya kutoa maazimio yao.

LOWASSA

Katika hatua nyingine, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, amezidi kuwasisitiza Watanzania wajitokeze kwa wingi kushiriki maandamano yaliyoandaliwa na chama hicho Septemba mosi.

Akizungumza wilayani Kilolo, Iringa jana, Lowassa aliwataka wananchi wasifanye vurugu wala kuharibu mali wakati wote watakaokuwa kwenye maandamano hayo.

“Tujitokeze kwa wingi Septemba mosi, mwaka huu, tuandamane bila kuharibu mali ya mtu kama tulivyofanya wakati wa kuchukua fomu pale Buguruni, tukaelekea Tume ya Taifa ya Uchaguzi hadi Kinondoni bila hofu.

“Tuandamane kwa sababu tuna chama imara kinachotetea uhuru, haki ya mwananchi, maendeleo na ustawi wa nchi na kinawapenda sana.

“Hata mimi nina hofu kama tusipotekeleza hili, nchi itakuwa wapi hapo baadae. Haiwezekani mtu mmoja ajiamulie tu kila jambo na kuvunja Katiba.
“Kuna wasuluhishi wanasema tuzungumze, tunakubali kuzungumza, lakini tuzungumze nini ikiwa mtu anavunja Katiba na hawamuonyi na hawamshauri? Hii si sawa kabisa.

“Yaani mtu mmoja anajiamulia kuvunja Katiba, anazuia mikutano, anazuia mikutano ya ndani na wasuluhishi hawamuonyi, nasema kabla ya kuja kwetu, wakamweleze yeye kwanza juu ya matendo yake,” alisema Lowassa.

Alisema hivi sasa Jeshi la Polisi linawaandama wafanyabiashara ili wasitoe kumbi za mikutano kwa ajili yake.

AMRI YA POLISI 

Wakati hayo yakijiri, Jeshi la Polisi limepiga marufuku mikutano ya ndani ya vyama vya siasa kwa madai kuwa wanatekeleza amri ya Rais Magufuli.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Mssanzya, alisema awali walikataza mikutano yote ya hadhara ya kisiasa kutokana na amri ya Rais Magufuli aliyesema isifanyike hadi mwaka 2020 huku mikutano ya ndani ikiendelea kufanyika.

HABARI HII IMEANDALIWA NA PATRICIA KIMELEMETA,NORA DAMIAN, ESTHER MBUSSI, HERIETH FAUSTINE, FERDINANDA MBAMILA

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles