24.9 C
Dar es Salaam
Sunday, April 21, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA, YANGA KAISHANGAENI MANCHESTER CITY

NA AYOUB HINJO

IMEKUWA kama wimbo ambao umezoeleka masikioni kila siku, ina maana kwamba itafika mahali utauchoka wimbo huo na kutaka mwingine tena ambao utakupa ladha mpya masikioni.

Imekuwa kama kelele masikioni mwa mashabiki wa soka hapa nchini kuhusu klabu za Simba na Yanga kumiliki  viwanja vyao. Inaonekana kama imezoeleka sasa, kila mmoja anaona jambo la kawaida, sababu aina ya timu zenyewe zimeshindwa kujipambanua ili kwenda na wakati.

Niliwahi kuambiwa kuwa hata viongozi wanaopiga kampeni na kuomba kura kwa wanachama wa klabu hizo ili kupata madaraka, wanatumia sera ya kujenga uwanja kama silaha muhimu ya kujipatia kura.

Ni miaka mingapi imepita tangu viongozi wa klabu hizo zenye umri wa zaidi ya miaka 70 waanze kuahidi watajenga viwanja.

Hakuna kingine ambacho viongozi wanaweza kudanganya zaidi ya viwanja, hiki ndicho unachoweza kusema na mara nyingi wamekuwa na hoja nyepesi sana, lakini hii yote inatokea sababu mpira wa nchi hii kwa ujumla unasimamiwa na watu wasiojua lolote kuhusu mpira wa miguu.

Hivi karibuni Bodi ya Ligi ilitangaza ratiba ya michezo itakayopigwa Jumamosi na Jumapili kutokana na mabadiliko kadhaa ya viwanja na michezo mingine kusogezwa mbele.

Timu za Simba na Yanga kwa pamoja zimepangwa kwenda Azam Complex, Chamazi kucheza michezo yao dhidi ya Lipuli na Prisons.

Lakini Bodi ya Ligi wamebadili tena ratiba hiyo kidogo kwa kuwarudisha Simba Uwanja wa Uhuru kucheza dhidi ya Lipuli.

Licha ya Simba kurejeshwa Uhuru, lakini wangejisikiaje kuutumia Uwanja wa Azam kama uwanja wao wa nyumbani? Nafikiri inatia aibu na kuumiza.

Nadhani hata kwa Yanga itakuwa hivyo hivyo, klabu  hizo zimekosa viwanja tangu enzi za kusaka Uhuru, ingawa tunaambiwa kwamba Yanga ilikuwa inatumia uwanja wake wa  Kaunda kwa michezo yake ya nyumbani.

Hata Ulaya, kuna timu ambazo hazina viwanja binafsi, lakini zimekuwa zikitumia viwanja vya Serikali kama mali yao. Hiyo ni mipango thabiti ambayo klabu imejiwekea kupitia wadhamini wake.

Mfano kwa Manchester City ambayo wanautumia Uwanja wa City of Manchester kama uwanja wao wa nyumbani wakiuita kwa jina la Etihad.

Etihad ni kampuni ambayo imeingia mkataba wa kuidhamini Manchester City, kwa maana hiyo waliingia makubaliano na Halmashauri ya Jiji la Manchester juu ya kuumiliki uwanja huo.

Hakuna kitu kingine zaidi ya mipango thabiti ambayo inatekelezwa pande zote husika zinazoguswa na mchezo wa soka, hapa namaanisha klabu, wadhamini na halmashauri. Pande zote hizo tatu zinanufaika kupitia mpira.

Timu inanufaika kwa mgawo wa fedha unaoingia, halmashauri pia inanufaika kwa kodi ambayo inalipwa na marupurupu mengine na wadhamini pia wangenufaika kwa kupata matangazo na kuonekana kupitia matangazo ya televisheni.

Manchester City ni mfano tu wa klabu  zinazomiliki viwanja kupitia makampuni, Hiyo inadhihirisha kuwa kuna klabu nyingi hazina viwanja si tu Tanzania hata  Ulaya lakini zinajiendesha kwa mfumo huo wa makampuni.

Simba na Yanga ingekuwa rahisi pia kwao kutumia mfumo huo, sababu wana uwezo huo kutokana na mashabiki waliokuwa nao. Wakati mwingine wadhamini wanaweka udhamini wao kutokana na wingi wa mashabiki.

Klabu hizi mbili zinashindwa kutumia rasilimali watu walizonazo kupata udhamini na mambo mengine. Inawezekana mipango hiyo wanayo lakini kutokuwa makini na vipengele vya mikataba imekuwa ikiwagharimu na mwisho wa siku hutokea mikataba kuvunjwa na makampuni kukacha kuwadhamini.

Hakuna weledi wa ufuatiliaji wa mambo mazuri zaidi ya viongozi kujinufaisha kwa masilahi binafsi ambayo mara nyingi yamekuwa yakidumaza maendeleo ya mpira wa nchi hii.

Naamini Simba na Yanga zina sura ya aibu pindi zinapoingia Uwanja wa Azam Complex kuutumia. Hakuna njia nyingine zaidi ya kupanga mipango yao vizuri na kujenga viwanja vyao kuepuka kelele hizi ambazo zinapigwa kuhusu wao.

Endapo hilo likifanikiwa kwa namna moja au nyingine hata mpira wa Tanzania utapiga hatua kubwa kuelekea mbele tofauti na hivi sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles