30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Membe aliaga Bunge

Na Arodia Peter, Dodoma
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe jana aliliaga rasmi Bunge na kusema hotuba yake ya bajeti ni ya mwisho akiwa kama Mbunge wa Mtama mkoani Lindi.
Akiwasilisha hotuba yake ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa bungeni jana, Membe pia alisema hotuba yake hiyo ni ya mwisho kama waziri katika wizara hiyo, lakini atahakikisha mrithi wake wa ubunge anatoka CCM ili warudi wote.
Ingawa Membe hakufafanua atarudi wapi na njia gani, lakini aliwaahidi wabunge kukutana katika nafasi nyingine.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wamehusisha kauli hiyo na nia yake ya kutaka kugombea urais baada ya Rais Jakaya Kikwete kustaafu Oktoba mwaka huu.
“Hii ni hotuba yangu ya mwisho nikiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ninachukua fursa hii kuwaaga wananchi wa Mtama niliowatumikia kwa miaka 15 na ninahidi kumsaidia mgombea ubunge wa CCM, ili turudi wote,” alisema Membe na kushangiliwa na wabunge.

Katika hotuba yake, Membe alizungumzia masuala mbalimbali ikiwamo mgogoro wa Burundi ambapo alisema viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanatarajia kukutana kesho Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili msimamo wa Burundi wa kuendelea na uchaguzi wakati bado nchi hiyo ikiwa kwenye machafuko.

“Kwa kipindi cha miezi miwili sasa hali ya kisiasa nchini Burundi imeendelea kudorora kutokana na uamuzi wa chama tawala cha CNDD-FDD kumtangaza Pierre Nkurunziza kugombea urais katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Juni 26,2015.

“Uamuzi huo ulisababisha vurugu na maandamano makubwa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Bujumbura na maeneo ya jirani na kusababisha vifo na watu wengine kukimbia nchi yao” alisema Membe.

Membe alisema baada ya machafuko kutokea Mei 6 mwaka huu na jaribio la kutaka kumuondoa madarakani, Rais Nkurunziza, Rwanda ilipokea wakimbizi wasiopungua 150,000 huku Tanzania ikipokea wakimbizi 51,000.

“Tanzania tunaamini amani ya Burundi ni amani ya Tanzania kwa hiyo tutawasaidia kwa lolote lile ili kuhakikisha amani ya Burundi inarejea,” alisema.

Aidha, katika hotuba yake, Membe pia alisema mpaka wa Tanzania na Malawi kwenye Ziwa Nyasa bado upo kwa msuluhishi na halijapatiwa ufumbuzi.
Alisema katika mkutano wa mwisho uliofanyika Machi 2014, pande zote mbili pamoja na msuluhishi walikubaliana kuwa mchakato huo usogezwe mbele mpaka baada ya uchaguzi mkuu nchini Malawi uliofanyika Juni 2014.

Wapinzani wahoji urafiki
Tanzania, Msumbiji

Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikianio wa Kimataifa, Ezekia Wenje alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na kile cha Msumbiji, FRELIMO, wameamua kutumia serikali za vyama vyao kuanzisha ushirikiano wa haraka hadi kufikia hatua ya kuacha mipaka huru.
“Mheshimiwa Spika, mbinu hiyo chafu imeshtukiwa huko Zanzibar ambapo inasadikiwa kwamba raia wa Msumbiji wanaandikishwa katika kambi za jeshi na kupewa vitambulisho vya ukaazi ili waweze kupiga kura katika uchaguzi wa Zanzibar.

“Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya upinzani bungeni tunaitaka serikali kulieleza Bunge hili kuna fursa gani za kiuchumi zilizogundulika Msumbiji hadi kuondoa masharti ya viza mbazo hazikuwepo tangu utawala wa baba wa taifa, Mwalimu Nyerere”alihoji Wenje.

Wenje ambaye pia ni Mbunge wa Nyamagana, (Chadema), alitaka serikali kujifunza kwa nchi mbalimbali duniani zilizofanya uchaguzi ambapo vyama tawala vilikubali kushindwa na hivyo kuwezesha upinzani kuchukua madaraka ya dola bila kumwaga damu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles