TIMU ya soka ya Simba imeendeleza wimbi la ushindi baada ya kuifunga timu ya Mwadui mabao 3-0 katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, iliyochezwa katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Mabao ya Simba katika mechi hiyo yalifungwa na Shiza Kichuya aliyefunga bao moja, huku Mohamed Ibrahim, maarufu ‘Mo’ akifunga mawili na hivyo timu hiyo kuendelea kuongoza ligi hiyo.
Mechi hiyo ilianza kwa kasi, huku timu hizo zikisomana kwa mashambulizi ya kushtukiza na kadri dakika zilivyokwenda ndivyo mechi ilivyokuwa ikiongezeka kasi.
Simba walikuwa wa kwanza kufika langoni mwa wapinzani wao katika dakika ya tano, ambapo Laudit Mavugo aliwachambua mabeki wa Mwadui na kuachia shuti lililopaa juu, huku akishindwa tena kutumia nafasi kama hiyo katika dakika ya saba.
Baada ya kuona Simba wanakuja juu, Mwadui walianza kupanga mashambulizi na katika dakika ya 14 Rashid Ismail aliachia shuti lililopaa juu ya lango la Simba, huku katika dakika ya 25 Kichuya akishindwa kuunganisha kwa kichwa krosi ya Mavugo na mpira kupaa juu.
Baada ya kuona muda unakwenda, Simba walitulia na kupanga mashambulizi na kufanikiwa kupata bao katika dakika ya 32, lililofungwa na Mohamed Ibrahim, baada ya kupokea pasi ya Mavugo kutoka winga ya kushoto.
Bao hilo liliwashtua Mwadui, ambao walianza kulinyemelea lango la Simba ambapo katika dakika ya 34 nusura wajipatie bao, baada ya kipa Vincent Angban kutaka kudaka mpira ulioruka juu na kumgonga kwenye paji la uso na kuokolewa na Method Mwanjale.
Katika dakika ya 35 Mzamiru Yassin alikosa nafasi ya wazi ya kuipatia Simba bao la pili, baada ya kushindwa kuunganisha pasi ya Mwinyi Kazimoto, ambapo lango lilikuwa wazi akataka kupiga na mpira ukampita kirahisi.
Simba walijiandikia bao la pili katika dakika ya 45 kupitia kwa Shiza Ramadhan Kichuya, akiunganisha pasi ya Mohamed Ibrahim, aliyeipiga kutoka winga ya kulia na kuzifanya timu hizo kwenda mapumziko ‘Wekundu wa Msimbazi’ wakiwa mbele kwa mabao mawili.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, Mwadui wakitaka kusawazisha, huku washambuliaji wao wakiongozwa na Paul Nonga, wakifanya kazi kubwa, lakini ukuta wa Simba uliokuwa chini ya Jjuuko Murshid, ulisimama imara.
Simba walijipatia bao la tatu katika dakika ya 50 kupitia kwa Mohamed Ibrahim, baada ya kupokea pasi kutoka kwa Ame Ally, aliyeingia kuchukua nafasi ya Mavugo.
Katika dakika ya 70 Mwadui walifanya shambulizi zuri, lakini shuti la Paul Nonga lilishindwa kulenga na kujaribu tena katika dakika ya 79 na shuti kushindwa tena kulenga goli.
Katika dakika ya 80 Mzamiru Yassin alishindwa kuunganisha mpira kwa kichwa kutokana na krosi ya Ame Ally, ambapo hadi dakika 90 zinamalizika Simba waliibuka na ushindi huo wa mabao 3-0 na hivyo kufikisha pointi 32, huku Kichuya akifikisha mabao nane.
Katika mechi nyingine, African Lyon imetoka sare ya bao 1-1 na Prisons katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Mwadui:
Shabani Hassan ‘Kado’, Iddy Mobby, David Luhende, Shaaban Aboma, Joram Mgeveke, Abdallah Mfuko, Salim Khamis, Morris Kaniki, Paul Nonga, Rashid Ismail na Miraji Adam.
Simba:
Vicent Angban, Janvier Bukungu, Mohamed Zimbwe, Method Mwanjale, Jjuuko Murshid, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Mwinyi Kazimoto/Said Ndemla, Laudit Mavugo/Ame Alli, Shiza Kichuya/Ibrahim Ajib, Mohamed Ibrahim.