Na WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
ASKARI wanne wa Jeshi la Polisi wameuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi baada ya kuwavamia wakati wakitekeleza majukumu yao.
Katika tukio hilo lililotokea Benki ya CRDB iliyopo Mbande, Mtaa wa Magengeni, Kata ya Chamazi wilayani Temeke, Dar es Salaam juzi, pia raia wawili wamejeruhiwa.
Kwa mujibu wa mashuhuda, majambazi hayo yalianza kuwashambulia kwa risasi askari walipokuwa wakikabidhiana lindo majira ya saa 1 usiku.
ASKARI WALIVYOVAMIWA
Akizungumza na MTANZANIA katika eneo la tukio jana, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Magengeni, Sadick Makanwa, alisema hakuna mtu aliyewatambua majambazi hao wakati wanafika eneo hilo kwani walikuwa wamevalia mavazi ya kawaida.
Alisema kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, askari walifika wakiwa na gari lao aina ya Noah lenye namba PT 3889 na kuliegesha mbele ya jengo la Benki ya CRDB.
“Ilikuwa majira ya saa 1:15 hivi, askari walikuja na gari yao na kuigesha mbele ya benki. Kama ilivyo kawaida yao huwa wanabadilishana lindo inapofika jioni.
“Askari mmoja alifungua mlango na aliposhuka toka kwenye gari, ghafla wakaanza kushambuliwa kwa risasi ambazo hakuna aliyejua zinatokea upande gani.
“Yule askari alianguka na dereva naye alishambuliwa akiwa ndani ya gari na kupoteza uhai palepale,” alisema Makanwa na kuongeza:
“Wakati huo kulikuwa na askari mwingine alikuwa anatoka ndani ya benki kwenda kuwapokea wenzake, alipoona mwenzake ameanguka, alianza kukimbia. Lakini ghafla naye alipigwa risasi ya kichwani akaanguka.”
Alisema askari mwingine aliyekuwa ndani ya benki alitoka na alipoona wenzake wapo chini, aliamua kukimbia na kutumia upenyo uliokuwa baina ya kibanda cha walinzi na ukuta wa jengo la benki, na kwenda kujificha kwenye nyumba ya udongo iliyokuwa mbali na eneo la tukio.
Makanwa alisema watu hao walikimbia kuelekea upande wa kulia karibu na kituo Kidogo cha Polisi ambapo walikuwa wameegesha pikipiki zao.
WALIVYOTUMIA PIKIPIKI
Alisema kwa mujibu wa mashuhuda, pikipiki hizo zilikuwa tatu na hazikuwa na namba za usajili.
“Walipakizana watatu watatu kwenye pikipiki mbili na wawili wakapanda kwenye pikipiki moja.
“Waliweka silaha zao kwenye kiroba na kuelekea upande wa kulia wa benki hadi karibu na kituo kidogo cha polisi ambako walikuwa wameegesha pikipiki zao,” alisema.
Alisema walitumia mbinu ya kujifanya wao ni raia wa kawaida wakisikika wakisema ‘wamekimbilia huku’, ili wasitambulike kama ndio waliofanya unyama wa kuua askari.
“Baada ya kupanda pikipiki, majambazi wawili waliokuwa na bastola walikaa nyuma ya pikipiki na walikimbia kuelekea Barabara ya Serengeti,” alisema Makanwa na kuongeza kuwa tukio hilo lilidumu kwa dakika saba hadi 10.
Makanwa alisema baada ya kufanya unyama huo, majambazi hao waliiba silaha na hawakuingia ndani ya benki kuchukua fedha.
“Hili tukio kwa namna lilivyotokea, inaonekana hawa watu walikuja muda mrefu na kujificha wakisubiri askari wafike ndipo wawavamie na kuwapora silaha, hawakuwa na nia ya kuiba fedha” alisema.
Shuhuda mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Abdallah, alisema wakati tukio hilo linatokea, alikuwa ndani ya mgahawa wake uliopo jirani na benki hiyo.
“Nilisikia mlio wa risasi, sikushtuka, nilifikiri ni askari ‘wameshtua’ kwa sababu huwa siku moja moja wanafyatua risasi. Lakini ghafla nilisikia kishindo ukutani karibu na dirisha, nikagundua ni risasi.
“Nililala chini, risasi ziliendelea kufyatuliwa kwa dakika kama tano kisha zikatulia. Nilianza kutambaa kuelekea chumbani, mara zilianza tena kufyatuliwa kwa dakika nyingine kama tano,” alisema Abdallah.
Shuhuda mwingine ambaye ni mmoja wa majeruhi, Aziz Yahaya, alieleza kuwa tukio hilo lilitokea akiwa kazini kwake, mita chache kutoka ilipo benki hiyo.
“Nilikuwa katika shughuli zangu za kila siku za kuuza mgahawa. Walikuja wateja wawili mtu na mke wake wakiwa na mtoto, wakaagiza chipsi mayai. Baada ya muda kidogo nikiwa nawandalia, nikasikia mlio wa risasi.
“Sikutilia maanani kwa sababu nilifikiri ni polisi wameamua kufyatua kama ilivyo kawaida yao kwani huwa wanajaribu silaha zao,” alisema Yahaya.
Alisema alipata wasiwasi baada ya kusikia milio ya risasi ikiendelea kurindima.
“Niliona si kawaida, ikabidi nianze kukimbia kuingia ndani huku nikiyumbayumba kujaribu kukwepa risasi, lakini kumbe nilikuwa nimeshapigwa risasi pasipo kujua.
“Nilipofika ndani ndipo niligundua nimepigwa risasi kwenye mkono wangu wa kushoto baada ya kuona damu zikichuruzika,” alisema akionyesha mkono wake ambao ulikuwa umefungwa bandeji.
Alisema alikaa ndani hadi hali ilipotulia ndipo akatoka na kukuta miili ya askari wawili wakiwa wamelala chini, mmoja ukiwa nje ya mgahawa wake.
KAULI YA POLISI
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Mssanzya, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa majambazi hao walikuwa na lengo la kupambana na askari na si kupora mali yoyote katika benki hiyo.
Alisema majambazi waliwavamia askari hao na kupora silaha mbili za SMG na risasi 60, huku wakijeruhi raia wengine wawili.
Aliwataja askari waliouawa katika tukio hilo ni E.5761CPL Yahaya, F.4660 CPL Hatibu, G.9524 PC Tito na G.9996 PC Gastone na raia waliojeruhiwa ni Ally Chiponda na Azizi Yahaya ambao wote ni wakazi wa Mbande.
Aidha Kamishna Mssanzya alionya hatua ya baadhi ya watu waliokuwa wakikejeli kuuawa kwa askari hao kupitia mitandao ya kijamii.
Ofisa Uhusiano wa Manispaa ya Temeke, Joyce Msumba, alithibitisha kupokewa kwa majeruhi mmoja, Ally Said (36) ambaye amejeruhiwa miguu yake yote miwili kwa risasi ambazo bado zilipo mwilini akisubiri kufanyiwa upasuaji.
Alisema kwa mujibu wa majeruhi huyo, alipigwa risasi wakati akienda kushuhudia tukio hilo.
Alisema pia walipokea mwili wa askari mmoja, Tito Mapunda ambaye alifariki dunia wakati akikimbizwa hospitalini.
NCHEMBA ALAANI
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, alilaani tukio hilo kupitia vyombo vya habari akiwataka majambazi hao wajisalimishe.
“Ninalaani kitendo hiki cha kuvamia askari na kuwauwa kisha kupora silaha. Nawataka watu waliofanya hivyo wajisalimishe wenyewe kabla hatujaanza msako mkali dhidi yao,” alisema.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwapo matukio kadhaa ya kuuawa kwa askari polisi.
Aprili 1, mwaka jana, askari wawili waliuawa na kuporwa bunduki aina ya SMG wilayani Mkuranga mkoani Pwani.
UJENZI WA KITUO
Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva, alifika katika eneo la tukio hilo jana akiwa na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na kufanya kikao cha dharura na wananchi wa eneo hilo, kisha kuendesha harambee kwa ajili ya ujenzi wa kituo kikubwa cha polisi.
“Baada ya wananchi kulalamika kuwa eneo hili halina ulinzi wa kutosha, tumefanya harambee na wananchi wamechangia matofali 4,500, mifuko 60 ya saruji na Mkurugenzi wa Halmashauri amechangia mabati kwa ajili ya ujenzi,” alisema Lyaniva.
Habari hii imeandaliwa na Jonas Mushi, Yassin Issah na Herieth Faustine