24.7 C
Dar es Salaam
Saturday, April 13, 2024

Contact us: [email protected]

POLISI WADAIWA KUJERUHI WATOTO KWA RISASI, BOMU

Na PENDO FUNDISHA -MBEYA

WATOTO wawili kutoka katika jamii ya wafugaji wilayani Mbarali, wanadaiwa kujeruhiwa kwa kupigwa risasi na bomu la machozi na polisi waliokuwa wanajaribu kuwaondoa baada ya kudaiwa kuvamia skimu ya umwagiliaji ya Mapogoro kwa ajili ya malisho.

Mganga Msaidizi wa Hospitali ya Mission Chimala, Peter Seif, akizungumza na waandishi wa habari, alithibitisha kuwapokea majeruhi wawili juzi saa moja jioni ambao alisema mmoja ana matundu mawili mguu wa kushoto linaloonyesha risasi ilipita wakati mwingine alishambuliwa na kitu chenye ncha kali.

Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Henry Likaranga (16) ambaye anadaiwa kujeruhiwa kwa risasi na Duka Sakana (17) ambaye inadaiwa alishambuliwa kwa bomu la machozi na kwamba hali zao zinaendelea vizuri licha ya kwamba Likaranga alipoteza damu nyingi kutokana na jeraha la risasi.

Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune, akizungumza kwa njia ya simu alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, ambapo alisema watoto hao waliingia katika skimu ya umwagiliaji ya wakulima wadogo wa mpunga kinyume na utaratibu.

Alisema juhudi za polisi kuwataka waondoke zilishindikana na ndipo wakalazimika kutumia bomu la machozi na risasi na kuwajeruhi watoto hao ambao wamelazwa Hospitali ya Mission Chimala kwa matibabu.

Mwenyekiti wa skimu hiyo, Mgaya, alisema baada ya kupata taarifa kuwa kuna kundi la ng’ombe linazagaa kwenye skimu yao, alikwenda polisi kutoa taarifa na kupewa askari watano na akiwa mbele kwenda kuwaondoa akasikia taarifa kuwa polisi wamejeruhi watoto wawili.

Mwenyekiti Kijiji cha Kapunga, Brighton Mwinuka, alisema kwa mujibu wa utaratibu skimu hiyo ya mapogoro iliyopo Kitongoji cha Ofisini Kata ya Itamboleo, imezuiwa kuingiza mifugo, hata hivyo alisema wao wanashangazwa na tukio hilo kwa kuwa utaratibu wa kiserikali haukufuatwa.

Alisema kukiwa na operesheni, wao wanataarifiwa na uongozi unatoa askari wa mgambo kwa ajili ya operesheni husika. “Sisi tumesikia tu na tunashangaa ni utaratibu upi ulifuatwa kwenda kuwabeba askari na kufanya walichofanya wakati hatuelewi kinachoendelea,” alisema.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ofisi, alisema ofisi yake haikuwa na taarifa kama kuna uvamizi katika skimu ya Mapogolo wala operesheni inayofanyika kuwaondoa wavamizi, lakini walichosikia ni kupigwa risasi kwa watoto.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohamed Mpinga, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo kwa njia ya simu, msaidizi wake alisema kiongozi huyo yupo kwenye kikao na hivyo atafutwe baadaye.

Hata hivyo, waandishi walipofika hospitalini walikutana na zuio la polisi wa Kituo cha Polisi Chimala, ambaye aliwaeleza waandishi kuwa hawawezi kuzungumza na majeruhi hao kwa kuwa mkuu wake wa kituo hajawaambia kuwa kuna watu watawahoji majeruhi na kwamba hata polisi bado hawajawahoji.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles