Theresia Gasper – Dar es Salaam
KIKOSI cha kimetua mkoani Morogoro, kikisubiri kuuamana na wenyeji wao, Mtibwa Sugar, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa kesho Uwanja wa CCM Gairo mkoani humo.
Simba itaikabili Mtibwa, ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kuchapwa bao 1-0 na timu ya JKT Tanzania inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa(JKT), mchezo uliotimua vumbi Ijumaa iliyopita Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Kwa upande mwingine, Mtibwa itaingia uwanjani ikiwa na jeraha, baada ya kulazwa bao 1-0 na wageni wao Lipuli, dimba la Gairo.
Kikosi cha Simba kiliondoka jijini Dar es Salaam jana yalipo maskani yake kwenda Morogoro ambako inapatikana Mtibwa.
Kocha Mkuu wa Simba, Sven VandenBroeck, alisema anatarajia mchezo huo utakuwa na ushindani mkubwa kutokana na uimara wa kikosi cha Mtibwa.
“Tunahitaji kufanya vizuri zaidi katika mechi zetu ukizingatia tunakutana na timu ambazo zimejipanga vizuri na wanakuwa wanakamia sana hivyo umakini unahitajika zaidi,” alisema.
Alisema katika mchezo uliopita dhidi ya JKT Tanzania timu yake ilikuwa na matatizo katika safu ya viungo, lakini kabla ya kukutana na Mtibwa atahakikisha anayatafutia tiba.
VandenBroeck alisema hapendezwi kuona timu yake inapoteza mchezo kwa mara nyingine, hivyo amewataka wachezaji wake kujitolewa ili kuipa matokeo mazuri timu yao.
Simba imeifuata Mtibwa pasipo nyota wa timu hiyo Deo Kanda, Erasto Nyoni, Miraji Athumani ambao wana majeraha.
Wakati Vandenbloeck akisema hayo, Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila amesema wanataka kuendeleza ubabe wao dhidi ya Wekundu hao.
Ikumbukwe kwamba, Mtibwa iliitambia Simba kwa kuilaza bao 1-0, timu hizo zilipokutana katika mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi, michuano iliyofanyika Januari , mwaka huu visiwani Zanzibar.
Simba inaogoza msimamo ikiwa na pointi 50, baada ya kushuka dimbani mara 20, ikishinda michezo 16, sare mbili na kuchapwa mara mbili.
Mtibwa inakamata nafasi ya 10 ikiwa na pointi 23.