30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kipilimba bosi mpya Usalama wa Taifa

Rais Dk. John Magufuli (kushoto), akimwapisha Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya wa Usalama wa Taifa, Dk. Modestus Kipilimba, Ikulu Dar es Salaam jana.
Rais Dk. John Magufuli (kushoto), akimwapisha Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya wa Usalama wa Taifa, Dk. Modestus Kipilimba, Ikulu Dar es Salaam jana.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli, amemteua Dk. Modestus Kipilimba, kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, akichukua nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Rashid Othman, aliyestaafu kwa mujibu wa sheria.

Kabla ya uteuzi huo, Dk. Kipilimba alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), iliyokuwa wazi baada ya aliyekuwa mkurugenzi wake, Dickson Maimu, kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ilieleza kuwa, Dk. Kipilimba aliapishwa jana mchana Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli pia amemteua, Robert Msalika (Makungu) kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa.

Kabla ya uteuzi huo Msalika alikuwa Ofisa Ubalozi katika Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia, huku aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, George Madafa akiteuliwa kuwa balozi ingawa bado hajapangiwa nchi atakayokwenda kuwakilisha.

Kutokana na uteuzi huo, imeelezwa kwamba wakurugenzi na naibu wakurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa waliopo wanaendelea na nafasi zao.

Kipilimba ni nani

Februari 15, mwaka huu Rais Dk. John Magufuli, alimteua Kipilimba kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Kabla ya uteuzi huo, Dk. Kipilimba alikuwa Mkurugenzi wa Menejimenti ya Udhibiti (Director of Risk Management) wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kabla ya kupelekwa NIDA, Kipilimba alikuwa Mkurugenzi wa Daftari na Tehama wa Tume yaTaifa ya Uchaguzi (NEC).

Wadau wampongeza

Mmoja wa wanasiasa ambaye pia alikuwa ni ofisa wa ngazi za juu wa Idara ya Usalama wa Taifa, alisema amefurahishwa na uteuzi wa Kipilimba katika nafasi hiyo nyeti kwani kazi hiyo anaijua.

“Nimempongeza Modestus Kipilimba kuwa DGIS wa TISS. Nimefurahi sana kwa sababu amesoma na anaijua sana kazi hiyo. Enzi za miaka ya 60, 70 na 80 idara nyingi za usalama duniani zilijikita na kazi ya kutafuta habari! Enzi hizo zikapitwa na wakati.

“…enzi za miaka ya 90 hadi 2000 zikajikita zaidi na uchambuzi wa habari. Kuanzia miaka 2001 hadi sasa idara nyingi zinachambua habari zikisaidiwa na ICT na emphasis ipo  kwenye inteligensia ya kiuchumi na ugaidi zinahitaji viongozi kwenye utaalamu huo,  Modestus amesomea yote hayo tumpatie ushirikiano……,” alisema kiongozi huyo ambaye jina lake linahifadhiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles