23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wasira, Mwigulu nao wajitosa urais CCM

MWIGULUWASIRA muda huuHEKAHEKA za kuwania kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea urais zinazidi kupamba moto baada ya makada wengine wawili, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba kutangaza kujitosa katika mbio hizo jana.
Wakati Wasira akitangaza kuhakikisha analeta mageuzi mpya kwa taifa, Mwigulu ameahidi Watanzania kuumiliki uchumi.
Wasira ambaye ni Mbunge wa Bunda, amekuwa ni kada wa pili huku Mwigulu akiwa wa tatu kutangaza nia ya kuwania uteuzi wa CCM, wakitanguliwa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, aliyetangaza juzi jijini Arusha.
Akitangaza uamuzi wake jana katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Mwanza, Wasira alisema kiu kubwa aliyonayo ni kuhakikisha utawala wake unafanya marekebisho makubwa endapo CCM itamteua kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25.
Alisema moja ya marekebisho ambayo atayafanya ni kutokuwa na huruma dhidi ya walarushwa pamoja na kulinda na kutetea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa nguvu zote.
“Nikipewa ridhaa ya kuongoza nitaanza kupambana na rushwa ambayo imeota mizizi kuanzia vijijini hadi ngazi ya taifa. Kuficha ukweli wa tatizo ni sawa na kuficha ugonjwa, mtu anayetaka kuwa rais lazima ajue matatizo ya watu wake.
“Lazima mnipime hata mie ninayezungumza haya, mtu aliyeajiriwa, hata kuandika barua ya mwanakijiji analazimisha rushwa. Katika sehemu ambazo zinalalamikiwa kama vile hospitali, mahakama hali si nzuri…halina kificho, nitahakikisha nasimamia hili ili kila chombo kitimize wajibu wake kwa mujibu wa sheria zilizowekwa,” alisema Wasira.
Alisema kuna kila sababu ya kuitisha mjadala wa kitaifa ambao utajikita kujadili na kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.
“Tunahitaji kuwa na mjadala wa kitaifa juu ya tatizo hili…nasema haya kwa sababu nimekuwa na rekodi nzuri katika utendaji kazi wangu, sijawahi kuhusika au kuhusishwa na kashfa zote zilizojitokeza katika awamu zote nne za utawala wa nchi hii,” alisema.
Alizitaja kashfa hizo kuwa ni sakata la uchotwaji wa fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow na akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na nyingine ambazo zimewahi kutikisa taifa.
“Usafi wangu huu ni moja ya sifa ambayo imesukuma kuingia kwenye kinyang’anyiro, siku moja Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliniuliza wewe Wasira unataka kuongoza au utajiri, nilipata tabu sana kumjibu…lakini nikajibu nikasema nataka kuongoza, akacheka. Hivi tujiulize jamani, mtu una mshahara tu hauwezi kukufanya uwe tajiri?” alisema na kuhoji Wasira.

MUUNGANO
Kwa upande wa Muungano, Wasira alisema endapo akiingia madarakani atahakikisha unalindwa kwa nguvu zote na kwake ni suala la kufa na kupona.
“Nawahakikisha moja ya vipaumbele vyangu ni kuhakikisha Watanzania wanakuwa wamoja ndani ya Muungano ulioasisiwa na wazee wetu,” alisema.

WIZI SERIKALINI
Kuhusu wizi uliota mizizi, licha ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kutoa ripoti, Wasira alisema endapo akichaguliwa atahakikisha mkaguzi huyo anapewa mamlaka zaidi.
“Sitakuwa na mjadala na wezi, tutamwezesha mno CAG ili hatua kali zichukuliwe… hatuwezi kuona haki ya Watanzania wengi inachukuliwa na watu wachache…hakuna mtu atakayesamehewa…tutafuata utawala wa sheria,” alisema Wasira.

RASILIMALI
Wasira alisema atahakikisha anasimamia rasilimali kama madini, gesi, wanyamapori na vingine ili Watanzania wote wafaidi.
“Tunataka kuona rasilimali zetu zinawasaidia wananchi kuondoa tatizo la umasikini, kwa mfano wale wanaozungukwa na migodi wanawezeshwa kupata migodi midogo midogo na makampuni ya wazawa yashirikishwe vizuri,” alisema Wasira.

ULINZI
Alisema kama akifanikiwa kuwa rais na amiri jeshi mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama, atahakikisha anaimarisha utendaji kazi wa vyombo vya dola, likiwamo Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Polisi.

ELIMU
“Suala la elimu ni la kuchukua hatua na si kulalamika, lazima tuwekeze elimu ya sayansi kwa sababu inaendesha dunia…hata hiki kipaza sauti ninachotumia ni kazi ya sayansi,” alisema.

SERA
Alisema kama akiteuliwa kuwa mgombea wa nafasi hiyo na kushinda, ataelekeza nguvu zake katika kuisimamia
Tanzania ili ibaki imara, yenye amani na umoja kama ilivyo sasa.
Kwamba atahakikisha taasisi zote muhimu za Serikali hasa mihimili mitatu ya kikatiba (Serikali, Mahakama, Bunge) zinaimarishwa na kuwezeshwa ili zitekeleze majukumu yao sahihi kwa mujibu wa katiba.

DIRA
Akizungumzia juu ya dira ya maendeleo kwa uongozi wake wa awamu ya tano kama atashinda, ni kuanza kujenga kwenye mafanikio ya Serikali ya awamu ya nne ilipoishia ili kuimarisha uchumi imara na wenye kuleta ushindani.

KILIMO VIJIJINI
Wasira alisema Serikali yake itahakikisha jembe la mkono linapelekwa katika Jumba la Taifa la Makumbusho na kujikita katika kilimo cha teknolojia.
“Nimeanza safari ya kulipeleka jembe la mkono katika Jumba la Taifa la Makumbusho, safari hii haitasubiri mpaka niwe rais la hasha, nitaianza sasa hivi nikiwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika,” alisema.

AJIRA
Alisema kwa mujibu wa takwimu kutoka Wizara ya Kazi na Ajira, karibu vijana milioni moja wanaingia katika soko la ajira nchini.
Wasira alisema takribani vijana 200,000 tu ndio wanaoajiriwa kila mwaka na kuongeza kuwa uwiano huo ni mbaya sana ambao kama hautashughulikiwa unaweza kusababisha matatizo ya kijamii na kisiasa.

AFYA
Alisema bado kuna tatizo kubwa katika sekta ya afya kutokana na rushwa kukithiri kwenye sekta hali inayofanya wananchi kukosa huduma bora.

MIUNDOMBINU
Wasira alisema Tanzania inahitaji miundombinu kuanzia vinu vya kufulia umeme hadi mifumo ya usambazaji maji safi, viwanja vya ndege, bandari, mitandao ya barabara, reli na mawasiliano ya simu ili kupata maendeleo.

KUHAMIA NCCR-MAGEUZI
Kuhusu swali la kwamba Wasira alitokea upinzani kwenda CCM, alijibu kuwa alibaini alikuwa amepanda gari bovu ambalo limepata ajali, hivyo aliamua kuondoka na hatothubutu kurudi huko kwani ni sawa na kutafuta ajali nyingine.

MWIGULU: NITAWAVUSHA WATANZANIA
NAIBU Waziri wa Fedha, Nchemba, ametangaza nia rasmi ya kugombea urais na kuahidi kuwa atawavusha Watanzania kutoka katika utegemezi na kuwapeleka katika uchumi wa kujitegemea.
Alitangaza nia hiyo katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere uliopo Chuo cha Mipango mjini Dodoma, alisema Watanzania wanayo ajenda inayowagusa na kwamba rais ajaye ni yule atakayeibeba.
Mwigulu ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi, alisema ametafakari na kutathimini ajenda ya Watanzania kwa sasa kwamba ni umasikini, hivyo amewaomba wamwamini na wamuunge mkono.
“Jambo kubwa la msingi ni ajenda ya Watanzania, nayatambua matatizo yao mimi ninatokea familia ya wafugaji ambaye nimeishi katika maisha magumu, umasikini sijaujua kwa kuusoma vitabuni, bali kwa kuuishi. Sipingi umasikini kwa niaba ya Watanzania isipokuwa umasikini ni jambo linalonihusu,” alisema.
Akizungumzia sababu ya kutangaza nia yake mkoani Dodoma, Mwigulu alisema: “Nimeona kuna mazingira ya watu kuanza umimi, ukwetu-kwetu. Kwa kuwa hili jambo ninalotafuta ni la kitaifa, hivyo nimeona nitangazie hapa Dodoma ambako ni makao makuu ya chama na Serikali, na kama nikishinda nitaapishwa hapa hapa na hapo ndiyo itakuwa mwanzo wa Serikali kuhamia Dodoma,” alisema.

UCHUMI
Alisema kwa zaidi ya miaka 50 sasa taifa limekuwa tegemezi, hivyo awamu ya tano itafungua ukurasa mpya kwa kuipeleka nchi katika uchumi wa kati kwa miaka 50 ijayo.
Ili kufikia mafanikio hayo, Mwigulu alisema Serikali yake itatekeleza Azimio la Maputo ambalo linazitaka Serikali za nchi za Afrika kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya kuinua sekta ya kilimo.

UTITIRI WA KODI
Mwigulu pia alionyesha kusikitishwa na kitendo cha upendeleo katika suala zima la ulipaji wa kodi, ambapo wafanyabiashara wakubwa wamekuwa wakipewa likizo ya kodi kwa muda mrefu huku wananchi wanyonge wakikamuliwa.
“Tunakwenda kuondoa utitiri wa kodi na tozo mbalimbali zisizowiyana na huduma inayotolewa. Haiwezekani mfanyabiashara mkubwa anapewa likizo ya kodi, halafu kijana amefungua saluni ndiyo kwanza anapaki rangi anapigwa nyundo ya kodi,” alisema.
RUSHWA
Kuhusu rushwa, Mwigulu alisema Serikali atakayoiongoza inakwenda kuitaja rushwa kama janga maalumu litakaloshughulikiwa kama jambo maalumu.
Alisema Serikali yake itabadilisha sheria namba 11 ya mwaka 2007 iliyounda Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ili kuipa mamlaka taasisi hiyo kufanya uchunguzi na kuwafikisha wahalifu mahakamani bila kuwapeleka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

UZOEFU
Mwigulu alibeza hoja za uzoefu, ujana na uzee zinazohubiriwa kama sifa mojawapo ya kuwa kiongozi wa nchi, akisema huko ni kufilisika kimawazo.
Alisema ujana peke yake wala uzee peke yake havitoshi kuwa sifa za kiongozi wa nchi, isipokuwa jambo la msingi ni uwezo, uaminifu, uadilifu na uzalendo kwa taifa.

KEKI YA TAIFA
Mwigulu alisema iwapo atafanikiwa kushinda, Serikali yake haitakuwa tayari kuona baadhi ya wananchi wanafaidika na keki ya taifa na wengine wakipiga miayo.
HUDUMA ZA JAMII
Kuhusu huduma za jamii, Mwigulu alisema Serikali yake itahakikisha inadhibiti mianya ya upotevu wa fedha ili ziende kutumika kuboresha huduma za jamii.

MUUNGANO
Mwigulu alisema atahakikisha anasimamia Muungano uliopo, kwani ni wa watu na si vitu.
Katika mkutano huo walikuwapo baadhi ya wabunge wakiwamo, Asumpta Mshama (Nkenge), Omar Badwel (Bahi), Modestus Kilufi (Mbarali), Abdalla Sharia (Dimani), Martha Mlata, Maria Hewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Iramba.
Mwigulu aliingia ukumbini humo saa saa 9:40 alasiri akiwa ameongozana na familia yake ambapo watu walisimama na kumshangilia na kupeperusha bendera za taifa.

Habari hii imeandaliwa na Patricia Kilemeta na Benjamin Masese (Mwanza), Khamis Mkotya na Arodia Peter (Dodoma)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles