23.9 C
Dar es Salaam
Sunday, April 21, 2024

Contact us: [email protected]

Sura ya pili ya Mfalme wa Morocco

Mfalme wa Morocco. Mohamed VI (katikati).
Mfalme wa Morocco. Mohamed VI (katikati).

NA MWANDISHI WETU,

NI vioja! Ndivyo unavyoweza kutafsiri sura ya pili wa maisha ya Mfalme wa Morocco, Mohammed VI ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku tano.

Mfalme huyo ambaye aliomba kuongezewa siku moja zaidi katika ziara yake nchini, kihistoria ndiye kiongozi wa kwanza wa taifa la Morocco kukanyaga nchini tangu uhuru.

Ametumia siku tatu kusimamia majukumu ya kikazi yaliyomleta, pia ametumia siku zilizobaki kwa mapumziko huko visiwani Zanzibar.

Tofauti na hadhi yake ya kifalme ambayo ndiyo inabeba sura nzima ya maisha yake katika ngazi ya kitaifa na kimataifa, sura ya pili ya maisha ya kiongozi huyo ni tofauti kabisa na taswira hiyo kwani imejaa vioja.

Vioja vya mfalme huyo vimeonekana wakati wa mapumziko yake visiwani Zanzibar. Picha mbalimbali zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zimemuonyesha akiwa katika maisha ya kawaida yasiyomtambulisha kama ni kiongozi wa nchi.

Moja ya picha hizo zimemuonyesha akiwa amevaa kaptula, fulana iliyokatwa mikono (car-wash) na raba, huku mkono wake wa kulia kashikilia mfuko unaoonyesha alikuwa kwenye manunuzi.

Hiyo ni tofauti na sura yake ya kwanza ya kifalme ambayo ilionekana wakati si tu anafika bali na katika dhifa ya kitaifa iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam. Alivaa majoho ya kifalme pamoja na kikofia kidogo kichwani.

Mmoja wa watu waliomshuhudia mfalme huyo katika sura yake ya pili visiwani Zanzibar, aliliambia MTANZANIA Jumapili kuwa kiongozi huyo aliingia katika mgahawa mmoja maarufu visiwani humo akiwa ameongozana na watu saba, huku walinzi wake wakibaki nje.

Alisema baada ya kuingia ndani ya mgahawa huo, aliagiza kinywaji kimoja chupa mbili na baada ya kuburudika, aligawa kiasi cha dola kwa baadhi ya wateja waliokuwapo na kisha akaondoka.

Sura hiyo ya upande wa pili wa maisha yake imemfanya mfalme huyo kuwa kivutio kikubwa, si tu visiwani Zanzibar, bali hata katika mitandao ya kijamii.

Duru zaidi zinaeleza kuwa Alhamisi iliyopita, mfalme huyo alizunguka na kufanya manunuzi ya vitu mbalimbali katika maduka kadhaa ya viunga vya mji wa Zanzibar, huku baadhi ya watu wakiomba kupiga naye picha.

Mwonekano huo unamfanya isiwe rahisi kwa yeyote kubaini kama ni mtu mweye hadhi ya juu katika ngazi ya kimataifa.

Katika uchunguzi wake, gazeti hili limebaini kuwa sura hiyo ya pili ya Mfalme Mohammed VI ni ya kawaida na imezoeleka nchini mwake na katika bara la Ulaya, ambako hupendelea kwenda mara kwa mara.

Mtandao wa PRI wa nchini Ufaransa, unamwelezea  mfalme huyo kama bingwa wa picha za ‘selfie.’

Mtandao huo unatanabaisha kuwa kiongozi huyo anapenda kupiga picha na watu wa kariba mbalimbali kwa mtindo wa selfie.

Kwamba mara nyingi anafanya hivyo pindi anapokuwa hajavaa majoho yake ya kifalme.

Mtandao huo umekwenda mbali na kumwelezea kuwa tabia yake ya kupiga picha nyingi akiwa katika sura ya pili ya maisha yake na kuziweka kwenye akaunti yake ya mtandao wa facebook, imemjengea marafiki wengi wanaofuatilia mtandao huo.

PFI inatanabaisha kuwa nje ya majoho yake ya kifalme, kiongozi huyo hupendelea kuvaa fulana na suruali za jinzi.

UTAJIRI WAKE

Kwa mjibu wa ripoti ya mwaka 2015 ya Jarida la Forbes, Mfalme Mohammed VI amekamata nafasi ya tano kati ya matajiri 50 barani Afrika.

Utajiri wake ni Dola bilioni 7. Alirithi utajiri huo kutoka kwa baba yake, Mfalme Hassan akiwa anamiliki asilimia 35 ya hisa za Kampuni ya Societe Nationale d’Investissement (SNI), ambayo inamiliki benki ya Attijariwafa, Kampuni ya madini ya Managem Group; Kampuni ya sukari ya Cosumar, na nyingine ya Centrale Danone.

ATEMBELEA NGORONGORO

Katika hatua nyingine, Mfalme Mohammed VI jana aliwasili katika Hifadhi ya Ngorongoro ambayo ni sehemu ya urithi wa dunia na moja kati ya maajabu saba ya dunia, kujionea vivutio mbalimbali vya utalii.

Mfalme huyo aliwasili katika hifadhi hiyo akitokea Zanzibar. Alitua kwa muda katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Chanzo cha kuaminika kiliiambia MTANZANIA Jumapili kwamba mfalme huyo alitua KIA akitokea Zanzibar na kisha kuendelea na safari yake Ngorongoro kwa kutumia ndege.

Safari hiyo ya Ngorongoro ni mwendelezo wa ziara yake nchini tangu alipowasili Dar es Salaam Oktoba 19, na kupokewa na mwenyeji wake Rais Dk. John Magufuli.

Ziara hiyo ya Mfalme Mohammed katika hifadhi ya Ngorongoro, inajengwa na umuhimu wa kipekee wa bonde hilo lililoanzishwa mwaka 1959, likiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 8,300.

Malengo ya ziara yake nchini ni kukuza diplomasia ya uchumi kati ya nchi hizo mbili.

Mara baada ya kumaliza ziara yake nchini, mfalme huyo anatarajiwa kuzitembelea nchi za Kenya, Rwanda na Ethiopia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles