23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Simba katika hesabu kali leo

simba-line-upNA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

TIMU ya Simba ipo katika hesabu kali za kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara leo, wakati itakapocheza dhidi ya timu ya Ndanda FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba itaingia uwanjani ikiwa na  kumbukumbu ya kuongoza Ligi Kuu  kwa saa 48 ikiwa na jumla ya pointi 48 baada ya kucheza michezo 21 sawa na  Yanga  iliyorejea kwenye nafasi hiyo kwa kuwa na pointi 50.

Vijana wa Msimbazi wataingia uwanjani wakifahamu kabisa kuwa si rahisi kuifunga Ndanda licha ya kupata ushindi wa bao 1-0 Januari mosi mwaka huu, kwenye mchezo wao wa mzunguko wa kwanza.

Kwenye mchezo wa leo kocha mkuu wa timu ya Simba, Jackson Mayanja, anatarajia kuingia uwanjani kifua mbele akiwa na matumaini ya ushindi kwa kutumia mfumo wa 4-3-3 ambao umempa ushindi kwenye michezo mitano kati ya sita ya mzunguko wa kwanza.

Zaidi ni kwamba hakuna majeruhi waliopatikana hadi sasa kwenye kikosi hicho, hivyo kocha huyo anapata uhakika wa kuwatumia vema washambuliaji wake mahiri, Ibrahim Ajib, Hamis Kiiza na Danny Lyanga.

Naye Kocha wa Ndanda, Abdul Mingange, anafahamu ugumu uliopo kwenye mchezo huo licha ya kutoa sare ya 0-0 dhidi ya Toto Africans katika mchezo wake wa mwisho akiwa ugenini.

Ndanda ipo nafasi ya nane ikiwa na pointi 24 baada ya kucheza michezo 21, katika michezo sita iliyopita timu yake iliweza kupata sare michezo mitatu na kufungwa mitatu.

Mingange ataingia uwanjani akiwa na tahadhari juu ya mabeki wake ambao wameruhusu kufungwa mabao 20 ambayo ni mengi ukilinganisha na wapinzani wao, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 19 kwenye michezo yote tangu ligi ianze.

Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo, Mbeya City inachuana vikali na Stand United katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Hata hivyo, kiungo mahiri wa Mbeya City, Haruna Moshi ‘Boban’, anasumbuliwa na ugonjwa wa malaria hali itakayomfanya kuwa nje ya uwanja hadi Machi 14, mwaka huu na kuukosa mchezo wa kesho dhidi ya Stand United.

Pia Mbeya City watamkosa kiungo wa kati, Kanny Mwambungu, ambaye ana kadi tatu za njano pamoja na beki, Deo Julius, anayesumbuliwa na majeraha ya goti.

Mbeya City wanakutana na wapinzani wao Stand United kesho kwa mara ya nne katika Uwanja wa Sokoine huku wakiwa na rekodi ya kufungwa mara mbili nyumbani na kushinda mechi moja.

Katika hatua nyingine, timu ya Tanzania Prisons jana imeshindwa kutamba katika uwanja wake wa nyumbani Sokoine, Mbeya baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Kagera Sugar.

Mbali na mchezo huo, timu ya JKT Ruvu iliibuka kidedea baada ya kuwanyuka Toto Africans mabao 2-1, mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Mabatini,  Mkoa wa Pwani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles