27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA YAFUNGA MWAKA KIBABE

WINIFRIDA MTOI-DARE ES SALAAM

TIMU ya Simba imeendelea kujizolea pointi tatu Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, baada ya jana kuichapa Ndanda mabao 2-0, katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo wa Simba ni kama salamu kwa Mtani wake wa Jadi Yanga, ambaye itaumana naye Jumamosi hii, katika mchezo wa Ligi Kuu utakaochezwa kwenye uwanja huo.

Mabao ya Simba yalifungwa na kiungo, Francics Kahata dakika ya 13, kabla ya Deo Kanda kufunga bao la pili dakika ya 85.

Ushindi huo unaifanya Simba kuendelea kujitika kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo,  ikifikisha pointi 34, baada ya kucheza michezo 13, ikishinda 11, sare mmoja na kupoteza mmoja.

Kipigo hicho kinaiacha Ndanda katika nafasi ya 19 na pointi zake nane, baada ya kushuka dimbani mara 14, ikishinda mmoja, sare tano na kupoteza nane.

Simba ilianza mchezo huo kwa kasi ikimiliki zaidi mpira na kusukuma mashambulizi ya kasi kwenda lango la Ndanda, ambayo ilionekana kupanga mipango yake taratibu.

Dakika ya 13, Kahata alindikia Simba bao la kwanza kwa mkwaju wa adhabu ndogo uliomshinda kipa wa Ndanda, Ally Mustafa ‘Bartez’.

Dakika ya 18, Bartez alifanya kazi ya ziada kupangua mkwaju mkali uliopigwa na Ibrahim Ajib na kuzaa kona ambayo hata hivyo haikuzaa matunda.

Dakika ya 25, Ajib alipoteza nafasi ya wazi ya kuifungia Simba bao la pili, baada ya kupokea pande safi kutoka kwa Haruna Shamte akiwa ndani ya eneo la hatari la Ndanda, lakini shuti lake lilishindwa kulenga lango.

Dakika ya 32, Bartez alisimama imara na kudaka shuti kali la mbali lililopigwa na beki wa kushoto wa Simba, Gadiel Michael.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilikamilika kwa Simba kwenda mapumziko ikiwa kifua mbele kwa bao 1-0.

Simba ilitawala zaidi mchezo wa kipindi cha kwanza kwa kumiliki mpira na kuinyima kabisa nafasi Ndanda ya kulisogelea lango lao na kufanya mashambulizi.

Dakika ya 57, Kocha wa Simba, Sven Vanderbroec alifanya mabadiliko kwa kumtoa Kahata na kumwingiza Deo Kanda.

Dakika ya 65, Simba ilifanya mabadiliko mengine alitoka Jonas Mkude na kuingia Mzamiru Yassin.

Dakika ya 74, Kocha wa Ndanda, Abdul Mingange alifanya mabadilikio alimtoa Nassoro Salehe na nafasi yake kuchukuliwa na Omar Ramadhani kabla ya

dakika ya 78 Ajib kutoka na kumpisha Clatous Chama.

Dakika ya 85, Kanda alindikia Simba bao la pili, baada ya kumalizia krosi ya Gadiel Michael.

Dakika ya 87, mwamuzi wa mchezo huo,  Omari Mdoe alimlima kadi ya njano beki wa Simba, Erasto Nyoni, baada ya kupinga uamuzi wake.

Dakika 90 za mtanange huo zilikamilika kwa Simba kuvuna pointi tatu na mabao 2-0 dhidi ya Ndanda.

Kipute kingine cha ligi hiyo kilikuwa katika dimba la Kambarage, Shinyanga ambapo wenyeji, Mwadui walishindwa kufurukuta nyumbani, baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na KMC.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles