27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 12, 2024

Contact us: [email protected]

Simba yamrejesha Mgosi

mgosiNA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM

TIMU ya Simba imeendelea kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), safari hii imemrejesha mshambuliaji wake wa zamani, Musa Hassan Mgosi, huku ikimnasa pia kipa wa JKU ya Zanzibar, Mohammed Abrahman Mohammed.

Mgosi, aliyeichezea Mtibwa Sugar msimu uliopita, alitemwa kwenye kikosi hicho msimu wa 2010/11 na kutimkia DC Motema Pembe ya DRC, kabla ya kurejea tena nchini.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, alisema wamempa mkataba wa mwaka mmoja mshambuliaji huyo baada ya kuridhishwa na uwezo wake aliouonyesha msimu uliopita wa ligi uliomalizika Mei 9, mwaka huu.

“Mgosi kwa sasa ni mchezaji wetu, hatujakurupuka kwenye usajili wake, tumezingatia uwezo wake aliouonyesha msimu uliopita na pia ni mchezaji mzoefu ambaye atatusaidia kuwaongoza wachezaji wetu vijana,” alisema.
Simba msimu uliopita walimrejesha mkongwe wao mwingine, Shaban Kisiga, ambaye alionyesha utovu wa nidhamu uliopelekea kutemwa. Akizungumzia kama suala hilo linaweza kujirudia kwa Mgosi, Hans Poppe, alisema: “Mgosi tunamwamini sana, hawezi kufanya hivyo na hana tabia za utovu wa nidhamu, tunamfahamu vizuri na yeye ametuahidi kufanya mambo mazuri.”
Hans Poppe alisema kipa wa JKU, Mohammed, yeye amesaini mkataba wa miaka miwili, amedai wamemchukua ili kuimarisha zaidi kikosi chao, hasa eneo hilo la ulinzi.

Mohamed anaungana na makipa wengine wa timu hiyo, mkongwe Ivo Mapunda, Hussein Shariff ‘Casillas’ na Manyika Peter Jr katika kuwania namba kwenye nafasi hiyo, lakini inadaiwa huenda Simba ikamtema Casillas, kutokana na makali yake kwisha.

Katika hatua nyingine, Kamanda huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), alisema bado wanaendelea na mazungumzo ya mwisho na mshambuliaji Laudit Mavugo, raia wa Burundi, huku akidai kwa sasa wanamsubiri mshambuliaji mwingine, Malimi Busungu, akubaliane na ofa waliyomwekea ili waingie naye mkataba.

Usajili huo wa Mgosi na Mohamed umefanya idadi ya wachezaji wapya waliosajiliwa na timu hiyo kufikia watano, baada ya awali kuwasajili kiungo Peter Mwalyanzi (Mbeya City) na mabeki Mohamed Faki (JKT Ruvu) na Samih Haji Nuhu, aliyekuwa akiichezea Azam FC msimu wa 2013/14.
Wakati huo huo, habari zilizolifikia gazeti hili wakati linakwenda mitamboni, zilidai kuwa uongozi wa Simba ulikuwa na kikao kizito na winga wao, Ramadhan Singano ‘Messi’, ili kumaliza suala la mgogoro wa mkataba wake ili asaini mkataba mpya.
Messi anadai amemaliza mkataba wake wa miaka miwili aliosaini mwaka juzi, lakini uongozi wa Simba unadai unakwisha mwakani, kwani nakala ya mkataba waliokuwa nao unaonyesha alisaini mkataba wa miaka mitatu, jambo ambalo winga huyo amepinga na kusema mkataba huo umeghushiwa.
Alipoulizwa Hans Poppe kuhusu kikao hicho, alisema: “Sitambui kikao hicho wala siwezi kufanya kitu na Messi, labda viongozi wengine wamemwita, ila mimi siwezi kufanya hivyo kwa mtu ambaye si mwelewa.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles